loader
Picha

Ligi Daraja la Kwanza ifufue netiboli

CHAMA cha Netiboli Tanzania (Chaneta) kimeandaa mashindano ya mchezo huo ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara yatakayofanyika jijini Mwanza kuanzia Agosti 12 hadi 26 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Ligi Daraja la Kwanza au Klabu Bingwa ya Taifa kama yanavyojulikana kwa jina jingine, ndio mashindano makubwa kabisa ya netiboli yanayoshirikisha klabu hapa nchini na yanayotoa wawakilishi watakaoshiriki mashindano ya Afrika Mashariki.

Tayari jumla ya timu 15 zimethibitisha kushiriki mashindano hayo, huku nyingine tano zikitangaza rasmi kutoshiriki mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali.

Uongozi wa Chaneta kwa sasa unafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa na kuwa na msisimko ili kurejesha uhai wa mchezo huo hapa nchini.

Hakuna ubishi kuwa netiboli ilikuwa miongoni mwa michezo sio tu iliyopendwa sana hapa nchini, bali pia ulikuwa mmoja wa michezo Tanzania iliyokuwa ikifanya vizuri kimataifa huko nyuma.

Miaka ya nyuma kulikuwa na timu kama Bora, Bima, Tanesco, Jeshi Stars, Magereza Kiwira, AICC ya Arusha, Uda na zingine, ambazo zilileta msisimko katika mchezo huo hapa nchini na zile zilizoshiriki mashindano ya kimataifa, nazo zilifanya vizuri na kutamba.

Baadaye, mchezo huo kama michezo mingine uliporomoka na kuanguka kabisa kabla ya miaka ya hivi karibuni kuinuka tena wakati wa uongozi wa akina Anna Bayi, ambao waliuinua mchezo huo hadi Tanzania kufi kia nafasi ya 13 kwa ubora duniani baada ya kushiriki mashindano mengi ya kimataifa na kufanya vizuri.

Mbali na kupanda kiviwango duniani, Tanzania pia iliwahi kutoa wachezaji wa kulipwa waliokwenda kucheza mchezo huo nje ya nchi kama Singapore, ambako mbali na kujipatia fedha nzuri, pia waliitangaza nchi kimataifa.

Tanzania ilikaribia kushiriki mashindano ya dunia kama ingefanikiwa kufi ka katika nafasi ya 10 kwa viwango vya ubora duniani, lakini haikuwa hivyo na badala yake iliporomoka na kuondoka kabisa katika viwango hivyo.

Na hii ilitokea baada ya kuingia kwa uongozi mpya, ambao ulishindwa kabisa kufuata nyayo za akina Bayi, ambao walipambana na kuuinua mchezo huo kitaifa na kimataifa na kuwa tishio kweli kweli na mchezo wenyewe kupendwa zaidi nchini. Kwa sasa Tanzania sio tu haimo katika orodha ya timu zilizomo katika viwango vya ubora duniani au Afrika, ila pia inadaiwa ada na Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (INF) kwa miaka mingi.

Sasa kuna uongozi mwingine, ambao umeonesha mwelekeo wa kimaendeleo kwa kuelekeza nguvu zake kwa kuanza na kutoa mafunzo ya makocha na waamuzi, ambao wengi ni walimu wa shule za msingi.

Uongozi huo unatakiwa kutumia mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza yatakayofanyika Mwanza kuimarisha zaidi mchezo huo, huku klabu shiriki zinatakiwa kujiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo ili apatikane bingwa mwenye uwezo kweli.

Ili kufanikisha ligi hiyo, Chaneta mnatakiwa kusaka wadhamini watakaowapunguzia mzigo wa gharama za uendeshaji wa ligi hiyo, ambayo bingwa wake mtetezi ni JKT Mbweni huku mshindi wa pili alikuwa Jeshi Stars katika mashindano yaliyopita.

Chaneta msiendeshe mashindano kwa kutegemea tu fedha za ada ya ushiriki kutoka kwa timu hizo 15, kwani fedha hizo hazitatosha na bila shaka mtaendelea kusuasua tu na kuurudisha nyuma mchezo huo.

Ni matarajio yetu kuwa mashindano hayo yataendeshwa vizuri na timu zitaonesha ushindani mkubwa na kumpata bingwa wa ukweli, ambaye ataliwakilisha vizuri taifa kimataifa.

WATANZANIA juzi walikesha wakishangilia baada ya timu yao ya soka ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi