loader
Picha

Miamba iliyotikisa dunia yaandika historia mpya

WALIPOKUTANA kwa mara ya kwanza, watu wengi walipigwa butwaa kwa sababu, hakuna aliyejua kama wangeshikana mikono na kukaa meza moja. Hii ni kutokana na uhasama mkubwa uliokuwapo kati yao na hapa nawazungumzia, Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un.

Trump na Kim wamekuwa kwenye mvutano mkali kiasi kwamba, watu wengi walihofia kuwa wangeitumbukiza dunia kwenye vita nyingine ya tatu. Hata hivyo, hatua ya wakuu hao kukutana Hoteli ya Capella katika kisiwa cha utalii cha Sentosa, Singapore ilitoa mwanga mapya kwa usalama wa dunia. Tunaambiwa kuwa mkutano wa viongozi hao ulikuwa wa kihistoria kwani walikutana kwa saa chache, lakini walizungumza masuala yenye umuhimu mkubwa.

Itakumbukwa kuwa silaha za nyuklia ndizo chanzo cha Trump na Kim ‘kuvimbiana’ huku kila mmoja akionesha ubabe ama jeuri kwa mwenzake. Kilichozidi kuleta hofu zaidi kama si kushitua dunia ni hatua ya Kim kurusha makombora ya masafa marefu, hususan lililopita katika anga ya Japan. Kitendo hicho kilitafsiriwa kama “uchokozi” huku Marekani na mataifa mengine yakiweka ‘mguu sawa’ kutokana na ‘kusoma alama za nyakati.’

Mbali na suala hilo, kitendo cha Rais Kim kusema kitufe cha kufyatua makombora yake kipo ndani ya ofisi yake kilisababisha taharuki nyingine kubwa kwa Marekani. Ndiyo maana Rais Trump aliapa kuwa atapambana na uongozi wa Kim endapo utaendelea kutishia nchi yake, huku wakiendelea kutupiana maneno ya hapa na pale.

Pengine kwa kuhofia kuwa vita ipo mbioni kunukia, Rais Kim alibadili mwelekeo na kuanza kurejesha uhusiano mwema na jirani yake, Korea Kusini. Itakumbukwa hapa kuwa, Korea Kaskazini na Korea Kusini kwa muda mrefu zilikuwa sawa na mbingu na ardhi kutokana na sababu mbalimbali. Mojawapo ya sababu ni kitendo cha Korea Kaskazini kuitazama Korea Kusini kama rafiki wa kweli wa Marekani, jambo ambalo halikufurahisha nchi hiyo. Hata hivyo, mapema mwaka huu Korea ya Kaskazini ilipeleka timu na ujumbe maalumu kwa ajili ya kushiriki michuano ya Olimpiki Korea Kusini mjini Pyeongchang.

Mambo haya na mengine mengi, yalifungua njia kwa Marekani kukutana na Kim, ingawa awali Trump alisusa ili kujiridhisha katika baadhi ya mambo. Iwe itakavyokuwa, lakini itoshe kusema hapa kuwa, hatua iliyofikiwa na mataifa hayo mawili inastahili kuigwa, kwani imeleta matumaini kwa watu wengi duniani. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, uzoefu umeonesha vita ina gharama kubwa na athari zake kwa nchi na dunia ni kubwa, hivyo meza ya mazungumzo ni muhimu zaidi.

Ni kwa kutambua hilo, Rais wa Urusi, Vladmir Putin aliweka bayana kuwa atasimama kidete ili kufanikisha mazungumzo kati ya marais hao. Taarifa zinaonesha kuwa, mazungumzo yao yalikuwa na mafanikio makubwa kwani walikubaliana kupunguza uhasama, lakini pia kupunguza silaha za nyuklia. Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), mambo manne yalifikiwa na kukubaliwa wakati wa mazungumzo kati ya marais hao.

Mambo muhimu Mosi ni kwamba, Marekani na Korea Kaskazini zitaanzisha uhusiano mpya ili kudumisha amani kwa ajili ya ustawi wa nchi hizo pamoja na wananchi wake. Jambo la pili ni kwamba, nchi hizo mbili zitashirikiana kwa karibu zaidi kujenga na kudumisha amani ya kudumu katika Rasi ya Korea. Jambo la tatu ni kwamba, Korea ya Kaskazini itahakikisha inaangamiza silaha za nyuklia katika rasi hiyo.

Jambo la nne ni kwamba, Marekani na Korea Kaskazini zimejitolea kuhakikisha mateka wa vita na watu waliotoweka vitani wanapatikana. Hii maana yake ni kuwa, wababe hawa wamekubali kufukuza giza na kukaribisha nuru kwa ustawi wa nchi zao na dunia kwa ujumla. Ni faraja kwa Guterres Kitendo cha Trump na Kim kukutana na kufanya mazungumzo kimetoa faraja kubwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, Guterres alikuwa akiumiza kichwa namna ya kumaliza mvutano kati ya mataifa hayo kwa usalama wa dunia.

Kwa lugha nyingine ni kwamba, Katibu Mkuu huyo alikuwa akifanya kila linalowezekana ili kuhakikisha viongozi hao wanazika kabisa tofauti zao. Hili limefanikiwa kwa kiwango chake kutokana na mazungumzo yaliyofanyika, na hili linatoa tafsiri chanya kwa Guterres katika kusimamia majukumu yake. Kuthibitisha namna alivyokuwa na kiu ya kuona mazungumzo hayo yanafikiwa, alikaririwa akisema: “Umoja huo utakuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa wakuu hao ili wafikie makubaliano.”

Pamoja na kazi kubwa iliyofanyika, jambo muhimu kwa sasa ni marais Trump na Kim kuhakikisha yaliyofikiwa yanaheshimiwa na pande zote mbili. Si tu kwa usalama wa mataifa hayo, lakini pia kwa dunia kwa sababu tatizo likitokea Marekani au Korea Kaskazini litaathiri pia maeneo mengine duniani. Tumejifunza nini? Tulichojifunza kwa wakuu hawa kukutana ni kwamba, vita si mwarobaini wa kuleta amani, bali mazungumzo. Hii inatokana pia na uzoefu wa Marekani katika masuala ya vita kwamba, inapoteza fedha nyingi na nguvu kazi katika mapigano na kuathiri uchumi wake.

Lingine la kujifunza ni kuwa, penye vita shughuli za uzalishaji husimama na wananchi huteseka hasa watoto na wanawake, hivyo meza ya mazungumzo ina tija zaidi. Kwa msingi huo, kilichofikiwa kati ya pande hizo mbili kiwe chumvi ya kuleta amani pale penye vita na matumaini ya kweli kwa waliokata tamaa. Trump na Kim wameonesha kuwa, penye busara na hekima hakuna linaloshindikana na hilo limejidhihirisha wakati wa mazungumzo yao. Watu wengi duniani wamejifunza na kuthibitisha kwamba, busara na hekima ni nyenzo muhimu katika kuzika tofauti na kuleta nuru mahali penye giza.

Fukwe nzuri na za kuvutia zinazofaa kwa kuota jua (sunbathing) ...

foto
Mwandishi: Julian Msacky

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi