loader
Picha

Bima ya Kilimo kuwezesha uchumi wa viwanda

SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) linakuja na Bima ya Kilimo, itakayosaidia kuunga mkono jitihada za serikali za kujenga uchumi wa viwanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Sam Kamanga amesema kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa na ndicho kinachotoa malighafi nyingi za viwandani nchini, hivyo aina hiyo ya bima itasaidia kujenga uchumi wa viwanda.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maonesho ya 42 ya Sabasaba yanayoendelea Dar es Salaam katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa, amesema NIC inaunga mkono jitihada za serikali za ujenga uchumi wa viwanda na kwamba aina hiyo ya bima itakuwa pia mkombozi wa wakulima pale majanga yanapowafika.

Amewataka Watanzania hususani wakulima, kuichangamkia aina hiyo ya bima kwani ina manufaa sana kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

Kamanga aliwataka Watanzania kutembelea banda lao ili waweze kupata elimu kuhusu aina ya bima wanazotoa na pia kujiunga na bima mbalimbali.

Alisema shirika lake limeimarisha huduma yake ya bima ya magari kwa nchi za Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) ili kuondoa udanganyifu. Alisema huduma hiyo kwa sasa imewekwa katika mfumo wa kidijiti hali ambayo inazuia bima bandia.

“Kwa sasa tuko kwenye kidijiti, hali ambayo inatuwezesha kuziba mianya yote ya udanganyifu,” amesema.

Amefafanua kuwa, udanganyifu ulikuwa unaikosesha serikali mapato na kwamba shirika lake limeziba mianya yote ya upotevu wa mapato.

Kamanga amesema, kwa sasa shirika lake linafanya kazi kisasa na liko kwenye ushindani na makampuni mengine ya bima.

Amewatoa hofu wateja wake kuhusu ulipwaji wa fidia kwa muda muafaka na kwamba, NIC ya sasa inamjali mteja na hakuna ucheleweshaji wa malipo iwapo itathibitika madai ni ya kweli.

“Tunalipa fidia kwa wakati ikithibitika madai ni ya kweli na hatuna njoo kesho….tunatoa huduma kisasa,” amesema.

HIFADHI ya Taifa ya Ruaha imejipenyenza katika vyuo vikuu 20 ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi