loader
Picha

Yanga zogo tupu

HALI ndani ya Yanga imezidi kwenda mrama baada ya Mwenyekiti wa muda wa kamati maalumu ya usajili, Abbas Tarimba kuachia ngazi kwa kushindwa kuelewana na viongozi wa klabu hiyo.

Juni 10, mwaka huu, kwenye mkutano mkuu wa wanachama wa Yanga, wanachama na Baraza la Udhamini liliunda kamati maalumu ya kusimamia usajili na masuala mbalimbali ya Yanga chini ya uenyekiti wa Tarimba, akisaidiana na mkuu wa mkoa wa zamani wa Dar es Salaam na Kilimanjaro, Said Meck Saidiki.

Akizungumza juzi sababu ya kuachia ngazi, Tarimba alisema baada ya uteuzi wao kuliibuka mengi kwenye mitandao ya kijamii yakionesha kuwabeza na kutoa vipengele vya kikatiba vikifafanua ubatili wa kamati hiyo. “Mtafaruku ukaanza kutokea kwenye makundi ya mtandaoni, yakaja maneno kwamba Baraza la Wadhamini na wanachama hawana mamlaka ya kuunda kamati maalumu, wenye mamlaka ni kamati ya Utendaji,” alisema. Alifafanua kuwa pia, makundi hayo yalitoa hadi vipengele na kuviweka mtandaoni huku kukiwa na habari nyingine za kuvuruga.

Tarimba alisema juzi kuna chombo cha habari kilitoa taarifa ya Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga kuwa ametangaza kuivunja kamati hiyo alipozungumza na wenyeviti wa matawi. “Suala sio hilo kuna gazeti leo limetoka (analitaja) wameandika kuwa Sanga amevunja hiyo kamati, amewaambia viongozi wa matawi na mimi nilikuwa nikitext (kutumiana ujumbe mfupi wa simu) na Sanga ananiambia bwana tafuta muda tuonane… mimi nionane naye wa nini wakati wao wakiwa na shida hawatoki ofisini kwangu… sasa leo mimi natafuta nini… “Wao wameshavunja hiyo kamati, kamati haipo, wafanye kazi zao waache sasa midomodomo mingi kwa sababu muda wenyewe umebaki mdogo mimi sitokuwepo na sipo kwa sababu kamati yenyewe kwanza keshaivunja na hata kama asingeivunja kwa utaratibu huu, aaah itakuwa ngumu kufanya nao kazi,” alisema. Alisema ameona ajiondoe kwa vile hajazoea maneno na kwamba yeye ni mtu mwenye kazi yake ya maana hivyo anahitaji kuendelea kulinda heshima yake. Tarimba, ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga mwanzoni mwa miaka ya 2000, kwa sasa ni Mkurugenzi Utawala na utekelezaji wa Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa. Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa hakupatikana kulizungumzia hilo baada ya simu yake ya mkononi muda mwingi kuwa imezimwa jana, huku Makamu Mwenyekiti Sanga akigoma kuzungumzia kwa madai alikuwa kwenye mkutano. Kwa upande wake, Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Sadick alisema bado hana taarifa za kujiuzulu kwa Tarimba kwa kuwa hawajawasiliana. “Nipo Mwanza na sijawasiliana naye kwa sababu tulikutana kama mara mbili na kukubaliana baadhi ya mambo tuyatekeleze,”alisema. Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, amewatoa hofu wanachama na mashabiki wa timu hiyo akidai kuwa watafanya usajili wa kutosha na kuwashangaza wengi. Akizungumza na gazeti hili jana, Nyika alisema pamoja na mambo mengi kujitokeza kipindi hiki ikiwemo kujiuzulu kwa Tarimba, Yanga bado itabaki kuwa imara kwa kusajili kila mchezaji ambaye ilimhitaji kwa ajili ya msimu ujao, hivyo haoni haja ya mashabiki wao kuwa na hofu. “Ni kweli Yanga inapitia katika kipindi kigumu lakini niwatoe hofu mashabiki wetu kwamba wasitishike na maneno ya mitaani na kujiuzulu kwa baadhi ya watu, Yanga ni taasisi kubwa inaendeshwa na watu wengi, kitu cha msingi ninachoweza kuwaambia ni kwamba timu yao ipo imara na tuliobaki tunaendelea kupambana kuhakikisha tunamsajili kila mchezaji ambaye kocha alimpendekeza,” alisema Nyika. Kiongozi huyo alisema mashabiki wanapaswa kuwaamini, kwani wapo kwenye kamati hiyo kwa miaka miwili sasa na wamekuwa wakifanya kazi nzuri kiasi cha Yanga kutawala soka la Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara mara tatu mfululizo. Alisema kujiuzulu kwa viongozi hao kunaweza kuwa pigo kwao kwa sababu nguvu imepungua lakini wao waliobaki watahakikisha wanaziba pengo hilo kwa kusajili wachezaji watakaorudisha heshima ya Yanga.

MUIGIZAJI wa Bongo Movie, Wema Sepetu amesema kuna uwezekano wa ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi