loader
Picha

Obama ni chachu wageni kutalii EAC

RAIS mstaafu wa Marekani, Barack Obama ameondoka baada ya ziara binafsi ya siku nane nchini, ambapo alizuru mbuga za wanyama za Serengeti na baadae kwenda Afrika Kusini kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa mwasisi wa Taifa hilo, hayati Nelson Mandela.

Tunaungana na Watanzania wengine kueleza furaha yetu kuhusu ujio huo wa Obama na familia yake kutembelea mbuga zetu za wanyama na kusaidia kutangaza utalii wetu.

Kwamba ameondoka akiwa amefarijika na mapokezi aliyopata na pia vivutio vya utalii alivyoviona inatupa faraja zaidi na kuhamasisha viongozi wengine na watu maarufu duniani, wasanii, wanamichezo na wanasiasa wengine, kutembelea vivutio vyetu vya utalii.

Rais Obama ameidhihirishia dunia uzuri wa vivutio hivyo kiasi cha kuahidi kuvitangaza nje ili ambao hawajawahi kwenda, watafute muda. Tunaungana naye kuwataka wote ambao hawajapata fursa hiyo, kutumia likizo zao fupi au ndefu, ziara rasmi na binafsi, kutembelea mbuga hizo na vivutio vingine vilivyoko huko.

Wafanye hivyo wakijua Tanzania kama moja ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na jumuiya nyingine za Kanda kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), inayo maeneo mengi ya watu kutalii. Maeneo hayo yanampa fursa mgeni kutoka nchi yoyote katika kanda hizo, kuendelea na utalii wake hapa akiunganisha na utalii ambao ameufanya katika nchi hizo au kuanzia nchini hapa na kuendelea na ziara kwa nchi nyingine.

Hatua ya Rais Obama kuanzia ziara yake Tanzania na kuimalizia Afrika Kusini imeonesha hilo linawezekana kutokana na miundombinu mizuri ya usafiri wa ndege iliyopo katika nchi hizi zote.

Tunawakaribisha kwa mara nyingine, Rais huyo wa 44 wa Marekani na familia yake, viongozi wengine wa nchi hiyo ambao wamekuwa na mapenzi makubwa na nchi za Afrika Mashariki na watu wake na nchi nyingine duniani, kufanya ziara kwa ukanda huu kwani una vivutio vya kitalii vya kutosha.

Tunaamini, kupitia kwao, familia zao, umaarufu wao, ushawishi wao, watasaidia kutangaza zaidi na zaidi, utajiri wa maliasili za wanyama na pia misitu na utamaduni wetu kwa wasioufahamu. Ziara ya Obama iwe chachu ya kufanya wengine nao wawaze, watamani, wapange kuja kutalii kujifunza, kufurahi na kubaini siri ya kutoka mbali kote kujichimbia Serengeti kwa siku nane.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi