loader
Picha

Tubadilike, tutibiwe ndani ya EAC

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zina kila sababu ya kujivuna kutokana na hali ya kujiimarisha katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta nyeti ya afya ambayo idadi ya madaktari, wauguzi, hospitali na taasisi zake zinaendelea kuongezeka baada ya nchi zetu kupata uhuru kamili kutoka kwa wakoloni waliozitawala.

Hakuna ubishi kwamba tumefikia hatua hiyo kwa umakini, ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo wataalamu wa sekta hiyo inayogusa uhai na maisha ya wananchi kwa ujumla wao. Ni ukweli pia kwamba kutokana na uhaba wa vifaa vya uhakika, utaalamu wa kutosha na unyeti wa baadhi ya magonjwa, nchi zetu kama zilivyo baadhi ya nchini nyingine barani Afrika zimekuwa zikilazimika kuwapeleka wananchi wake wenye mahitaji ya huduma zisizopatikana katika nchi zetu, kwenda kutibiwa nje.

Nchi hizo ni pamoja na India kwa lengo la kupigania afya za wananchi bila kujali gharama ambazo zinaambatana na huduma hizo. Tumepata faraja baada ya taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Katibu Mtendaji wa Tume ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki (EAHRC), Profesa Gibson Kibiki kwamba sasa huduma ambazo tulikuwa tunazitafuta nje ya EAC tena kwa gharama kubwa, zinapatikana ndani ya nchi zetu. Alizitaja huduma hizo kuwa ni za matibabu ya magonjwa ya moyo, figo, saratani.

Alisema wagonjwa wenye matatizo ya figo wanaweza kutibiwa Kenya ambako huduma hiyo inatolewa kwa viwango vya juu na wenye magonjwa ya moyo wangeweza kutibiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Muhimbili, Dar es Salaam nchini Tanzania ambayo inatoa matibabu ya kibingwa. Matibabu mengine alieleza ni yale ya saratani yanapatikana Uganda ambako matibabu ni ya kiwango cha juu, wakati matibabu kwa mtandao, uhandisi tabibu na ukarabati wa kiafya yanapatikana kwa ubora pia nchini Rwanda.

Ndiyo maana sisi tunasema watu wa EAC tuna kila sababu ya kutumia hospitali, vituo na wataalamu wetu waliopo maeneo hayo ndani ya EAC kujipatia huduma tunazohitaji kutibiwa kwa magonjwa hayo badala ya kung’ang’ana kwenda kupata huduma hizo nje ya nchi zetu.

Tunapenda kutoa mwito kwa wanasiasa na serikali zetu ndani ya EAC kuendelea kuwaelimisha watendaji katika sekta hiyo na wananchi kwa ujumla wao kutumia taasisi zetu hizo badala ya kuendeleza ukiritimba wa kutibiwa nje ya nchi tena kwa gharama kubwa. Lengo kubwa kwa kila nchi makini kutumia rasilimali watu ya kwao ni pamoja na kukuza ajira, utaalamu na kujihakikishia ukomavu halisi katika sekta husika na kuwa huru kwa kujikomboa kutoka utegemezi wa nje ya nchi. Tubadilike ili kujikwamua kitiba na kiuchumi.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi