loader
Picha

Mjusi wa Tanzania nchini Ujerumani balozi wa utalii

TANZANIA imebahatika kuwa na viumbe adimu duniani ambao wanavutia watalii kila kona ya dunia. Moja ya vivutio hivyo ni mjusi ambaye anafahamika kwa jina la Tendaguru anayepamba makumbusho ya Ujerumani.

Tendaguru ni mjusi mkubwa kuliko hata tembo ambaye anaaminika kuwa ndiye mnyama mwenye umbo kubwa wa nchi kavu na mnyama mwenye uzito mkubwa, aliyehifadhiwa katika Makumbusho ya viumbehai ya Berlin, Ujerumani. Mjusi huyo alivumbuliwa katika eneo la Tendaguru mkoani Lindi miaka 100 iliyopita. Mjusi huyo ambaye ana uzito wa tani 50 ni kivutio adimu katika makumbusho ya Berlin, Ujerumani. Mjusi huyo kwa jina la kitaalamu anaitwa dinosaur ambapo masalia ya mjusi huyo katika eneo la Tendaguru, yalikusanywa na kupelekwa Ujerumani ambako wataalamu waliyaunda na kisha kuyaweka kwenye Makumbusho ya Berlin yaliyojengwa tangu mwaka 1889.

Tendaguru ndilo jina ambalo linatumiwa na watafiti na wataalamu katika machapisho yaliyopo kwenye makumbusho hayo ambapo wanalitumia jina hilo kutambulisha mijusi wote wakubwa sio wa Tanzania pekee bali pia wanaotoka katika nchi nyingine. Mjusi huyo anakadiriwa kuwa na umri wa miaka milioni 150, ana urefu wa meta 13.7 kwenda juu, anakadiriwa kuwa na moyo wenye uzito wa kilo 400 na chakula cha mjusi huyo kilikuwa ni mimea.

Mwanasayansi wa mambo ya kale, Dk Daniella Schliart anasema mjusi huyo aligundulika kati ya mwaka 1907 na 1909 ambapo watafiti katika eneo la Tendaguru walikuwa wanatafiti madini ndipo walikutana na masalio hayo kisha kukusanya masalia na kuyasafirisha hadi nchini Ujerumani. Wanasayansi hao na watafiti walibaini kuwepo aina 13 tofauti za mijusi ambao baadhi yao waliishi kwa kula mimea na wengine nyama.

Dk Schliart anabainisha namna walivyopata umri wa mjusi huyo ni kwa kuangalia makundi ya madini yalivyopangiliwa na kwa kutumia programu za kompyuta. Masalio ya mjusi huyo yanatunzwa kwa kutumia kemikali maalumu za kumlinda asije akasambaratika. Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa kimataifa na Sayansi, Dk Christopher Hauser anasisitiza kuwa Tanzania inahitaji wataalamu wa mambo kale ambao wamepata mafunzo maalumu ya kuhudumia masalia ya mijusi wa kale.

“Tanzania itayarishe wataalamu wa kutunza masalia ya mijusi kwa sababu wanakaa miaka mingi hivyo wanaweza kuharibika. Utafiti unaonesha kuwa bado Tanzania kuna masalio ya mijusi katika eneo la Tendaguru na maeneo mengine,’’ anasisitiza Dk Hauser. Licha ya kuhifadhiwa masalia ya mjusi huyo kutoka Tanzania katika Makumbusho ya Ujerumani kuna masalia ya viumbe wengine ambao ni nyoka, ndege, simba, chui na mijusi wakubwa kutoka nchi mbalimbali. Makumbusho ya nchini Ujerumani yapo chini ya Wizara ya Elimu na Utafiti ambayo huingiza wastani wa watu 500,000 kwa mwaka ambapo kiingilio chake ni euro nane kwa kila mtu anayetembelea makumbusho hayo.

Nchi ya Ujerumani na Tanzania zimekubaliana kuendeleza tafiti za masalia ya mijusi katika eneo la Tendaguru. Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi mapema mwaka huu kutembelea Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin,Ujerumani.

Meja Jenerali Milanzi aliongoza msafara wa Tanzania ulioshiriki maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya ITB Berlin 2018 yaliyofanyika Ujerumani yakishirikisha taasisi tano za serikali na kampuni binafsi 60 kutoka Tanzania. Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Ujerumani, Profesa Johannes Vogel alimueleza Meja Jenerali Milanzi kuwa shughuli kubwa inayofanywa na makumbusho hiyo ni utafiti kwa ajili ya maendeleo ya sayansi, elimu na ufahamu wa mambo mbalimbali kuhusu dunia.

Akizungumzia fursa zilizopo za kushirikiana kutafiti maeneo yaliyogundulika masalia ya mijusi hao na viumbe wengine, Profesa Johannes alisema makumbusho yake yapo tayari kushirikiana na wanasayansi wa Tanzania ili kujenga uwezo wa kufanya utafiti na kupata matokeo yatakayochangia katika hazina ya maarifa na sayansi ya viumbe na mazingira. “Masalia ya mjusi huyu yachukuliwe kuwa urithi wa dunia nzima na hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha urithi huu hauachwi ukapotea. Hivyo, ni vema tukaimarisha utafiti katika eneo walikopatikana ili kupata masalia mengi zaidi na kuitangaza Tanzania katika nyanja za utafiti," anasisitiza profesa huyo.

Anasema Makumbusho ya Ujerumani ipo tayari kufanya ziara ya kuimarisha mazungumzo na mamlaka za Tanzania ili utafiti katika eneo la Tendaguru uendelee kwa manufaa ya Tanzania na dunia nzima.Kwa upande wake, Milanzi aliahidi kutoa ushirikiano ili kuwezesha tafiti hizo kufanyika Tanzania kwa ajili ya ustawi wa sayansi na uchumi wa nchi zote mbili. Makumbusho ya Berlin ina mikusanyo mingi ya viumbe mbalimbali zaidi ya milioni 30 ikiwemo ya mijusi kutoka nchi nyingine duniani. Mkusanyiko huo kwa pamoja unatoa mvuto kwa watafiti na watalii kutembelea na kufanya shughuli zao chini ya makumbusho hiyo.

Kuendelea kuwepo masalia ya mjusi huyo katika makumbusho hiyo kuna manufaa zaidi ya kuitangaza Tanzania kiutalii na utafiti wa kisayansi kuliko masalia hayo kurejeshwa nchini Tanzania kwa kuwa mjusi huyo ni balozi wa utalii na utafiti wa kisayansi anayeitangaza Tanzania sehemu mbalimbali duniani.

Makala imeandikwa kwa msaada wa mitandao na Albano Midelo ambaye ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917.

HAKUNA ubishi kwamba ili kuimarisha biashara yoyote ile duniani, zikiwemo ...

foto
Mwandishi: Albano Midelo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi