loader
Picha

Ukosefu wa vyoo unavyozitesa familia nyingi Bukoba

CHOO ni moja ya sehemu muhimu ambayo kila kaya inapaswa kuwa nacho sambamba na kukitumia na hata kukihudumia ipasavyo ili kuepusha magonjwa mbalimbali.

Hata hivyo, bado wapo baadhi ya watu wasiothamini umuhimu na matumizi ya choo bora, hali inayowafanya baadhi ya watu kujenga nyumba, bila kujenga choo. Kimsingi, matumizi sahihi ya vyoo huchangia kuepusha magonjwa ya mlipuko yakiwamo ya kipindupindu na kuhara yenye madhara makubwa ndani ya muda mfupi.

Vyoo vina mchango mkubwa katika kujenga uchumi imara kwani ukosefu wa huduma hizo katika maeneo ya kazi na nyumbani una madhara makubwa katika kupunguza uzalishaji na pia, husababisha au kuongeza matumizi ya kipato cha familia au jamii kwa kuhudumia wagonjwa au kushughulikia msiba. Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza kampeni ya “Nipo Tayari” inayohamasisha ujenzi na matumizi sahihi ya vyoo bora ili kutunza mazingira na kulinda afya za watu.

Kampeni inalenga kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo kinachokidhi vigezo vya ubora ifikapo mwaka 2020 bila kujali kaya ipo mjini, au kijijini. Kampeni hii inawahusisha wenyeviti wa vijiji, maofisa watendaji wa mitaa, vijiji na kata, maofisa afya, huku mamlaka za wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wakitumika kuhamasisha umuhimu wa matumizi bora ya vyoo.

Moja ya mbinu zinazotumika kuhamasisha ujenzi na matumizi bora ya vyoo, ni viongozi wa maeneo husika wakiwamo wa kisiasa kupita nyumba hadi nyumba ili kukagua vyoo vinayotumiwa na wanakaya. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisa afya mkoani Kagera, Nelson Rumbeli, asilimia 3.2 ya wakazi wa mkoani Kagera waliokaguliwa katika kaya zao, hawana vyoo kabisa na kwamba, baadhi ya wakazi bado wana kasumba ya kuchimba mashimo madogo madogo katika mashamba yao kwa ajili ya ‘kujihifadhi’ kama choo.

Anasema katika utekelezaji wa Kampeni ya Nipo Tayari katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, kaya 247,813 zimekaguliwa. Kaya 7,893 kati ya hizo, zilibainika kuwa hazina choo kabisa hivyo zinatumia mfumo usio rasmi katika kujihifadhi. Ilibainika pia kuwa, kaya 3,677 huchangia vyoo na majirani hivyo wanatembea umbali wa dakika tano hadi 10 kufuata choo kwa jirani ili kujihifadhi.

“Kaya zilizobainika kutokuwa na vyoo, zimepewa muda kuhakikisha zinajenga na kutumia choo ipasavyo,” anasema na kuongeza kuwa, majina ya wahusika yatabandikwa katika ofisi na maeneo ya serikali za mitaa na vijiji kwenye mbao za matangazo yakiwa na kichwa cha habari: “WAFUATAO HAWANA CHOO NYUMBANI KWAO.”

Anasema hadi sasa maofisa wa afya, wenyeviti wa vijiji na maofisa watendaji ili kutunga sheria ndogondogo zitakazowawajibisha wasio na vyoo. Ofisa afya huyo anasema, Sheria Mama ya Mwaka 2009, inamtaka mtu asiye na choo kulipa faini ya shilingi milioni moja anapofikishwa mahakamani au kifungo cha miezi mitatu; au adhabu zote.

Anasema kuepusha lawama katika operesheni ya ukaguzi inayoendelea, mtu anapotembelewa ili kukaguliwa na upungufu kubaini, hupewa ilani ya marekebisho ya siku 7, siku 14 na siku 28; siku hizo zikipita, bila marekebisho kufanyika mhusika hulazimika kupelekwa mahakamani. Anaitaja Halmashauri ya Wilaya ya Muleba miongoni mwa halmashauri nane zilizopo mkoani Kagera, kuwa ndiyo inayoongoza kwa kutokuwa na vyoo ikiwa na asilimia 19 pekee ya vyoo bora huku Manispaa ya Bukoba ikiongoza kuwa na vyoo bora kwa asilimia 79.

Mkazi wa Kata ya Kitendaguro, Johannes Marco (36) anashindwa kubainisha sababu za kushindwa kuwa na choo na hata anakopata huduma hizo sambamba na familia yake. Anasema anajipanga kujenga choo bora taratibu kwani gharama za ujenzi huo zipo juu katika katika Manispaa ya Bukoba. Marco anaiomba serikali kuingilia suala la watumishi wa idara ya afya wanaofanya ukaguzi kwani wamekuwa wakitoza faini kati ya Sh 200,000 hadi 300,000 kwa mtu asiyekuwa na choo kiasi ambacho ni kikubwa mno.

“Siwezi kubainisha kuwa mimi na familia yangu tunajihifadhi wapi, tumekuwa tukichimba mashimo kwa ajili ya kujihifadhi kama unavyojua choo ni gharama kubwa kutokana na mafundi tulionao hivyo najipanga kujenga choo bora hivi karibuni kwa sababu nimetolewa faini,” anasema Marco. Naye Zamoto Ngaiza (39) mkazi wa Mtaa wa Kyakailabwa, Kata Nyanga katika Manispaa ya Bukoba, anaelezea madhara ya kukosa choo akisema, ameishi na familia yake kwa miaka miwili bila choo.

“Nimeishi vizuri na baba yangu hivyo hata nilipooa na kuaga nyumbani kuhamia hapa kwangu, sikuona umuhimu wa kujenga choo kwani bado niliona tunaishi vizuri tutaendelea kutumia choo kimoja maana kwangu siyo mbali na nyumbani, lakini shida ilikuwa ni usiku mpaka unakata tamaa…” anasema Ngaiza. Anaongeza: “Tumekuwa tukitembea karibu mwendo wa meta 150 kufika kwa wazazi ambapo kuna choo na ndicho tulichokuwa tunakitumia, lakini sasa toka kampeni ilipoanzishwa na kutufikia, leo tuna siku ya tano tunatumia choo cha familia yetu.”

Anasema walikuwa wanapata ugumu hasa nyakati za usiku, mmoja wetu au hata mtoto anapowaamsha akisema anataka kujisaidia au tumbo linamuuma kwani katika mazingira hayo, wakati mwingine walilazimika kutumia ndoo au beseni kumwekea mtoto ajisaidie haja kubwa na kwenda kusafisha vyombo hivyo usiku huohuo. Baada ya kuwa na choo nyumbani anasema: “Sasa tunajisikia furaha kwa kuwa sasa tunajihifadhi hapa karibu hata kama ikitokea shida kama tumbo kukuchafuka usiku, au dharura nyingine familia inapata sehemu ya kujisaidia haraka na karibu.”

Mkazi huyu anawashukuru viongozi wa mtaa wanaoendelea kuhamasisha na kutekeleza majukumu yao ya kuwa na vyoo bora huku akisisitiza kuwa, amebaini ukweli kuwa, choo ni nyumba. Diwani wa Kata ya Bakoba, Jimmy Mwakyoma anasema mara nyingi kupitia mikutano ya vijiji anaendelea kuhimiza wananchi umuhimu wa kujenga vyoo bora na kuvitumia katika maeneo ya kazi na makazi ya watu hususani, kila kaya.

Anasema lengo lake na kamati ya afya na wenyeviti wa mitaa, ni kuhakikisha kata yao inaongoza katika Manispaa ya Bukoba kwa kujenga na kutumia vyoo bora. Naye Mjumbe wa Mtaa wa Katatolwansi, Kata ya Kashai, katika Manispaa ya Bukoba, anasema mtaa wake kwa kushirikiana na idara ya afya, tayari wametunga sheria ndogondogo ili kuzichukulia hatua kaya zisizo na vyoo. Anasema licha ya faini ya Sh 200,000 hadi 300,000 iliyowekwa, bado wapo baadhi ya watu wanaoona ni bora kulipa faini na kuendelea kukaa katika kero na mazingira hatari kiafya, kuliko kujenga choo na kukaa katika mazingira salama.

Anasema hao watapelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Anasema kupitia mikutano ya mitaa, wameazimia kuwa atakayebainika kutokuwa na choo bora, watatafutwa mafundi watakaojenga choo haraka na kaya italazimika kulipia gharama zote na faini. Kwa mujibu wa Mjumbe huyo, kuwa na vyoo bora ni ajenda ya kudumu katika mikutano ya mitaa na kwamba, majina ya watu wasio na vyoo yatakuwa yanasomwa hadharani katika mikutano.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Bukoba, Dk Hamza Mugula anasema kutokana na kutokuwepo vyoo bora mwaka 2015 kuliwahi kuwepo magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu jambo lililoleta mshutuko kwa wananchi. Anasema maeneo mengi yaliyokumbwa ni pamoja na ya mitaa yenye watu wengi hasa ambao vyoo vyao vilikuwa vimepasuka.

Dk Mugula anayataja maeneo ya visiwani kuathirika zaidi kwani baadhi ya vyoo hutiririsha maji katika ziwa na hayo ndiyo wananchi wanayatumia katika kunywa, kuoga, kupikia na kufulia Mganga Mkuu huyo anatoa mwito kwa wananchi kuchukua hatua ili kuepusha hofu iliyotanda mwaka 2015 kutokana na ugonjwa wa kipindupindu uliojitokeza katika baadhi ya maeneo huku akisisitiza kuwa kujenga vyoo bora utakuwa mkombozi wa afya za wananchi wengi na bajeti ya dawa itaelekezwa katika masuala mengine. Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Bukoba ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Richald Ruyango kupitia Baraza la Madiwani la Bukoba anasema kuanzia sasa uongozi bora utapimwa kutokana na namna viongozi watakavyoshirikiana na wananchi kuhakikisha wanajenga vyoo bora.

Fukwe nzuri na za kuvutia zinazofaa kwa kuota jua (sunbathing) ...

foto
Mwandishi: Diana Deus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi