loader
Picha

Uzalishaji washusha bei ya mbaazi

WIZARA ya Kilimo imesema hali iliyosababisha kuporomoka kwa bei ya mbaazi ni kutokana na ongezeko la uzalishaji wa zao hilo katika nchi za India, China, Brazil, Myanmar, Canada, Msumbiji, Sudan na Tanzania.

Naibu Waziri Dk Mary Mwanjelwa alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM).

Katika swali lake, Chikota alisema wakulima wa mbaazi mikoa ya Mtwara na Lindi wameshuhudia kuporomoka kwa bei katika msimu wa mwaka huu pamoja na kwamba walihamasika kulima kwa wingi.

Aliuliza, je, ni nini kilisababisha kuporomoka kwa bei ya mbaazi na je, serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha hali hiyo haijitokezi msimu ujao?

Akijibu swali hilo, Dk Mwanjelwa alisema ni kweli bei ya zao hilo iliporomoka kutoka wastani wa bei ya Sh 2,750 kwa kilo mwaka 2014/15 hadi Sh 700 kwa msimu wa mwaka 2015/16 na kufikia wastani wa Sh 300 kwa msimu wa mwaka 2016/17 katika mikoa mbalimbali nchini.

Alisema pamoja na ongezeko hilo la uzalishaji mwezi Agosti 2017 nchi ya India ambayo ndio wanunuzi wakuu wa mbaazi zao ilizuia uingizaji wa mbaazi kutoka nje ya nchi hiyo kwa kuwa walikuwa na uzalishaji mkubwa wa kukidhi mahitaji yao.

Alisema hali hiyo itasababisha ukosefu wa soko la uhakika wa mbaazi zilizozalishwa nchini msimu wa 2016/17. "Ili kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika serikali imeandaa mikakati mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao hususani mbaazi," alisema.

Alibainisha mikakati ya muda mfupi ni pamoja na Wizara kupitia Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko itaongeza idadi ya mazao yatakayonunuliwa ambayo ni pamoja na mazao jamii ya mikunde, mbegu za mafuta na nafaka katika msimu wa mwaka 2018/19.

Alisema kwasasa bodi hiyo imepata soko la tani 100,000 za soya, tani 20,000 za ufuta na tani 3,500 za mbaazi ambazo zitauzwa kwa wadau ndani na nje ya nchi. Pia bodi itanunua tani 6,000 za alizeti kwa ajili ya kukamua mafuta katika kiwanda chake kilichopo Kizota jijini Dodoma.

"Mkakati wa muda mfupi ni kuuza mbaazi katika soko la bidhaa na kuhamasisha utumiaji wa mbaazi hapa nchini katika maeneo mbalimbali hususan katika shule na majeshi."

Dk Mwanjelwa alisema serikali kupitia maofisa lishe waliopo katika Halmashauri watatoa mafunzo ya namna bora ya kuandaa vyakula vitokanavyo na mbaazi. Pamoja na hayo, alisema mikakati ya muda mrefu ni pamoja na Kampuni kutoka India kujenga kiwanda kiitwacho Mahashree Agro processing Ltd kitakachosindika aina zote za mazao ya jamii ya kunde, korosho na ufuta katika kata ya Mkambarani wilayani Morogoro.

Alisema kitakuwa na uwezo wa kusindika tani 200 za aina mbalimbali ya mikunde kwa siku na kuuza katika soko la ndani na nje na kitaanza uzalishaji mwaka 2019.

HIFADHI ya Taifa ya Ruaha imejipenyenza katika vyuo vikuu 20 ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi