loader
Picha

Mfumuko wa bei wapungua

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetangaza kwamba mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Julai mwaka huu, umepungua hadi kufikia asilimia 3.3 ikilinganishwa na asilimia 3.4 katika mwezi Juni, mwaka huu.

Akitangaza jana jijini hapa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Ephraim Kwesigabo alisema mfumuko wa bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini na hivyo imepungua kutoka mwezi uliotangulia.

Kwesigabo alisema kupungua kwa mfumuko wa bei, kunamaanisha kwamba kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka uliohishia Julai, mwaka huu, imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwa kwa mwaka ulioishia Juni, mwaka huu.

Kwesigabo ambaye kitaaluma ni Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii alisema, kupungua kwa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu, kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula.

"Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kati ya Julai mwaka jana na Julai mwaka huu, ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 9.5.

"Vyakula vingine ni mtama kwa asilimia 17.8, unga wa mihogo kwa asilimia 14.1, matunda jamii ya machungwa kwa asilimia 22.2, maharage kwa asilimia 5.8 na mihogo mibichi kwa asilimia 12.5," amesema Kwesagabo.

Hali ya mfumo wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki (EAC), Uganda mfumo wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Julai mwaka huu umeongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 2.2 kwa mwaka unaoishia mwezi Juni mwaka huu.

Alisema kwa upande wa Kenya, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Julai mwaka huu, umeongezeka hadi asilimia 4.35 kutoka asilimia 4.28 kwa mwaka ulioshia Juni, mwaka huu.

Alisema kupungua kwa mfumo wa bei kwa kiwango hicho hadi kufikia asilimia 3.3 kulitokea takribani miaka 15 iliyopita haujatokea katika kipindi chote cha katikati.

NBS ndiyo taasisi yenye wajibu na mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji wa Takwimu rasmi nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za mfumuko wa bei kwa ajili ya matumizi ya serikali na wadau wa takwimu nchini.

Akizungumzia mfumo wa bei kupungua nchini, Katibu Mtendaji wa Chama cha wenye Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) jijini Dodoma, Idd Senge alisema umepungua kutokana na ukweli kwamba uzalishaji wa mazao mwaka jana na mwaka huu umekuwa mzuri hivyo kuna chakula kwa wingi.

Lakini pia Watanzania wamekuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha na kununua bidhaa kutokana na ukweli kwamba mtu hawezi kutumia fedha kwa sababu hana uhakika wa kupata nyingine kesho.

Alisema tabia hiyo ya nidhamu ya fedha imekua miongoni mwa Watanzania kuanzia kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, hivyo watu wamekuwa wakitumia jasho lao na hakuna nyongeza kwenye jasho lao, hivyo mapato na matumizi yanafanyika kwa adabu tofauti na zamani.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi