loader
Picha

TRA yataja vigezo msamaha wa madeni

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeainisha sifa za walipakodi watakaonufaika na msamaha wa madeni ya kodi za nyuma yakijumuisha riba na adhabu.

Pia TRA itatoa msamaha wa riba na adhabu ambayo utahusu kodi zote zinazotozwa kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na TRA isipokuwa ushuru wa forodha na mapato mengine yasiyo ya kodi kama kodi za kajengo na ada za matangazo.

Hatua hiyo inakuja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na sehemu ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015.

Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango amepewa mamlaka ya kutoa utaratibu maalumu wa kuwezesha Kamishna Mkuu kutoa msamaha wa riba na adhabu wa hadi asimilia 100 riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 tofauti na asilimia 50 ya hapo awali.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema jijini Dar es Salaam kuwa, serikali ilisikia kilio cha wafanyabiashara waliolalamikia kuwepo kwa malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma yakijumuisha riba na adhabu, na hivyo Bunge lilifanya marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na sasa imeshaanza kufanyiwa kazi.

Amesema, lengo kuu la msamaha huu ni kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni ya riba na adhabu kwa kuwapa fursa ya kulipa malimbikizo ya madeni ya msingi ya kodi “Principal Tax” kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha 2018/19 ili kuwapa motisha ya kulipa kodi kwa hiyari na kwa wakati.

Kamishna huyo alisema kuwa walipakodi watakaonufaika na utaratibu huo ni wale waliowasilisha ritani za kodi lakini bado wanadaiwa kodi yote au sehemu ya kodi zitokanazo na ritani hizo lakini pia wale ambao hawajawasilisha ritani za kodi na wana madeni ya kodi.

Aliongeza: “ Wengine watakaonufaika mbali na wale waliowasilisha na hawajawasilisha ritani za kodi, ni ambao walikuwa wanafanya biashara bila kusajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), namba ya usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VRN) au usajili mwingine wa kodi kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

“Pia waliowasilisha pingamizi za kodi kwa Kamishna Mkuu na ambao pingamizi zao bado zinashughulikiwa katika ofisi za Mamlaka ya Mapato na sio kwenye mahakama za kikodi. Pia ambao wamewasilisha pingamizi katika mahakama za kikodi na mashauri yao bado hayajatolewa maamuzi,” alisema na kuongeza;

“Wengine watakaopata msamaha ni wale ambao bado wana madeni ya nyuma ya kodi ambayo hayatokani na kesi za jinai za kodi, utakatishaji fedha, usafirishaji wa binadamu au shughuli nyingine haramu,” alisema Kamishna huyo huku akiwahimiza walipakodi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo maalumu la utoaji wa msamaha wa riba na adhabu.

Aidha Kichere alisema kuwa msamaha wa riba na adhabu utahusu kodi zote zinazotozwa kwa mujibu wa Sheria zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Alisema: “Tutatoa msamaha kwenye kodi zote isipokuwa: Ushuru wa Forodha unaosimamiwa chini ya Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na Mapato mengine yasiyo ya kodi ambayo TRA imepewa jukumu la kisheria la kuyakusanya. Mapato hayo ni kama vile: Kodi za Majengo na Ada za Matangazo.”

Katika kutoa msisitizo Kamishna alisema kuwa mlipakodi atakayestahili kupata msamaha wa riba na adhabu endapo yeye binafsi au mwakilishi wake aliyeidhinishwa kisheria atawasilisha maombi ya msamaha kwa kujaza Fomu maalumu Na.ITX207.01.E inayopatikana katika tovuti ya mamlaka hiyo kwa kufuata maelekezo yaliyowekwa.

Hata hivyo, amesema msamaha utatolewa kwa maombi yatakayokidhi masharti na kukubaliwa na Mamlaka ya Mapato ambapo Kamishna Mkuu wa TRA na Mlipakodi husika watasaini mkataba wa makubaliano utakaoanisha deni lote la kodi; riba na adhabu inayosamehewa, pamoja na kodi isiyo na riba wala adhabu itakayopaswa kulipwa kabla ya tarehe 30 Juni, 2019. Machi 20, mwaka huu, Rais Dk John Magufuli katika Mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara (TNBC) uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam alitoa rai ya kutoa msamaha kwa walipakodi wa namna hiyo.

ILI Tanzania ijenge Uchumi wa Viwanda, hadi kufikia mwaka 2025 ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi