loader
Picha

Biashara huria ni muhimu duniani licha ya majaribu ya Trump

Wakati nchi za Afrika zikiendelea na juhudi za kuanzisha eneo la biashara huria na kuhimiza biashara ichochee ongezeko la uchumi katika miezi ya hivi karibuni tumekuwa tukisikia mivutano ya kibiashara ikiendelea katika maeneo mengine duniani.

Kwa upande mmoja kuna nchi Marekani, ambayo inalalamika kuwa mazingira ya biashara duniani si rafiki kwa taifa hilo, jambo ambalo limesababisha Serikali ya Rais Donald Trump kuchukua hatua za upande mmoja kujaribu kurekebisha hali hiyo.

Kwa upande mwingine kuna nchi mbalimbali kama vile China, Canada, Brazil na hata Umoja wa Ulaya zinazoona kuwa Marekani inakiuka kanuni za biashara ya kimataifa zilizowekwa na Shirika la Biashara Duniani (WTO) kwa kutoza ushuru usio wa haki kwa nchi wanachama wa shirika hilo. Nchi hizo zimeeleza wazi kuwa endapo Marekani ikifanya hivyo, basi nazo zitajibu kwa kutoza ushuru bidhaa za Marekani zenye thamani kama inayotoza Marekani.

Hali hii ya mvutano wa kibiashara kama ya sasa haijawahi kutokea duniani na imefanya kuwe na wasiwasi kuwa mafanikio yaliyopatikana katika kufufua uchumi wa dunia, uliokuwa umedorora kutokana na msukosuko wa fedha uliotokea mwaka 2008, yanaweza kupotea na kuirudisha tena dunia kwenye msukosuko mwingine. Ni wazi kuwa dunia kwa sasa imefungamana kwa kiasi kikubwa, uamuzi unaofanywa na nchi moja, unaweza kuwa na athari kwa nchi nyingine.

Ndiyo maana katika siku za hivi karibuni, viongozi wa nchi mbalimbali duniani na hata wa mashirika ya kimataifa, wamekuwa wakitoa tahadhari kuhusu kauli na maamuzi yanayofanywa na wanasiasa kwa uchumi wa dunia. Ikumbukwe kuwa hali ya utulivu duniani na maendeleo yanayoonekana katika sehemu mbalimbali, yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wa karibu kiuchumi na kibiashara, unaofanya kila nchi ione umuhimu wa nchi nyingine kwa maendeleo na usalama wake.

Kinachofanywa na serikali ya sasa ya Marekani ni wazi kuwa kinahatarisha amani na maendeleo ya dunia. Mivutano ya kibiashara dunia si jambo geni, mivutano hiyo imekuwepo kati ya makampuni na hata kati ya nchi, japokuwa haikuwahi kutokea kwa kiwango kama cha sasa. Hata hivyo mara zote mivutano hii imekuwa inatatuliwa kwa njia za mawasiliano ya pande mbili au kwa kutumia utaratibu wa WTO.

Kuna njia nyingine nyingi za kutatua mivutano hiyo Kinachoonekana kwa sasa ni kuwa Rais Donald Trump wa Marekani anasimama kwenye majukwaa nchini Marekani na kutumia Twitter, kutangaza kwa utaratibu upande mmoja (unilateralism) kuzitoza ushuru nchini nyingine bila hata kuwasiliana kwa udhati na nchi hizo, au hata bila kufuata kanuni za WTO.

Hali hii imeleta mazingira ya wasiwasi kuhusu utulivu wa biashara na haisaidii kwenye kuendeleza uchumi wa dunia. Inawezekana kuwa Trump mwenyewe hajui anataka nini na endapo anajua, basi hajui namna ya kukipata. Lakini ni wazi kuwa hawezi kupata anachotaka kwa kuziathiri nchi nyingine bila kuiathiri nchi yake. Kuna mifano kadhaa ya athari za vitendo vyake vya kufanya maamuzi ya upande mmoja kwa uchumi wa Marekani ikiwemo kuyumba kwa masoko ya hisa kila anapotoa kauli za kutoza ushuru dhidi ya nchi nyingine na kampuni maarufu ya kutengeneza pikipiki ya Harley Davidson.

Kampuni hii imeamua kuhamishia baadhi ya shughuli zake nje ya Marekani ili kukwepa ushuru wa kulipiza kisasi kutoka Umoja wa Ulaya. Jambo ambalo pia linatia wasiwasi ni hali ya kukosa udhati na kuaminika kwa serikali ya Rais Trump. Wafanyabiashara na makampuni mahali popote duniani ikiwa ni pamoja na wa Marekani, wanafanya kazi katika mazingira ya kuaminika na kutabirika.

Bila kuwepo mazingira ya kuaminika ni vigumu kwa wafanyabiashara na makampuni kufanya uwekezaji. Marekani kwanza imeonyesha hali ya kutoaminika kwenye kuheshimu makubaliano na WTO ambayo ilikuwa kinara wa kuyatunga, Rais wake kuwa kigeugeu kwa yale anayosema na anayoahidi kwa viongozi wenzake na hivi karibuni hata wawakilishi wa Marekani kwenye mazungumzo ya biashara wameonyesha hali kama hiyo.

Fadhili Mponji anaishi Beijing, China na ni mtangazaji wa China Radio International (CRI).

 

UGONJWA wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya ...

foto
Mwandishi: Fadhili Mponji

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi