loader
Picha

Mwenyekiti atuhumiwa kuchoma nyumba

MWENYEKITI wa kitongoji cha Rala katika Kijiji cha Buganjo Wilayani Rorya, Peter Ogalo na wenzake sita wamekamatwa kwa tuhuma za kuchoma nyumba ya mkazi wa kitongoji hicho, Odhiambo Matiko baada ya kumtuhumu kuwa anahusika katika wizi wa ng’ombe wawili.

Ng’ombe hao wa Isidoli Chacha wanadaiwa kuibiwa na Odhiambo na nduguye, Onyango. Hata hivyo, uongozi wa kijiji na kata umepinga kukamatwa kwake na wananchi hao wakidai Odhiambo alichoma nyumba yake mwenyewe kwa nia ya kujihami dhidi ya wanakijiji hao.

Diwani wa Kata hiyo ya Bukwe, Charles Wembe amesema katika kijiji hicho, Odhiambo na nduguye Onyango, wanatuhumiwa kwa matukio ya wizi wa mifugo mara kwa mara.

Amesema, Julai 25, mwaka huu ng'ombe wawili mali ya Chacha waliibiwa ambapo wananchi walijitokeza na kufuatilia nyayo na baada ya msako mkali wakishirikiana na askari Polisi waliwapata ng'ombe hao wamefichwa porini.

Amesema hata baada ya kuipata mifugo hiyo, wananchi waliwatilia shaka Odhiambo na Onyango kuhusika na tukio hilo la wizi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Buganjo, Abich Siambe alisema baada ya Odhiambo na Onyango kubaini wanatajwa na wananchi kuhusika na wizi huo, usiku Odhiambo alihamisha mizigo yake ndani ya nyumba, kubomoa milango yake na kuichoma moto.

“Aliiwasha moto nyumba na kutokomea usiku siku hiyo na kesho yake kurejea na kumtuhumu Mwenyekiti wa Kitongoji na wakazi wake kuwa ndio wamemchomea nyumba yake kitendo ambacho uongozi wa Kitongoji, Kijiji na kata tunapingana nacho,” amesema Siambe.

“Hawa watu ni wezi wametusumbua kwa muda mrefu kwa wizi wa mifugo wanayoitorosha kwenda kuiuza Mabera Kenya. Tunaomba Polisi kufanya uchunguzi kuhusu suala hili,” alisema.

Alisema wameitisha mkutano wa kitongoji na kijiji cha Buganjo leo kuwabaini na kuwataja wezi wengine wa mifugo kwa kupigiwa kura na wananchi kukomesha uhalifu katika eneo hilo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Tarime Rorya ACP Yahaya Mdogo alithibitisha kukamatwa kwa Ogalo akisema wanahojiwa kwa tuhuma hizo.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafi kisha ...

foto
Mwandishi: Samson Chacha, Rorya

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi