loader
Picha

Polisi aeleza alivyomkamata Halima Mdee

MKUU wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, Batseba Kasanga ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa alimkamata Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) nyumbani kwa wazazi wake wanaoishi Ubungo Kibangu, Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa, Julai 3, mwaka jana katika maeneo ya Ofisi za Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Dar es Salaam mwanasiasa huyo  alimtukana Rais John Magufuli kwamba "anaongea hovyo hovyo anatakiwa afungwe breki", kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Kasanga ambaye ni shahidi wa tatu wa upande wa mashitaka, amedai mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba kuwa, Julai 4, mwaka jana alipokea agizo kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, Mark Njela aliyemtaka kwenda nyumbani kwa wazazi wa Mdee, Ubungo Kibangu ili kumkamata Mdee kwa tuhuma hizo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, Kasanga alidai alipofika nyumbani kwa wazazi wa Mdee, mama mzazi wa Mdee aliwaeleza wamsubiri Halima kwa kuwa alikuwa amepumzika kidogo.

Amedai walikwenda nyumbani huko, kwa kutumia gari la doria akisaidiana na askari wawili na walipofika walipokewa na kaka yake Mdee ambaye aliwaelekeza kwa mama yao.

Kasanga alidai baada ya kusubiri kidogo, Mdee alitoka na wakamueleza kuwa wamekwenda kumkamata na kumpeleka Oysterbay Polisi na kwamba wakati huo alikuwa yupo vizuri na baadhi ya ndugu zake walitoka wakaongozana naye kwenda kituoni hapo.

“Tulipofika Oysterbay Polisi, Njela hakuwepo hivyo nilimpigia simu na kunielekeza nimkabidhi Mdee kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (RCO), Davis Msangi,” alidai Kasanga.

Pia alidai kuwa baada ya kumkabidhi kwa Mdee kwa RCO Msangi aliondoka na kurudi kituoni kwake kuendelea na majukumu yake.

Hata hivyo, alieleza kuwa yeye alikuwa hajawahi kumuona Mdee ana kwa ana na alikuwa akimsikia katika vyombo vya habari, ikiwamo luninga na magazeti.

Shahidi huyo alidai tangu alivyomkamata hadi sasa, hakuwahi kuyafuatilia maneno yaliyotamkwa na mbunge huyo. Mdee anatetewa na mawakili Peter Kibatala na Hekima Mwasipu.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 11, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na mashahidi wa upande wa mashitaka.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafi kisha ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi