loader
Picha

Tume kupanga bei ya gypsum

TUME ya Madini Tanzania inapanga kuweka bei elekezi ya kuuza madini ya jasi (gypsum) nchini kwa kuwa wanunuzi wanawapunja wazalishaji kwa kununua madini hayo kwa bei ndogo zaidi.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini Tanzania, Profesa Idris Kikula ametoa msimamo huo baada ya kutembelea mgodi wa jasi Kijiji cha Manda, Kata ya Manda wilayani Chamwino.

Alisema, wameamua kuweka bei elekezi kudhibiti wanunuzi kujipangia bei ya chini. Alisema mchakato utafanyika mapema ili kuweka uwiano wa bei kati ya wazalishaji na watumiaji wa madini kuondoa upunjaji uliopo.

"Bei elekezi ikiwekwa kutakuwa na uwiano wa bei ya wazalishaji na wanunuaji badala ya utaratibu wa sasa ambao viwanda vinanunua kwa bei kandamizi," amesema Profesa Kikula.

Mmoja wa wazalishaji, Daniel Tamwemezi amesema wazalishaji wanashindwa kuuza bidhaa hiyo kwa kukosa soko na wakipata wanunuzi wananunua kwa bei ndogo na wanapata hasara.

Amesema wameshindwa pia kuuza madini hayo nje ya nchi kutokana na serikali kuzuia ili madini yaongezewe thamani kupata bei nzuri.

Amesema wenye viwanda vya saruji wamekuwa wakinunua kwa Sh 57,000 kwa tani bei ambayo ni ndogo na hairudishi gharama za uzalishaji.

Samwel Msanjila alisema changamoto yao kubwa ni ukosefu wa soko nchini hivyo kufanya viwanda kutumia mwanya kuwakandamiza.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Manda, Chamwino, Michael Mpanduka amesema, kwa kukosa soko, hata kata hiyo na kijiji hicho wamekosa mapato na wananchi wake wana hali ngumu kimaisha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Manzase, Kambona Matonya aliomba serikali iwaruhusu wazalishaji kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi ili kijiji kinufaike.

WAKUU wa Mikoa ya Tabora na Geita, wamesema Jukwaa la ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Chamwino

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi