loader
Picha

Teknolojia inavyosaidia kufundisha ufundi stadi

MOJA ya nguzo muhimu katika kufikia malengo ya uchumi wa kati, ni kutayarisha nguvukazi yenye maarifa na stadi sahihi za kazi. Takwimu zinathibitisha kuwa, ufundi stadi ndio unaochangia zaidi nguvukazi katika viwanda. Uwiano wa kimataifa unaonesha kuwa, kwa utendaji wenye ufanisi katika kiwanda chochote, mhandisi mmoja anahitaji kuwa na mafundi mchundo watano na mafundi stadi 25.

Katika kukidhi matakwa hayo, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) imeendelea kuhakikisha kuwa inaweka mikakati mbalimbali ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kufikia idadi kubwa zaidi ya vijana popote walipo. Kaimu Mkurugenzi wa Veta, Dk Bwire Ndazi, anaitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyuo vipya, kubuni mbinu za utoaji mafunzo ili kufikia makundi mengi zaidi, pamoja na kuboresha miundombinu ya vyuo vilivyopo ili viweze kuhudumia idadi kubwa zaidi.

“Pamoja na mikakati hiyo, Veta inakitazama Chuo cha Walimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kwa jicho la kipekee kutokana na umuhimu wake katika kufanikisha mikakati mingi iliyojiwekea,” anasema. Anaongeza: “Hii ni kwa kuwa, ni kupitia chuo hicho pekee ambako walimu wa ufundi stadi nchini huandaliwa.”

Anasema wahitimu kutoka MVTTC hutarajiwa kuwa na stadi za ualimu na za ufundi stadi zinazowawezesha kuandaa rasilimali watu yenye stadi za kazi kwa ufasaha wanapohitimu mafunzo. Naye Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Habibu Bukko, anasema ili kukidhi matakwa hayo sambamba na mahitaji ya sasa, MVTTC inaendelea kuimarishwa ili iende sambamba na ukuaji wa teknolojia.

Anasema, MVTTC sasa inaimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa karibu kila eneo lake la mafunzo ya ualimu wa ufundi stadi. Kufanya hivyo inaelezwa kuwa, hakuwawezeshi tu walimu tarajiwa wa ufundi stadi kwenda kufundisha teknolojia za kisasa katika vyuo vya ufundi stadi nchini, bali pia vifaa hivyo hurahisisha ufundishaji na kuongeza udahili kwa MVTTC.

“Kwa sasa MVTTC ina vifaa vingi vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ambavyo hutupa nafasi ya kutoa mafunzo kwa ufanisi zaidi na kuhudumia idadi kubwa zaidi ya wanafunzi wanaohitaji kusomea ualimu wa ufundi stadi,” anasema. Anasema uwezo wa chuo hicho kwa sasa ni kudahili wanafunzi 440 kwa mwaka kwa ngazi ya stashahada na cheti.

Anasema mafunzo hutolewa chuoni Morogoro na katika vituo vya nje ya chuo vipatavyo 13 vilivyopo Mikumi, Dar es Salaam, Karagwe, Mwanza, Kagera, Mbeya, Mafinga, Iringa, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Ruvuma na Dodoma. Mafunzo hayo hutolewa kwa miaka miwili kwa ngazi zote, ngazi ya cheti na stashahada kwa mafunzo ya ndani na miaka mitatu kwa mafunzo yatolewayo nje ya chuo. Anasema zaidi kuwa jitihada za kufikia mikoa yote zipo mbioni kuzalisha walimu wengi wa mafunzo ya ufundi stadi, ikiwa ni maandalizi ya kukidhi mahitaji ya walimu kwa vyuo vya ufundi stadi ambavyo ni zaidi ya 500 nchi nzima.

Anaongeza kuwa, pamoja na kusoma masomo ya ualimu, pia hujifunza masomo ya ufundi stadi kuwapandisha madaraja ya fani zao kutoka ngazi tatu hadi ya tano (NVA 3 – NTA 5) kwa mafunzo ya ngazi ya astashahada na hadi ngazi ya sita (NTA 6) kwa mafunzo ya ngazi ya Stashahada ya Ualimu wa Ufundi Stadi. Aidha, wanachuo hupata fursa ya kwenda kujifunza kwa vitendo viwandani kwa muda wa miezi mitatu kila mwaka ili kuongeza uwezo wao wa kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia katika soko la kazi.

Anataja baadhi ya maboresho katika vifaa chuoni hapo kuwa ni pamoja na matumizi ya vifaa viwakilishi (simulators) vya kufundishia fani za umeme wa nyumbani na viwandani. Vingine ni vifaa vya kutolea mafunzo kwa njia ya video vinavyowezesha mafunzo ya masafa kati ya MVTTC na kampasi zake kwa kuanzia na Chuo cha Veta cha Mkoa wa Dodoma. Kadhalika, kuna vifaa kwa ajili ya maabara ya lugha ili kukuza uwezo wa wanafunzi kutumia lugha ya Kingereza.

“Maktaba ya chuo pia imeimarishwa kwa kuunganishwa kwenye mtandao wa maktaba, e-library na vyuo vikuu hapa nchini,” anaongeza. Mkufunzi wa Fani ya Umeme Chuoni hapo, Annelisa Andengulile, anasema vifaa hivyo vinawawezesha kumwelewesha mwanafunzi kuelewa kwa haraka na kwa urahisi zaidi kuliko inavyokuwa kwa matumizi ya vifaa vingine. Anasema ndani ya mwezi mmoja tu tangu vifaa hivyo kufungwa kwenye karakana, ameweza kuelewa matumizi yake na anaendelea kujifunza zaidi ili amudu matumizi yake. Kaimu Mkuu wa Chuo hicho anatoa mwito kwa vijana wengine zaidi kujitokeza kwa wingi kusomea ualimu wa ufundi stadi kwa kuwa vyuo vingi vya ufundi stadi vinatarajiwa kujengwa nchini na kwamba, vitahitaji walimu wa kutosha ili kuvihudumia.

“Mahitaji ya walimu wa ufundi stadi yanazidi kuongeza kila siku. Kwa sasa MVTTC inaandaa walimu kwa ajili ya vyuo vipya vya mikoa ya Geita, Simiyu, Katavi na Njombe.” ”Ikumbukwe kuwa, Serikali ina nia ya kujenga chuo cha ufundi stadi kila wilaya (kuna Wilaya 187). Vyuo hivi vitahitaji walimu zaidi kwani, hata waliopo sasa hawatoshelezi vyuo vilivyopo,” anasema. Anasema chuo hicho pia kipo kwenye hatua za mwisho za kuanzisha mafunzo kwa njia ya masafa ili kufundisha taaluma ya ualimu wa ufundi stadi kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano na kwamba, mpango huu unatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu.

Fukwe nzuri na za kuvutia zinazofaa kwa kuota jua (sunbathing) ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi