loader
Picha

Halmashauri zaagizwa zitoe vifaa badala ya fedha

VIONGOZI wa Halmashauri za wilaya nchini wametakiwa kubadili mfumo wa kuviwezesha vikundi kwa kutoa vifaa badala ya fedha.

Badala ya kutoa fedha taslimu kwa vikundi vya akinamama, vijana na wenye ulemavu, sasa wametakiwa kutoa vifaa vya ufundi, sayansi na teknolojia vitakavyosaidia vikundi kuanzisha, kukuza na kudumisha miradi ya maendeleo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde ametoa agizo hilo alipozungumza na viongozi wa halmashauri nchini na Wakuu wa Wilaya.

Alizungumza nao wakati akifunga Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati, yaliyokuwa yakifanyika viwanja vya Nzuguni, Dodoma.

"Badala ya kutoa fedha taslimu inatakiwa kutoa vifaa vya ufundi, sayansi na teknolojia ambavyo vitasaidia kuanzisha, kukuza na kudumisha miradi itakayosaidia kuondoa umasikini hasa wa kipato," alisema.

Akifunga maonesho hayo inayohusisha mkoa wa Dodoma na Singida, Mavunde alisema, wakati umefika kuachana na mfumo wa kutoa fedha badala yake vitolewe vifaa vya ufundi.

"Mtindo wa utoaji fedha asilimia nne kwa vikundi vya vijana, nne kwa wanawake na mbili kwa wenye ulemavu, umekuwa hauna tija, kwanza fedha zinazotolewa ni kidogo lakini pia urejeshaji wake umekuwa hauna afya," alisema.

Aliwataka viongozi hao kuweka utaratibu na kubadili mfumo huo wa kutoa fedha ambazo ni sehemu ya mapato yao ya ndani ya kusaidia vikundi hivyo kwani baadhi ya fedha hizo zimekuwa haziwafikii walengwa na hata urejeshaji wa mikopo umekuwa wa kusuasua.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema maonesho ya mwakani yatakuwa bora zaidi kwa kuwa hofu ya kuingiliana na uwepo wa stendi katika viwanja hivyo haupo kwa sababu eneo bado limebaki.

Ameitaka Kamati ya Maandalizi ya maonesho hayo kufanya maandalizi mapema kuboresha zaidi kuliko mwaka huu ilipofanya imechelewa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi amewakaribisha wananchi maonesho ya Kanda ya Kati mwakani mkoani kwake akisema wamejiandaa kufanya maajabu makubwa.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafi kisha ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi