loader
Picha

Kichuya, Okwi, Ndemla wafunika

WACHEZAJI Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi, Saidi Ndemla na Jonas Mkude jana walifunika katika utambulisho kwa mashabiki wa timu hiyo. Mbali na wachezaji hao, kocha msaidizi, Masoud Djuma naye alifunika kwa kupata shangwe nyingi za mashabiki wa Simba.

Simba, jana ilihitimisha tamasha lake, Simba Day linalofanyika Agosti nane ya kila mwaka kwa takriban miaka 10 sasa.

Tamasha hilo huwa maalumu kwa kutambulisha wachezaji wao na benchi la ufundi kwa mashabiki, lakini pia hutumika kutambulisha jezi zao itakazovaa ugenini na nyumbani katika msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

Hata hivyo jana tamasha hilo liliboreshwa zaidi kwa kutambulishwa kikosi cha timu ya vijana, Simba B na kikosi cha timu ya wanawake, Simba Queens.

Baada ya utambulisho wa vikosi hivyo uliofanywa na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara ukaja utambulisho wa timu ya wakubwa ambapo wachezaji hao na kocha Djuma walifunika wenzao kwa kupigiwa shangwe nyingi zaidi na mashabiki waliojaza uwanja.

Kichuya

Alipotajwa uwanja mzima ulizizima kwa shangwe, hasa baada ya Manara kusema kuwa ndiye mchezaji aliyetoa pasi nyingi za mabao msimu uliopita.

Shangwe hizo zilitoa tafsiri kwamba Kichuya anakuwa miongoni mwa wachezaji vipenzi vya mashabiki.

Okwi

Akiwa mchezaji pekee kwenye kikosi hicho aliyekuwepo wakati Simba inafanya tamasha hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2009, naye shangwe nyingi zilimiminika juu yake.

Mashabiki walilipuka kwa shangwe hasa pale Manara alipotangaza kuwa ndiye mfungaji bora msimu uliopita.

Okwi bado kipenzi cha mashabiki wa Simba kama ilivyo siku zote anapoichezea timu hiyo.

Mkude

Anastahili kupendwa na mashabiki kwani amekuwa mvumilivu katika hali zote za Simba na kuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo. Jina lake lilipotajwa jana, uwanja ulilipuka kwa shangwe huku mashabiki wakiimba jina lake, Mkude, Mkude, Mkude.

Ndemla

Shangwe za jana baada ya jina lake kutajwa lilidhihirisha furaha za wanasimba kumbakiza mchezaji huyo kwa msimu mwingine.

Ndemla alimaliza mkataba wake na kabla ya kusaini mwingine kulikuwa na tetesi kwamba anawaniwa na watani wa jadi wa mabingwa hao, Yanga na kwamba alikuwa kwenye hatua nzuri za kumwaga wino.

“Walisema wanamchukua! Sasa amebaki nyumbani, Said Ndemla,” alitangaza Manara kwa madaha.

Djuma

Hakuna siri kwamba kocha huyu ametokea kuwa kipenzi cha wana Simba.

Wanavyomzungumza vijiweni, wanavyomfurahia wakimuona inadhihirisha kwamba mashabiki wa Simba ‘hawapindui’ kwa Djuma.

Jana utambulisho wake ulizusha shangwe kubwa pengine kuliko watu wote wa benchi la ufundi waliotambulishwa.

Pengine ni kutokana na kuwa kijana na namna anavyojiweka karibu na mashabiki wa timu hiyo, lakini pia jinsi anavyomudu mbinu mbalimbali za kuwadhibiti wapinzani hasa anapoachwa kuliongoza benchi la ufundi mwenyewe, ndicho kinachowavutia wana Simba.

Wachezaji wengine waliotambulishwa jana mbali na hao ni Ally Salim, Abdul Suleiman, Rashid Juma, Paul Bukaba, Mohammes Hussein, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Nicholas Gyan, Mohamed Ibrahim, James Kotei.

Wengine ni Yusuf Mlipili, Asante Kwasi, Aishi Manula, Deogratius Munishi, Marcel Kaheza, Adam Salamba, Hassan Dilunga, Sergio Wawa, Mohamed Rashid, Meddie Kagere, Cletus Chama na John Bocco.

KAMPUNI ya MultiChoice imetangaza kuonesha michezo yote ya michuano ya ...

foto
Mwandishi: Rahimu Fadhili

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi