loader
Picha

'Ushiriki wa vijana muhimu kukuza kilimo'

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama amesema ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo utachochea kasi ya ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza uzalishaji nchini.

Akizungumza mkoani Njombe alipotembelea mashamba ya wakulima wa majani ya chai kijiji cha Luangu, Kata ya Uwemba kunakojengwa kiwanda cha Unilever kitakachosindika chai ili kuwainua kiuchumi wakulima, Waziri alisema vijana wana nafasi kubwa kuleta mageuzi makubwa sekta ya kilimo kubadilisha maisha.

“Serikali imeleta mageuzi katika sekta ya kilimo kufanikisha azma yake ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025,” alisema.

Alisema sekta hiyo ina fursa lukuki na endapo vijana wengi watazitumia, maisha yatabadilika haraka na uzalishaji utaongezeka, sekta kukua.

Waziri alipongeza pia Kampuni ya NOSC kununua majani ya chai kutoka kwa wakulima wadogo wadogo walioungana kwenye ushirika mkoani Njombe kuendeleza kilimo hicho huko.

Alisema mpango wa ubia kati ya sekta za umma na binafsi ni mzuri ndio maana serikali iliamua kuuanzisha ili kuhakikisha kuna kituo kimoja na ukifanyika mpango wa mageuzi, ukasimamiwa vyema, sekta ya kilimo nchini itafanikiwa zaidi.

“Tuna mikakati mingi ya kuboresha kilimo na wa kisera kuwezesha wananchi kiuchumi. Uwezeshaji huo kwa asilimia kubwa unachangiwa na kilimo,” alisema waziri huyo.

Akizungumzia mradi wa kiwanda cha Unilever utakaonunua majani ya chai yenye ubora kutoka kwa wakulima unaoratibiwa na NOSC, waziri alisema kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ambao ndiyo waratibu watahakikisha wanazileta sekta zote pamoja ndio maana amefanya ziara ya kuja kujifunza na kuangalia kuwa mazao makubwa ya kimkakati yanatengenezewa mfumo mzuri.

“Ninatambua na kupongeza juhudi za wadau wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT),” alisema na kuongeza kuwa serikali inaunga mkono hilo.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya NOSC, Filbert Kavia alisema kampuni yake ina mkakati wa kuwaendelea wakulima wadogo wa chai huko.

Alisema kuna mradi wa chai wa Njombe Vision unaowahusisha wadau wakubwa watano. Kavia alisema mdau mkubwa wa kwanza ni kufanya kazi ya ubia na Sagcot iliyounganisha sekta za umma na binafsi na kuzitatua changamoto.

Alisema NOSC ina mkakati wa kumsimamia mkulima mdogo wa chai kuzalisha chai yenye ubora unaotakiwa na kupeleka katika kiwanda cha Unilever kuchakata mazao na kuuza nje.

“Lengo la mradi huu ni kutoa ajira za moja kwa moja au za kupitia mashambani. Nosc sasa hivi tupo katika mpango kupitia Woods Foundation na Halmashauri ya Mji wa Njombe na Sagcot kupima mashamba na kuhakikisha wanapata hati miliki. Hii ni chachu kubwa kuhakikisha vijana wanakuja kujiunga. Kipaumbele ni vijana wajiunge kwenye ushirika,” alisema Kavia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sagcot, Geoffrey Kirenga alisema kilimo cha chai kinaweza kupanda kutoka tani 35,000 ambazo zimekuwa zikizalishwa kwa miaka 10 ikilinganishwa na Kenya ambayo imekuwa ikizalisha tani 450,000 iwapo wataalam wa kilimo wataendelezwa.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafi kisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Njombe

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi