loader
Picha

Ripoti ya ‘Uwezo’ ilivyozua mjadala maendeleo ya elimu

KUSHINDWA kuwalisha watoto chakula cha mchana shuleni ni moja ya vipengele nyeti vilivyoonekana kuwakera wadau wa elimu wilayani Mbarali waliohudhuria uzinduzi wa Ripoti ya Sita ya Utafiti wa Uwezo uliofanyika mwaka 2015 katika wilaya 159 nchini. Utafiti huo kwa wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, ulifanywa na Shirika la Tanzania Health and Development Initiative (THDI) kwa ufadhili wa Twaweza kupitia mradi wa Uwezo.

Utafiti ulilenga kujua uwezo wa watoto walio na umri wa kati ya miaka saba hadi 16 wa kusoma Kiingereza, Kiswahili na kufanya Hesabu ambapo mitaala iliyotumika kuwapima wanafunzi ni ile ya darasa la pili. Akitoa matokeo ya utafiti huo mbele ya wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo uliofanyika mjini Rujewa, mratibu wa mradi wa Uwezo wa THDI, Leocardia Uswege, alisema ni asilimia tatu tu ya shule za msingi zilizopo wilayani hapa zinatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi.

Uswege alisema kutokana na kutopata chakula cha mchana mashuleni, wanafunzi wamekuwa wakishindwa kuwa makini wanapofundishwa hivyo kusababisha kukosekana kwa uelewano baina yao na walimu. Alisema hilo ni miongoni mwa mambo yanayochangia matokeo mabovu wilayani humo, hususani kwa kipindi cha miaka hiyo ulipofanyika utafiti. Kipengele kingine kilichosababisha mjadala mkali kwa wajumbe waliohudhuria uzinduzi ni uwezo mdogo wa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba katika kujua Kingereza, Kiswahili na Kuhesabu.

Kwa mujibu wa Uswege, utafiti ulionesha nusu ya wanafunzi wanaohitimu darasa la saba wilayani Mbarali hawajui kusoma na kuandika somo la Kiingereza huku pia asilimia 11 kati ya wahitimu hao wakiwa hawajui kusoma Kiswahili. Alisema pia utafiti umebaini kuwepo kwa changamoto ya mahudhurio ya wanafunzi na walimu ambapo kwa Mbarali, mahudhurio ya wanafunzi ni asilimia 76 ikiwa imepitwa na kiwango cha kitaifa cha asilimia 71 na kwa walimu mahudhurio ni asilimia 81 ikiwa imepita pia kiwango cha kitaifa cha asilimia 75.

Mengine yaliyobainika katika utafiti huo ni pamoja na uwiano wa wanafunzi kwa walimu darasani kutoendana ambapo bado kuna maeneo wanafunzi wanakuwa wengi darasani kiasi cha kumfanya mwalimu ashindwe kufuatilia mwenendo wa kujifunza wa mwanafunzi mmoja mmoja. Halikadhalika, utafiti ulionesha wazazi wengi kutofuatilia kabisa maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao wanaporudi nyumbani. Kwa kuonesha kutoridhishwa na hali ilivyo baada ya matokeo ya utafiti huu, maazimio yaliyofikiwa na wadau pamoja na wananchi ni pamoja na kuhakikisha suala la chakula shuleni linakuwa agenda ya kudumu.

Wadau walitaka suala hili lizungumzwe kila mahali na kila wakati ili wazazi wasio na uelewa watambue kasoro hii inavyokwamisha maendeleo katika sekta ya elimu. Akizindua ripoti hiyo kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, katibu tawala wa wilaya, Oliva Sule, alipongeza utafiti huo kwa kuwa umewapa taswira ya hali ilivyo katika sekta ya elimu na hatua gani jamii na serikali kwa ujumla vinapaswa kuchukua. Alisema kinachotakiwa kufanyika sasa ni mjadala wa pamoja wa namna ya kutatua changamoto zilizoainishwa ikiwemo kuhakikisha wanafunzi wanapata mlo shuleni. “Hapa hakuna haja ya kunyoosheana vidole.

Ni wakati wa kila mmoja kujiuliza amefanya nini, anafanya nini na atafanya nini. Tutamlaumu mwalimu hapa lakini tukumbuke mwalimu atatumia uwezo wake wote kufundisha lakini akili ya mtoto haitapokea kwa kuwa anasumbulia njaa. Hajala. “Au mwalimu amemfundisha kwa uwezo wote mtoto akirudi nyumbani mzazi wala haulizi nini kafundishwa au amepewa kazi gani na mwalimu ili aifanye akiwa nyumbani,” alisema Sule.

Akaongeza: “Kwenye hili suala la chakula inasikitisha kuona wale mnaohamasisha mnaanza kunyooshewa vidole na wazazi wakisema mna lengo la kujikusanyia vyakula. Utakuta wazazi wanawaita walimu mchwa, ukiwauliza nini unaambiwa wanataka tuwakusanyie vyakula ili wale wao na si wanafunzi. Hii inawakatisha tamaa hata walimu wenyewe.”

Alisema ni suala la kila mzazi kujiuliza kwamba kama siku mwanawe anaposhinda nyumbani atahakikisha anampa chakula inakuwaje sasa siku anaposhinda shule haoni sababu ya kumlisha mwanae. “Madiwani pia watusaidie kuongea na wazazi, wazungumze kwenye vikao vya maendeleo ya kata, waagize pia lizungumzwe kwenye vikao na mikutano ya vijiji. Ni aibu kwa wilaya ya Mbarali yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula kwa wingi tukaishia asilimia tatu tu ya shule kulisha wanafunzi chakula cha mchana,” alisisitiza Sule.

Aliwataka pia wakuu wa idara na watendaji wengine kushirikishana na ofisi ya mkuu wa wilaya pale kunapokuwa na changamoto. “Usibaki unaumia na changamoto peke yako, sema ili tutafute ufumbuzi kwa pamoja. Lakini na wazazi sasa tutoke nje ya boksi la kubaki unasema mtoto huyu hana akili kama mama yake au kama baba yake kumbe ni sisi wenyewe wazai hatujatekeleza wajibu wetu wa malezi bora,” alisema Katibu tawala huyo wa Mbarali. Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali, Mganga Ngomuo, alisema matokeo ya Utafiti huo yanasaidia kutambua ni kwa nini kumekuwepo na wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika katika kidato cha kwanza na cha pili kwenye shule za sekondari.

“Kama mtoto yuko darasa la saba anapewa maswali ya darasa la pili anashindwa, vipi ukimpa ya darasa lake? Na hili ndilo darasa linalotoa wanafunzi wanaokwenda sekondari. Ndiyo sababu siku ya siku tunapokea malalamiko ya uwepo wa wanafunzi hawa katika sekondari zetu. “Lazima tukae tupitie upya. Tufanye tathmini na tusibakie kusema tuko vizuri kumbe huko chini kuna tatizo kubwa. Na hii itamgusa kila mmoja kwa nafasi yake, awe mzazi, kiongozi wa dini, kiongozi wa kimila, mwalimu, watendaji na madiwani sote kwa pamoja kila mmoja ajitafakari,” alisisitiza Ngomuo.

Mganga mkuu wa wilaya ya Mbarali, Albert Sichone alisema kwa kuwa ubongo wa binadamu unatakiwa kujengwa katika kipindi cha tangu kutungwa kwa mimba hadi umri wa miaka mitano ni muhimu lishe bora ikazingatiwa. Akiongea kitaalamu zaidi, Dk Sichone alisema wanafunzi wasiopata chakula shuleni huku bado wakiwa na umri ambao akili yao inahitaji lishe ili kukomaa kiakili wanaweza kuathirika kwa udumavu wa mwili na akili na hivyo kukosa uwezo darasani. “Utafiti huu unatuonesha pia tatizo lililopo kwenye familia zetu.

Kama tuna tatizo la lishe kwenye familia zetu na kama uwezo wa kutunza familia ni mdogo tutawapa kazi kubwa walimu kufundisha watoto tuliowazaa. Hapa sasa tunaona kuna ulazima wa sekta zote zikaenda sambamba, iwe kilimo, afya, elimu na nyinginezo kwa kuwa zinategemeana ili kupata matokeo chanya,” alisema mtaalamu hiyo wa masuala ya afya. Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Brown Mwakibete alisema: “Utafiti lazima ujibiwe na utafiti mwingine na si kuongea tu jukwaani hivyo kwa matokeo ya utafiti huu inatupeleka sisi kwenye utafiti mwingine ili kujua tulipo hivi sasa. Kazi mliyoifanya ni kubwa na imetupa mwanga.

“Utafiti huu ulifanyika mwaka 2015, hapo katikati yapo mambo yamekwishafanyika hasa kutokana na uchapaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli. Lakini yaliyokwishafanyika hayatupi mwanya wa kubeza matokeo ya utafiti huu. Lakini pia niwaombe wataalamu waliododosa wasiishie hapa baada ya kutoa ripoti hii bali wazidi pia kutoa elimu kwa kaya,” alisema.

Akizungumzia suala la kutoa chakula shuleni, Makamu Mwenyekiti huyo alisema anachoona ni uvivu tu wa wananchi na pia kukosa uelewa kwani Mbarali siyo ya kushindwa kutoa chakula kwa watoto wake shuleni. Ofisa Elimu Msingi, Benjamin Kazi, na wa Sekondari, Ibrahim Ngolloh na Mdhibiti wa ubora wa Elimu wilayani hapa, Mathias Asanwisye walisema kwa nyakati tofauti kwamba ni vyema ripoti hiyo ya utafiti ikatumika kuboresha kiwango cha taaluma shuleni na isipuuzwe.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali wilayani hapa (Usangonet), Terdey Mhagama alisema kupitia utafiti huo kuna vitu vya kuzungumzwa na si kufumbia macho kwani kuna matatizo makubwa shuleni ambayo pasipo jitihada madhubuti kuchukuliwa yanaweza kuendelea kuwa kikwazo kwa walimu na wanafunzi. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la THDI, Grace Mkumbwa, licha ya ripoti ya utafiti huu imetolewa baada ya miaka miwili kupita, jitihada za ushirikiano wa pamoja zinahitajika ili kukabili changamoto zilizobainishwa kwenye taarifa. Alikiri kwamba huenda yapo mambo ambayo tayari yametafutiwa ufumbuzi na Serikali.

Fukwe nzuri na za kuvutia zinazofaa kwa kuota jua (sunbathing) ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi