loader
Picha

Yajue mambo yatakayoipamba Nanenane Simiyu

“NITUMIE nafasi hii kualika wadau wote ndani na nje ya nchi nikiamini hawatatoka watupu… Tunafanya kitu cha kipekee….” Ndivyo anavyosema Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akielezea maandalizi ya Sikukuu ya Wakulima maarufu kama Nanenane.

Nanenane ambayo ni sikukuu inayosherehekewa kila ifikapo Agosti 8, mwaka huu itasherehekewa kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu. Eneo hilo la Nyakabindi ambalo awali lilikuwa msitu mkubwa ulio umbali wa takribani kilometa 20 kutoka mjini Bariadi, sasa litakuwa sehemu muhimu itakayotumiwa na maelfu ya watu wanaotarajiwa kushiriki maonesho hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika katika kanda mpya ya Ziwa Mashariki.

“Uwanja una uwezo wa kuchukua waoneshaji 450 ambao kila mmoja anakadiriwa kuwa na watu wasiopungua watano; ukiongeza na watu wanaokuja kuangalia maonesho, idadi ya watu inaweza kufika 5000,” anasema Mratibu Sherehe za Nanenane, Kanda ya Ziwa Mashariki, Dk Gamitwe Mahaza. Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mtaka, anasema yatakuwa maonesho ya kipekee; yenye utofauti na mengine. Anasema: “Kwetu sisi tumeyatafsiri kama maonesho rasmi ya shughuli na teknolojia mbalimbali za kilimo.”

Mtaka anasema malengo yao ni kwamba teknolojia mbalimbali za kilimo, uvuvi na ufugaji zitaoneshwa. Kutakuwa na semina na makongamano mbalimbali kwa ajili ya kujengea uwezo wakulima, wafugaji na wavuvi. Haya yatakuwa ni maonesho ambayo kanda hii mpya imeendelea kualika watu wa makundi yote ndani na nje ya nchi washiriki huku ikisisitiza kuwa, kila mdau atafurahi na kunufaika nayo. “…tunafanya kitu cha kipekee… tunaweka ladha za kimataifa ili kuwaona wenzetu katika maonesho ya aina hii yanayohusu shughuli za kilimo yanaonesha shughuli gani,” anasema mkuu wa mkoa huyo.

Anaongeza kuwa, inazinduliwa tovuti ya Nanenane Simiyu kuwezesha watu mbalimbali kufanya usajili wa ushiriki kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha hata walio nje ya nchi kujisajili. Mratibu sherehe za Nanenane, Kanda ya Ziwa Mashariki, Dk Gamitwe Mahaza anasema Ubalozi wa Indonesia umewahakikishia kushiriki maonesho hayo. “Juzi tulikuwa na Balozi wa Indonesia nchini; amethibitisha kushiriki na ameomba eneo maalumu kwa ajili ya ushiriki,” anasema Mahaza. Aidha, baadhi ya mashirika ya kimataifa yamethibitisha kushiriki maonesho hayo. Miongoni mwa mashirika hayo ni pamoja na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP).

“Sisi Nanenane yetu ni ya kipekee kwa sababu tunataka kujenga jengo kubwa la kisasa ambalo mshiriki utabeba bidhaa zako, utaingia na bidhaa zako wala huhitaji kubeba turubai,” anasema Mahaza. Jengo hilo la maonesho linajengwa na halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu na lina eneo la meta 62.5 kwa 24. Linakadiriwa kuchukua watu 150 na vitu vyao walivyodhamiria kuonesha. Thamani ya jengo hilo ni Sh milioni 662. 4 na mkandarasi ameanza kazi ili ifikapo Agosti mosi, liwe limekamilika.

Akielezea zaidi maandalizi kwa upande wa miundombinu katika viwanja vya Nyakabindi, Mahaza anasema lipo jukwaa kwa ajili ya viongozi lililopata ufadhili kutoka Benki Kuu (BoT) kufanikisha ujenzi. Aidha, wanaendelea na matengenezo ya barabara zinazotenga maeneo na ameshapatikana mdau atakayechonga barabara hizo zenye takribani kilometa sita. Kuhusu maji, Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeridhia kuwachimbia kisima kirefu na kusambaza huduma hiyo. Hata hivyo, hiki kitakuwa kisima cha kudumu.

Aidha, wamezungumza na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wameridhia kuunganisha nishati hiyo kwenye eneo la maonesho. “Umeme upo, zipo nguzo za umeme mkubwa wa gridi ya taifa. Kinachotakiwa ni kuushusha kutoka laini ya gridi ili uingie kwenye matumizi,” anasema. Maeneo mengine kama vile vyoo, ukumbi wa kupokea wageni pia yanaandaliwa na wadau mbalimbali wameombwa kuchangia ujenzi wake kabla ya maadhimisho hayo hayajaanza Agosti mosi.

Miongoni mwa makundi yaliyothibitisha ushiriki ni pamoja na halmashauri zote 21 za kanda pamoja na baadhi ya wizara. Miongoni mwa shughuli zinazoendelea sasa ni pamoja na ugawaji wa maeneo ya vipando. Haya ni maeneo kwa ajili ya upandaji wa mimea mbalimbali kwa ajili ya maonesho. “Kanda ya Ziwa Mashariki kuna halmashauri 21 katika mikoa mitatu. Zote zinaendelea na maandalizi ya vipando,” anasema. Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji, Wizara ya Uvuvi na Wizara ya Viwanda tayari zipo mkoani Simiyu zikiendelea na maandalizi. Taasisi mbalimbali za usambazaji pembejeo kwa wakulima pia zimeshaanza shughuli zake tayari kwa maonesho.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Magereza na BoT pia ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki sawia maonesho hayo. Kwa mujibu wa Mratibu, maonesho yatafunguliwa na Makamu wa Rais na Agosti 3. Anasema hii ni siku iliyotengwa kama siku ya Kilimo Kwanza. Waziri Mkuu ndiye anategemewa kuwa mgeni rasmi katika maonesho haya. Nanenane ni sikukuu zinazosherehekewa nchini kote Agosti 8 kila mwaka. Taarifa ya serikali kupitia tovuti yake inaeleza kuwa, sherehe hizo hutayarishwa na kuratibiwa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na Shirika la Chama cha Kilimo Tanzania (Taso) na kuhusisha taasisi, wizara na mtu mmoja mmoja wanaoshughulika na kilimo.

Miaka iliyopita sherehe hizi zilikuwa zikifanywa Julai 7 kila mwaka na kuzingatia mafanikio makubwa na changamoto zinazokabili sekta ya kilimo inayowashirikisha wadau wote kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa. Nanenane husherehekewa katika ngazi ya kanda na majina ya viwanja vinavyotumika kwa ajili ya maonesho katika mabano ni; Kanda ya Nyanda za Juu za Kusini (John Mwakangale, mjini Mbeya); Kaskazini (Themi, Arusha) , Mashariki (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Morogoro) na Kanda ya Ziwa (Nyamhongolo, Mwanza) na Kanda ya Kusini, zilifanyika Ngongo. Baada ya kugawanywa kwa mikoa iliyokuwa ikiunda Kanda ya Ziwa, zikazaliwa kanda mbili; Kanda ya Ziwa Magharibi yenye mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita; na Kanda ya Ziwa Magharibi inayoundwa na Simiyu, Mara na Shinyanga.

Fukwe nzuri na za kuvutia zinazofaa kwa kuota jua (sunbathing) ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi