loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Neymar abebeshwa lawama

PAMOJA na kuwasaidia mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia, Brazil kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia kwa kuifunga Mexico, nyota wa timu hiyo Neymar amelaumiwa kwa vitendo vyake visivyo vya kiuanamichezo. Brazil sasa ina kibarua kingine wakati itakapokutana na Ubelgiji katika mchezo wa robo fainali.

Ubelgiji iliifunga Japan kwa mabao 3-2 na kutinga katika hatua hiyo ya pili ya mtoano. Neymar alifunga bao moja na kutengeneza jingine na kuwezesha Brazil kuikandamiza Mexico kwa ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa katika hali ya joto kali. LAWAMA KIBAO Lakini Neymar amekuwa akilaumiwa sana kwa vitendo vyake vya kujirusha na kujifanya kaumia pale anapoguswa kidogo tu na mchezaji wa timu pinzani. Kitendo cha hivi karibuni kabisa alikifanya katika kipindi cha pili, wakati kiungo wa Mexico Miguel Layun alipoonekana kumgusa katika kifundo cha mguu.

Neymar alijiangusha na kujibiringisha kama vile ameshutuliwa na umeme na kuwashangaza wengi akiwemo kocha wa Mexico, Juan Carlos Osorio. Osorio alisema mchezaji huyo amekuwa na tabia hiyo ya `kujifanya’ kitendo ambacho kinamfanya kuushushia hadhi mchezo wa soka. “Nafikiri ni aibu kwa mchezo wa soka,“ alisema kocha huyo wa Mexico, Osorio, kwamba Neymar amekuwa na tabia ya ajabu katika soka. “Tumepoteza muda mwingi kwa sababu ya mchezaji mmoja tu…tulipoteza mfumo wetu wa uchezaji katika kipindi cha pili, kwa sababu ya mwamuzi.

“Hii ni mbaya sana kwa dunia na dunia ya soka.” NI MASIKITIKO Mitandao ya kijamii ilionesha jinsi mashabiki wa soka walivyokuwa na hasira dhidi ya Neymar kwa udanganyifu, ambapo mshambuliaji wa zamani wa England, Alan Shearer alielezea nyota huyo wa klabu ya Paris Saint-Germain kama ni wa kusikitikiwa kwa vitendo vyake. “Hakuna wasiwasi kuhusu tabia yake. Ni mchezaji anayependa kujifanya,“ alisema Shearer, ambaye yuko hapa akifanya kazi katika Shirika la Utangazaji la BBC.

“Lakini ni jambo la aibu wakati anapojibingirisha chini pale tu anapoguswa utafikiri ameumizwa kweli.” Hata hivyo, Neymar alipuuza ukosoaji huo dhidi yake baada ya mchezo huo aliocheza katika kiwango cha juu. “Sijali sana kukosolewa, au kupongezwa, kwa sababu hiyo inaweza kushawishi ta- bia yako,“alisema. “Katika mechi mbili zilizopita sikuzungumza na waandishi wa habari kwa sababu sikutaka suala hilo. Nachotaka ni kucheza, kuisaidia wachezaji wenzangu, na kuisaidia timu yangu pia.”

Beki wa Brazil, Thiago Silva alimpongeza Neymar, ambaye ndio kwanza amerejea kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia baada ya kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi mitatu kutokana na kuwa majeruhi. “Ni jambo zuri jinsi anavyocheza, hasa baada ya kukaa nje ya uwanja kwa miezi mitatu kutokana na maumivu, “ alisema Silva ambaye ni mchezaji mwenzake wa PSG. Walipocheza dhidi ya Mexico, Neymar alicheza vizuri lakini Brazil ilibidi kusubiri hadi dakika za mwisho ili kutinga hatua ya robo fainali.

Mbrazili huyo mwenye umri wa miaka 26 alifunga bao la kwanza la Brazil walipocheza dhidi ya Mexico katika dakika ya 51 na kuifanya timu hiyo kuwa mbele kwa bao 1-0. Nyota huyo wa Brazil akiwapita mabeki kibao wa timu pinzani na kukimbia katika eneo la Mexico, kabla hajatoa pasi kwa Willian na kuendelea kukimbia katika boksi.

Willian anayeichezea klabu ya Chelsea ya England ndiye aliyefunga bao la ushindi baada ya kupiga mpira uliompita Guillermo Ochoa. Mexico ilijikuta ikipoteza kabisa mfumo wake na huenda Brazil ingeweza kufunga zaidi baada ya safu ya ulinzi ya Mexico kujichanganya mara kwa mara, na kiungo wa Real Madrid, Casemiro aliyemjaribu Ochoa lakini alishindwa kufunga.

Neymar ana mabao mawili hadi sasa akiongozwa na mchezaji nyota wa England, Harry Kane, ambaye anaongoza kwa upachikaji mabao katika mashindano ya mwaka huu hadi sasa baada ya kufunga mabao matano. Lakini Silva ana matumaini kuwa Neymar ataendeleza makali akishirikiana na wachezaji wenzake wa Paris Saint-Germain kama akina Edinson Cavani na Kylian Mbappe wakati wakipeleka mbele zaidi Brazil. “Ni kweli, nilisema hivi kabla ya mechi, “aliongeza Silva. “Ni matumaini yangu atanisikiliza mimi katika robo fainali.”

MANCHESTER United leo itaikaribisha Liverpool katika ...

foto
Mwandishi: MOSCOW, Urusi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi