loader
Picha

ATCL kutua majiji makuu 16 duniani

KATIKA kuhakikisha kuwa Kampuni ya Ndege ya Air Tanzania (ATCL) inapasua anga kikamilifu, imepanga kuwa ifi kapo 2022, ndege zake zitakuwa zikifanya safari kwenye majiji makubwa ya nchi 16 tofauti duniani.

Kwa mujibu wa mpango uliowasilishwa mbele mawakala wakuu wa huduma za ndege na utalii, Kaimu Meneja wa Mauzo na Usambazaji wa kampuni hiyo, Edward Nkwabi alisema kwenye mpango wake utakaoisha 2022, awamu ya kwanza ya huduma za anga za kampuni hiyo kwenda nje mbali na kuanza na Comoro, zinatarajiwa kuwa mwishoni mwa mwezi huu ndege hizo zitaanza na safari Bujumbura, Burundi na Entebbe, Uganda kisha Mumbai nchini India.

Pia alisema kwenye awamu ya pili ya safari za kimataifa zinazotarajiwa kuanza Desemba mwaka huu, ndege za ATCL zitaanza kwenda Harare (Zimbabwe), Lusaka (Zambia), Johannesburg (Afrika Kusini) na Guangzhou, China. Hata hivyo, kwenye mpango huo ambao ni wenye kuonesha kuwa ifikapo 2022, serikali itazidi kujivunia shirika hilo, meneja huyo alisema wanatarajia ndege hizo zitatua Nairobi (Kenya), Lubumbashi (DRC), Kigali (Rwanda), Accra (Ghana), Lagos (Nigeria), Dubai (UAE), Muscat (Oman) na London, Uingereza.

Mpaka sasa kampuni hiyo linafanya safari kwenye maeneo 11, ikiwemo nchi ya Comoro. Kwa mujibu wa mpango huo ulioelezewa na Meneja wa mauzo, kabla ya kumalizika kwa mwaka huu, wanatarajia kuongeza safari zake kwenye miji saba tofauti ambayo ni Mpanda, Iringa, Arusha, Musoma, Pemba, Kahama na Shinyanga. Mawakala 300 Meneja wa Mauzo huyo alisema kuwa wao kama kampuni, mpaka sasa wamesajili mawakala 300 ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye mauzo ya tiketi za ndege za Air Tanzania.

Alisema, “Tumesajili mawakala 300 ambao wote kwa ujumla mpaka sasa wanachangia asilimia 70 ya makusanyo yatokanayo na tiketi.” Mapato yapaa mara 6 Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi akizungumza wakati akijadiliana na mawakala, alisema kuwa mapato ya kampuni hiyo yalipanda kutoka Sh milioni 700 kwa mwaka 2016 hadi kufikia Sh bilioni 4.5 kwa mwaka 2017, hatua ambayo aliitaja kuwa ni nzuri. Alisema, “Mapato yetu yamepanda na hii inatokana na umakini tulioweka kwenye kazi, kuanzia kwa watumishi mpaka kwenye huduma, na kimsingi pia inatokana na sapoti kubwa tunayopata kutoka kwa mawakala wa huduma za anga na utalii. Nawapongeza sana.

“Pia hasara zimepungua kutoka shilingi bilioni 14 mwaka 2016 hadi shilingi bilioni 4.3, hatua ambayo ni nzuri na tunataka kuhakikisha kuwa hakuna hasara na kampuni inakua na kuingizia serikali kipato,” alisema Matindi. Aliongeza kuwa ndege za kampuni hiyo, kwa sasa zinatoa huduma kwa wakati ambapo kwa mwaka 2017/18 huduma zinawahishwa kwa asilimia 90 ukilinganisha na asilimia 66 za mwaka 2016. ATCL yateka soko Akielezea hali halisi ya ukuaji wa kampuni hiyo ikiwemo kuaminika na ndege zake kutumika zaidi, Nkwabi alisema ATCL inazidi kumega sehemu kubwa ya soko la anga na hiyo inatokana na huduma pamoja na kuongezeka kwa ndege kwenye shirika.

Alisema, “Mwaka 2016, kwenye soko kuu la huduma za anga, tulikuwa tunamiliki asilimia 2.4 ya soko hilo, mwaka 2017 tukapanda na tukalimiliki kwa asilimia 6.9 na mpaka Machi mwaka huu, tumelishika soko hilo kwa asilimia 24. “Ni wazi kuwa tunakuwa na tutaendelea kupanda kadiri tutakavyoshirikana na mawakala na pia sisi kutoa huduma bora na kwa wakati,” alisema Meneja huyo.

Marubani, wahandisi wa kutosha Matindi ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji alisema mpaka sasa kampuni hiyo ina wahandisi 50 ambao wote wana utaalamu wa juu wa kuhudumia ndege, na hata hivyo alieleza kuwa kati yao, 12 watahudumia ndege ya aina ya Boeing Dreamliner. Alisema, “Tuna wataalamu, na tunaendelea kupeleka wengine ili wapate ujuzi, kwa Dreamliner tuna marubani wanane ambao wote walifuzu kwenye mafunzo waliyokuwa wakifanya kwenye Shule ya Boeing kule nchini Marekani na tayari wanne wameanza kazi baada ya kumaliza muda wa majaribio.

“Pia tuna wahandisi 12 kwa ajili ya ndege hiyo, na wana mafunzo ya kutosha, lengo letu ni kuwa na wataalamu wa kutosha ambao watahudumia ndege zetu inavyopasa,” alisema Matindi. Mawakala wapongeza Ikiwa ni siku maalumu ya mawakala wa huduma za ndege na uongozi wa ATCL kukutana, waliishukuru ATCL kwa ushirikiano wanaotoa na pia waliipongeza serikali kwa kufufua kampuni hiyo, kwani itapunguzia wananchi gharama lakini pia itatoa ajira kwa watanzania.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na uongozi wa ATCL, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Usafiri (Tasota), Agnes Rwegasira alisema walikutana na ATCL kufahamiana na kuona jinsi wanaweza kufanya kazi kwa pamoja na kufanikiwa. Alisema, “Lengo la kukutana kuoneshwa na ATCL yale ambayo wanayafanya na kusikiliza kwetu kile tunachokitaka, na hii itatusaidia kujua tunashirikiana vipi ili tuweze kuona ATCL inakuwa kubwa na inaaminika duniani kote.”

Mkurugenzi wa Karibu World, Musharaf Dhanji akizungumza kwa niaba ya mawakala wenzake wa huduma za anga na utalii, alisema wao kama mawakala, wanayofuraha kuwa ATCL inapanua huduma na kufika mbali. “Tutapata faida na ATCL itapata faida, hii yote ni matunda ya ujio wa ndege mpya za kampuni, nawapongeza sana kwa kuwa na huduma bora na ushirikiano. Sisi kama mawakala tunaahidi kuendelea kushirikiana,” alisema wakala huyo.

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kutowachagua wagombea uongozi katika Uchaguzi ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi