loader
Picha

Majuto kuzikwa leo, hoteli zafurika

PILIKAPILIKA na hali ya taharuki ilikuwa kubwa mkoani Tanga tangu kupata taarifa za kifo cha gwiji wa vichekesho nchini, Amri Athumani ‘King Majuto’ juzi usiku.

Majuto alifikwa na umauti juzi usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu tangu aliporudi nchini kutoka India, alikoenda kwa matibabu zaidi mwezi uliopita.

Mpaka jana mchana hoteli za Tanga na nyumba za wageni mjini Tanga, zilijaa wageni waliofika kwa ajili ya maziko ya Majuto, anayetarajiwa kuzikwa leo baada ya swala ya Ijumaa.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Familia, Suleiman Msei, Majuto atazikwa katika shamba lake lililopo eneo la Kiliku, nje kidogo ya jiji la Tanga.

Tangu kutokea msiba huo, viongozi mbalimbali na waombelezaji wamekuwa wakimiminika nyumbani kwake Donge mjini hapa kutoa pole.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella alisema serikali imeweka mazingira katika usalama, tayari kwa maziko ya gwiji huyo wa filamu na maigizo ya vichekesho.

Jijini Dar es Salaam, wadau wa sanaa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais John Magufuli na Rais mstaafu Jakaya Kikwete jana waliongoza maelfu ya watanzania, kuaga mwili wa msanii huyo mkongwe kwenye viwanja vya Karimjee Dar es Salaam.

Kabla ya kupelekwa Karimjee, mwili wake uliswaliwa kwenye Msikiti wa Maamur, Upanga, Dar es Salaam.

Viongozi wengine waliofika viwanja hivyo kumuaga gwiji huyo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, Mbunge wa Viti Maalumu CCM Pwani, Zainabu Vullu na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir.

Pia, alikuwepo Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa na wasanii mbalimbali. Akizungumza viwanjani hapo, mtoto wa Majuto, Ashraf alisema baada ya kuagwa, mwili huo utasafirishwa kwenda Tanga kwa maziko.

“Saa 10:00 jioni leo (jana) tutausafirisha mwili wa baba yetu kwenda Tanga kwa ajili ya maziko ambayo yatafanyika kesho (leo) nyumbani kwake,” alisema Ashraf.

Alisema hali ya baba yake ilibadilika juzi saa 9:00 alasiri, alipokuwa amelazwa katika Wodi ya Jengo la Sewahaji na kulazimika kupelekwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Ilipofika saa 1:30 usiku hali yake ilibadilika ghafla na madaktari walijitahidi kunusuru uhai wake, lakini saa 2:00 usiku aliaga dunia.

Salamu za rambirambi za Rais Rais Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe kutokana na kifo cha King Majuto na kusema atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu kwenye sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alielimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za chama na serikali katika kuhimiza maendeleo.

“King Majuto alikuwa kielelezo cha safari ndefu ya sanaa kwa nchi yetu, kwa muda wote amedhihirisha kipaji, ujuzi na uwezo wa hali ya juu katika uigizaji na uchekeshaji na hivyo kuwa kipenzi cha Watanzania na wasanii wenzake, hatutasahau ucheshi wake, upendo na uzalendo kwa nchi yake wakati wote wa uhai wake," alisema Rais Magufuli.

Januari 31 mwaka huu, Rais alikwenda kumjulia hali King Majuto, alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili, kabla ya kusaidia safari yake kwenda India kutibiwa katika Hospitali ya Apollo Mei 4 na kurejea nchini Juni 22, mwaka huu, akisema yuko fiti baada ya kufanyiwa upasuaji.

Hata hivyo, alifikia hospitali baada ya kurudi India. Baadae aliruhusiwa kutoka hospitali na kutangaza rasmi kustaafu shughuli zote za sanaa kwa sababu za kiafya. Wiki iliyopita alikimbizwa tena katika Hospitali ya Muhimbili, baada ya hali yake kuwa mbaya hadi alipoaga dunia.

Wasanii wamlilia Msanii Lucas Mhuvile ‘Joti’ aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa : “King Majuto umetuachia maumivu makubwa sana katika tasnia ya komedi Tanzania, sisi wanao tutakukumbuka kwa kazi zako, upendo wako, tabasamu lako daima milele, tulikupenda sana ila Mungu amekupenda zaidi, pumzika kwa amani Mzee wetu”.

Mwigizaji wa Vichekesho, Steve Nyerere naye aliandika "Kweli kaka, Mzee wetu katutoka. Tunalia kwa kumpoteza Mzee wetu".

King Majuto ndiye mwigizaji wa kwanza, kuandaa kazi zake katika mikanda na kuuza, huku akifanya kazi na Shirika la Filamu Tanzania, Tanzania Film Company (TFC).

Baadaye alijiunga na kundi la sanaa la Muungano Cultural Troupe chini ya Dk Norbert Chenga na Tanzania One Theatre (TOT) chini ya Kapteni John Komba (marehemu), kisha aliamua kufanya kazi zake binafsi.

King Majuto atabaki kuwa msanii mkubwa kwenye historia ya sanaa za filamu na uchekeshaji Tanzania na ameigiza zaidi ya filamu 1000 Buriani King Majuto, Mola akupumzishe kwa amani. Innalilahi Wainailahi Rajiun

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafi kisha ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu, Dar na Tanga

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi