loader
Picha

Watendaji waagizwa kudhibiti bidhaa feki

WATENDAJI wote wa taasisi za serikali waliopo katika mipaka ya nchi, wametakiwa kuwa wazalendo wa kweli kwa kudhibiti bidhaa zisizo na ubora, kuingia nchini ili nchi isiwe jalala la bidhaa zisizo na ubora kwa walaji na watumiaji.

Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante Ole Gabriel ametoa agizo hilo kwenye eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Alisema hayo alipotembelea Kituo cha Pamoja cha Forodha kati ya Tanzania na Kenya, kujionea utendaji kazi na kuona changamoto zinazowakabili watendaji wa taasisi 15 za serikali zilizopo katika kituo hicho.

Ole Gabriel alisema watendaji wasiwe sehemu ya matatizo, bali wawe sehemu ya kutatua changamoto zilizopo katika kituo cha Namanga ikiwamo kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zinakuwa na ubora wenye kiwango kinachostahili kwa mlaji na mtumiaji.

Alisema kuruhusu kuingiza bidhaa zisizo na ubora yaani bidhaa feki ni kuingiza nchi na wananchi wake katika matatizo makubwa na hilo halitavumiliwa kwa mtendaji yeyote aliyefanya hivyo kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yake ili iwe fundisho kwa wengine.

Alisema watendaji wote wa taasisi zote za serikali waliopo mipakani mwa nchi, wanapaswa kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zinakidhi viwango ili kulinda bidhaa za nchini.

Alisema nchi iendelee wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli, ikiwamo kufanya kazi kwa bidii bila ya kusukumwa na kufuata misingi mizuri ya kazi bila ya kushawishiwa na rushwa kwa lengo la kuingiza nchi katika hasara kubwa kiuchumi.

“Tunatakiwa kuwa wazalendo wa kweli na tusiwe watu wa kupokea misaada bali tunapaswa kuwa watoa misaada,” alisema

Akizungumzia biashara, alisema mpaka wa Namanga ni kati ya mipaka ya nchi yenye kufanya vema katika biashara, hivyo aliwataka wakuu wa idara za serikali mpakani hapo kuhakikisha wanaboresha utendaji kazi wao wa kila siku na kuondoa changamoto zilizopo ili mfanyabiashara na mwananchi aweze kupata huduma bila ya urasimu wowote.

Katibu huyo alisema hatua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Kituo cha Namanga pekee yake kukusanya mapato ya serikali zaidi ya Sh bilioni 55 na kuvuka malengo ya Sh bilioni 54 kwa mwaka, ni hatua nzuri na ya kupongezwa.

Meneja Msaidizi wa Forodha Mkoa wa Arusha, Edwin Iwato alisema taasisi zote za serikali katika kituo hicho, zinafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na ndio maana ukusanyaji na utendaji kazi unakuwa mzuri na wenye ufanisi.

Alisema wastani wa magari makubwa malori 50 hadi 100 hupita kwa kuingia na kutoka yakiwa na bidhaa mbalimbali kila siku.

Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani Tanzania, John Mduma aliwataka wafanyabiashara kufanya biashara safi na zenye usafi na kuwasisitiza kulipa kodi halali kwa bidhaa wanazoingiza na kuzalisha.

ILI Tanzania ijenge Uchumi wa Viwanda, hadi kufikia mwaka 2025 ...

foto
Mwandishi: John Mhala, Longido

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi