loader
Picha

Hii ndiyo Geita inayopokea kijiti Jukwaa la Biashara

MKOA wa Geita ulioanzishwa mwaka 2012 unapokea kijiti cha kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Fursa za Biashara nchini kutoka mkoa wa Arusha. Jukwaa hili linalotarajiwa kurindima katika mji wa ‘dhahabu’ wa Geita Agosti 15-16 ni la tatu kwa mwaka huu na la saba tangu majukwaa haya yalipoanzishwa mwaka jana.

Kama kawaida Jukwaa linaandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha HabariLeo, Daily News, SpotiLeo na mitandao kadhaa ya kijamii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, chini ya uongozi wa Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi. Mkoa wa Geita ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania. Umepakana na Kagera kwa upande wa magharibi, Shinyanga upande wa kusini, Mwanza upande wa mashariki na Ziwa la Victoria kwa upande wa kaskazini.

Makao makuu ya mkoa yapo Geita mjini

Kabla ya kuanzishwa kuwa mkoa, sehemu kubwa ya Geita, ilikuwa mkoani Mwanza. Lakini wilaya yake moja (Chato) ilikuwa mkoa wa Kagara na nyingine (Bukombe) ilikuwa mkoa wa Shinyanga. Mkoa wa Geita ulikadiriwa kuwa na wakazi 1,882,141 mwaka 2015. Makabila makubwa katika wa Geita ni Wasukuma, Wasumbwa, Walongo na Wazinza. Geita inaundwa na wilaya tano za Bukombe, Chato, Geita, Mbongwe na Nyang’hwale.

Mkoa wa Geita una majimbo sita ya uchaguzi ya Geita Mjini ambayo mbunge wake ni Costantine Kanyansu (CCM) na Geita Vijijini linaloongozwa naye Joseph Kasheku ‘Msukuma’ (CCM). Majimbo mengine ni Busanda iliyo chini ya mbunge Lolensia Bukwimba (CCM), Mbogwe ambayo mbunge wake ni Augustino Masele (CCM), Bukombe ya Dotto Biteko (CCM) na Chato ambayo mbunge wake ni Dk Medard Kalemani (CCM). Mkoa wa Geita unapitiwa na mito kadhaa ambayo ni pamoja na Bwiga, Ichuankima, Ikonka, Jakabaga, Kafunso, Mabubi na Muhama.

Mito mingine ni Mwunekese, Nyabulela, Nyakukutu, Nyamasenga, Nyamazama, Roata, Shiperenge na Mto Usigaga. Wilaya Nyang’hwale Nyang’hwale ni moja kati ya wilaya tano za Mkoa wa Geita. Makao makuu ya wilaya hii ni kilichokuwa kijiji cha Kharumwa. Wilaya hii kwa upaande wa Kaskazini inapakana na Wilaya ya Sengerema, Kaskazini inapakana na Wilaya ya Misungwi na Shinyanga Vijijini wakati kusini inapakana na Kahama Vijijini huku upande wa Magharibi ikipakana na wilaya ya Geita.

Wilaya hii iliyoanzishwa mwaka 2012 wakati mkoa wa Geita unaundwa iligawanywa kutoka wilaya ya Geita. Wakati wa sensa ya mwaka 2012 Nyang’hwale ilikuwa watu 148,320. Kwa upande wa Usafiri, wilaya ya Nyang’hwale haina barabara kuu ya lami bali ina barabara mbili za kawaida zinazouinga na miji ya Geita, Kahama na Sengerema.

Kiutawala Nyang’hwale ina kata 12 ambazo ni Bukwimba, Busolwa, Izunya, Kafita, Kakura, Kharumwa, Mwingiro Nyabulanda, Nyang’hwale, Nyijundu, Nyugwa na Shabaka Wilaya ya Mbogwe Mbogwe ni wilaya nyingine kati ya tano za mkoa wa Geita. Wilaya hii kwa upande wa kaskazini inapakana na wilaya ya Chato na Geita, mashariki inapakana na Kahama vijijini pamoja na Kahama mjini, kusini inapakana na Kahama vijijini wakati magharibi inapakana na wialaya ya Bukombe.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Mbogwe ambayo ilianzishwa pia mwaka huo wa 2012 ilikuwa na watu 193,922. Kwa upande wa usafiri wilaya ya Mbogwe imeunganishwa kwa barabara (kutoka Morogoro hadi kwenye mpaka wa Tanzania na Rwanda), linalopita katika wilaya hiyo kutoka mashariki hadi magharibi. Wilaya hii ina kata 16 za Bukandwe, Ikobe, Ikunguigazi, Ilolangulu, Iponya, Isebya, Lugunga, Lulembela, Masumbwe, Mbogwe, Mgemo, Nanda, Ng’homolwa, Nyakafulu, Nyasato na Ushirika. Wilaya ya Geita Wilaya ya Geita ndio pia makao makuu ya mkoa wa Geita.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 wilaya hii ilikuwa na jumla ya watu 807,619. Wilaya ya Geita inapakana na wilaya za mkoa wa Mwanza kwa upande wa mashariki, Wilaya ya Nyang’hwale kwa upande wa Kusini pamoja na mkoa wa Shinyanga na wilaya ya Mbogwe na kwa upande wa magharibi wilaya ya Geita napakana na wilaya ya Chato. Moja ya mradi mkubwa katika wilaya ya Geita ni mgodi wa madini wa Geita Gold Mine (GGM) ulioko umbali wa kilometa nne magharibi mwa mji wa Geita.

Mgodi huo unamilikiwa na kampuni ya Anglo- Gold Ashanti. Kabla ya kuanzishwa kwa mkoa wa Geita Machi mwaka 2012, wilaya hii ilikuwa moja ya wilaya katika mkoa wa Mwanza. Barabara kubwa inayounganisha wilaya hii ni ile inayotokea Mwanza hadi Bukoba. Geita ina kata 35 za Bugalama, Bugulula, Bujula, Bukoli, Bukondo, Bulela, Bung’wangoko, Busanda, Butobela, Chigunga na Ihanamilo Kata zingine ni Isulwabutundwe, Kagu, Kakubilo, Kalangalala, Kamena, Kamhanga, Kasamwa, Kaseme, Katoma, Katoro, Lubanga, Lwamgasa, Lwezera, Mtakuja na Nkome Kata zingine zinazounda wilaya ya Geita ni Nyachiluluma, Nyakagomba, Nyakamwaga, Nyamalimbe, Nyamigota, Nyanguku, Nyarugusu, Nzera na Senga Wilaya ya Chato Wilaya ya Chato nayo ni moja ya wilaya tano za mkoa wa Geita ulioko kaskazini magharibi mwa nchi yetu.

Makao makuu ya wilaya hii yako katika mji wa Chato. Rais John Magufuli, historia inaonesha kwamba alizaliwa hapo Chato mwaka 1959. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Chato ilikuwa na watu 365,127. Wilaya ya Chato ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa sehemu ya Mkoa wa Kagera baada ya kugawanywa kwa wilaya ya Biharamulo. Ulipoanzishwa mkoa wa Geita mwaka 2012, ndipo wilaya hiyo ikaondolewa Kagera na kupelekwa Geita. Kata za wilaya ya Chato ni 23 ambazo ni Bukome, Buseresere, Butengorumasa, Buziku, Bwanga, Bwera, Bwina, Bwongera, Chato, Minkoto na Ichwankima, Kata zingine za wilaya ya Chato ni Ilemela, Ilyamchele, Iparamasa, Kachwamba, Kasenga, Katende, Kigongo, Makurugusi, Muganza, Muungano, Nyamirembe na Nyarutembo.

Wilaya ya Bukombe Bukombe ni wilaya nyingine kati ya tano zinazounda mkoa wa Geita. Mji wa Ushirombo ndiko yaliko makao makuu ya wilaya hii. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Bukombe ilikuwa na watu 224,542. Kabla ya Machi 2012, Bukombe ilikuwa moja ya wilaya nane za mkoa wa Shinyanga. Wilaya hii ina kata 15 za Bugelenga, Bukombe, Bulega, Busonzo, Butinzya, Igulwa, Iyogelo, Katente, Lyambamgongo, Namonge, Ng’anzo, Runzewe Mashariki, Runzewe Magharibi, Ushirombo na Uyovu. Uhondo Geita Wadau kutoka wilaya hizo tano Agosti hii wanaletewa Jukwaa la Biashara ambalo linatazamiwa kuwakutanisha na taasisi kadhaa za fedha, Mamlaka ya Mapato (TRA), Baraza la Uwekezaji la Taifa (NEEC) na wadau kutoka makundi na sekta mbalimbali za kijamii na kibiashara.

Ni jukwaa linalotazamiwa kubadilisha mitazamo ya wakazi wengi wa Geita kuhusu biashara na uwekezaji na pia kupitia jukwaa hilo Watanzania wengi wanatazamiwa kujua fursa za kibiashara zilizoko katika mkoa wa Geita. Kuanzia wiki iliyopita, vyombo vya habari vya TSN muda wote vitakuwa vinaumulika kwa kina mkoa wa Geita. Jukwaa la biashara linatazamiwa pia kuwazindua wafanyabiashara wazawa wa Geita kufikiria kufanya makubwa zaidi kwa faida yao, mkoa na taifa kwa ujumla.

Wafanyabiashara wadogo wa Geita watatumia fursa zilizopo kwa kuwekeza pakubwa na hivyo kuwa pia wafanyabiashara wakubwa. Inatazamiwa pia kwamba kupitia jukwaa hili, baadhi ya wafanyabiashara wataacha kuhangaika na vitu ambavyo havina tija kubwa baada ya kuziona fursa na kuwa wawekezaji wakubwa. Wafanyabiashara wenye nia ya kunufaika na biashara zao lakini wana matatizo madogo madogo kama vile kutojua ni wapi watapata mitaji yenye unafuu, masuala ya usajili, taratibu za kodi na kadhalika, kupitia jukwaa hili watapata majibu.

Wadau walio tayari Baadhi ya taasisi ambazo mpaka sasa zimeonesha nia ya kuongea na wakazi wa Geita kwa ajili ya maendeleo yao ni taasisi za fedha za Benki za NMB, Azania Bank, TIB Corporate Bank, TTCL Pesa pamoja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC). Taasisi zingine ni Shirika la Umeme (Tanesco) ambalo muhimu sana kwa uchumi wa viwanda, Bohari Kuu la Dawa (MSD) ambalo linasambaza dawa nchi nzima na kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika na Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) itakayohamasisha wananchi wa Geita umuhimu wa kujiunga na mifuko ya pensheni. Kama kawaida, Mamlaka ya Mapato (TRA) ambayo imekuwa ikitoa elimu kubwa ya mambo ya kodi na ambayo imekuwa ikijibu maswali mengi yenye uhakika katika majukwaa yaliyotangulia inatazamiwa kuwemo pia “ndani ya nyumba”. Wadau zaidi wanaotaka kueleza wanachokifanya sambamba na kufanya biashara na wananchi wa Geita bado wanakaribishwa.

Fukwe nzuri na za kuvutia zinazofaa kwa kuota jua (sunbathing) ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi