loader
Picha

Sababu za mbwa kupata ‘mtoko’

MTOKO ni neno la Kiswahili; ni nomino ya kitendo ‘Kutoka’. Kamusi Kuu ya Kiswahili inaelezea neno kutoka kwamba ni Kuanzia; mfano, Kutoka Nairobi hadi Bujumbura bila kupumzika. Katika muktadha wa makala haya, neno ‘mtoko’ kama nilivyowahi kulitumia katika shairi langu Mbwa Apate Mtoko, lililochapishwa katika gazeti hili, Desemba 15, 2017, limekusudiwa kumaanisha kuhama mazingira fulani yaliyozoeleka na kwenda mazingira tofauti ya ugeni yanayoleta furaha, hamasa na mtizamo mpya katika maisha.

Kwa mfano, katika moja ya beti za shairi hilo ninaeleza: Mbwa hupenda upendo, Furaha na burudani, Kukiwepo na uhondo, Aingie ukumbini! Na siyo akae kando, Na kufungiwa bandani, Mitoko ya kila mara, Mbwa hupata werevu. Mbwa raha mkutane, Kisha mtoke nyumbani, Njiani msemezane, Utamu wa safarini, Na mahala mjichane, Kwa nyama za hotelini, Mitoko ya kila mara, Mbwa hupata werevu. Shairi hili linahimiza wafugaji kwenda katika mazingira tofauti na mbwa wao ili mbwa wao wapate furaha na kuwa na ari mpya ya kazi.

Matembezi ni sehemu ya mazoezi na huongeza uhusiano kati ya mbwa na mwenye mbwa. Mtoko ni muhimu, lakini imekuwa siyo desturi ya wengi kuwatoa mbwa na kwenda nao kwenye mazingira tofauti ili waweze kujifunza na kuondoa msongo wa mawazo unaosababishwa na mazingira yaliyozoeleka. Mbwa akishinda kwenye banda kwa muda mrefu bila kutolewa nje, anapata athari za kiafya, mfano miguu kupinda kwa kukosa mazoezi na ukosefu wa jua linalomsaidia mwili kupata vitamin D.

Watu wengi katika nchi za Maziwa Makuu, hawajui kutengeneza banda zuri kwa ajili ya mbwa, kwa kutokujua au mitazamo potofu mintarafu nyumba ya mbwa. Baadhi huamini kwamba, ili mbwa awe mkali, anatakiwa awekwe kwenye banda lenye giza asiweze kuona jua. Mtizamo huu siyo sahihi kwani akiwa katika mazingira hayo kwa muda mrefu, anakosa vitamini D, na kusababisha upungufu wa madini ya calcium miguu kupinda na mifupa kuvunjika kirahisi.

Mbwa anayeshinda ndani kwa muda mrefu, anakuwa mchafu, huvamiwa na wadudu kama kupe, manyoya na ngozi hulowa kila mara kutokana na majimaji yasiyokauka kwa haraka ndani ya banda. Hali hii husababisha mbwa kunuka na hatimaye kunyanyapaliwa. Katika muswada wa Kitabu Bustani ya Mbwa kilicho mbioni kuchapishwa, nimeelezea kiundani athari nyingine za mbwa kutopata mtoko kuwa ni pamoja na zile za kisaikolojia.

Hapa, mbwa anakuwa mgeni kwa vitu vya kawaida ambavyo hajawahi kuona. Kwa mfano, magari na sauti za magari, wanyama wenzake, mito, madaraja na watu. Imeandikwa: “Mbwa akipata mtoko wa mara kwa mara anapata fursa ya kuzoea vitu visivyo na madhara na kupunguza au kumaliza kabisa mihemko isiyo na sababu.”

Muswada unafafanua kiundani ukisema: “Ukiwa na mbwa kwenye mtoko, atapata fursa pana ya kujifunza tabia yako na wewe kujua zaidi tabia yake. Anakuwa na uwezo wa kutabiri mambo unayotarajia afanye. Kwa mfano; namna ya kutembea na jinsi unavyokabiliana na matukio mbalimbali ambayo kwake ni kitisho.” Mkiwa katika matembezi, ni wakati mzuri kuimarisha mafunzo ambayo mbwa alikwisha kupata hapo awali, kwa kumpa amri mbalimbali kama vile keti, simama, lala, subiri n.k.

Kitaalamu, mbwa anapopata mtoko, hujisikia vizuri, hujawa na furaha na kama ilivyoelezwa awali, huongeza uhusiano. Mkiwa barabarani, zungumza naye kwa kumuita jina azidi kulizoea na mnunulie zawadi hususani chakula. Unaweza kutumia gari katika matembezi, lakini ni muhimu ukafika mahala ukamshusha na mkazunguka kwa kutumia miguu katika viunga vya karibu. Hata hivyo, baada ya shairi hili kutoka gazetini Desemba 2017, mshairi mmoja kwa jina Ephraim Mwaluvinga (Mwalu), alipinga mbwa kupata mtoko, kwa kusema: “Huyo Atakuwa Mbwa Koko.”

Katika shairi lake, Mwalu anatoa hoja kwamba, mbwa akitoka nje ya himaya yake atakuwa koko kwa maana ya mbwa mzururaji (Japo mbwa koko maana yake ni mbwa mzururaji) na akaona ni kitendo kisichokubalika. Sababu nyingine Mwalu anasema, mbwa anaweza kupata magonjwa kwa kuchangamana na mbwa wazururaji ambao hawana uangalizi wala matibabu. Ephraim Mwaluvinga anaendelea kusema, kunaweza kutokea mapigano na mbwa koko wanaozagaa barabarani na kutokea sarakasi ya hatari.

Hoja nyingine anayowasilisha katika shairi lake, ni mbwa kuacha lindo au kazi yake ya kulinda kwa ajili ya mtoko, hali ambayo wezi wanaweza kuitumia na kufanya uhalifu. Shairi la Mwalu lilichapishwa katika gazeti la Habarileo (Desemba 17, 2017). Baada ya kulichapisha, nilimpigia simu na kusema: “Hoja zako zilikuwa nzito; umetumia weledi kuchambua athari za mbwa kutoka nje ya himaya yake na kweli kulikuwa na hoja katika dukuduku zako; lakini pamoja na hayo, mbwa kupata mtoko kuna umuhimu zaidi.”

Nikasisitiza kuwa, mtoko kwa mbwa ni muhimu kwani humsaidia mbwa kujifunza mazingira na kujua kuyatofautisha ili asimsumbue bwana wake kwa mambo yasiyokuwa ya msingi. Mbwa kazi yake ni kuangalia usalama wa himaya na kujulisha hatari kwa kubweka; mwenye ufahamu atajulisha kwa ufanisi mambo yanayotokea nje, lakini mbumbumbu anakuwa kero kwa bwana wake. Kwa mfano, mbwa ambaye hajawahi kutoka nje akisikia ngurumo za gari au honi, humjulisha hatari, wakati siyo hatari.

Kwa msingi huo, panapotokea hatari ya kweli, mwenye nyumba anaweza kupuuzia akidhani ni kelele za kila mara za mbwa, hivyo kufanyiwa uhalifu kirahisi. Tunaweza kusema, mbwa anapotoka mara kwa mara anajengewa ufahamu na kuweza kuchambua mambo yaliyo salama na ya hatari na kazi ya ulinzi kuwa ufasaha. Ni kweli anaweza kukutana na wanyama wengine wakati wa matembezi kama vile mbwa wenzake, paka, mbuzi, ng’ombe n.k; na pengine akataka kuwashambulia au kuonesha woga.

Hata hivyo, mbwa akikatazwa au kutiwa moyo pale anapoogopa, ataanza kujenga ujasiri na kujiamini na hatimaye kutambua siyo vitisho kwake. Kisha nikamjibu Mwalu kupitia ushairi kwamba, ili kuepusha mbwa kupigana na wenzake, ni vema akadhibitiwa kwenye kamba wanapokuwa matembezini, hususani anapohemka na kushindwa kutii amri anazopewa na bwana wake. Vile vile, mbwa anatakiwa kuchanjwa dhidi ya magonjwa ya maambukizi. Katika shairi la kujibu hoja za Mwalu, Nilisema: “Mtoko ni Dawa.”

Kimsingi, mbali na mbwa kupata uelewa wa mambo mbalimbali, mtoko humsaidia kupata furaha, na hamasa ya kufanya kazi na ujasiri kama ilivyoelezwa. Baada ya kujibu shairi la Mwalu, anakubali kuelimika na kukubali ‘Mbwa Apate Mtoko.’ Kusema ukweli hoja zake zilikuwa ni hoja za mtu anayetaka kujua kitu. Katika shairi lake la kukiri kuelimika na kushauri mbwa apate mtoko, alisema: “Ni mengi nimejifunza, Ufugaji mbwa wako.”

Baada ya kusoma shairi la Mwalu, hakuonekana kama mtu aliyeelimika tu, bali kama mdau muhimu katika ufugaji wa mbwa na kuelimisha wenzake katika jamii kuhusu faida za ufugaji. Kwa kuwa alikuwa anasoma mashairi ya uelimishaji, alielimika kwa kiasi kikubwa kuwa na utaalamu unaohitajika wa kufuga mbwa. Katika kumtia moyo, ninandika tena kumpongeza Mwalu kwa kufaulu somo la Ufugaji wa Mbwa na kumchagiza sasa aanze kufuga na kuelimisha jamii inayomzunguka nilipomwambia: “Mwalu umeshahitimu, Sasa ukafuge Mbwa.” Dk Egyne Emmanuel ni msomaji, mchangiaji, mtaalamu wa mifugo na mwandishi wa muswada wa kitabu uitwao Bustani ya Mbwa ulio mbioni kuchapishwa. Anapatikana kwa S.L.P 16561, DSM. Simu 0754 440233 na marandu72@ hotmail.com

KIPINDI cha Watanzania kutafuta uongozi wa nchi kimewadia tena ambapo ...

foto
Mwandishi: Dk Egyne Emmanuel

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi