loader
Picha

Mwarobaini unavyonukia migogoro ya hifadhi, wananchi

KATIKA maeneo mengi nchini watu wamekuwa wakiishi kwa amani na kushirikiana na watumishi wa serikali wa hifadhi za taifa. Hata hivyo, yapo maeneo mengine machache ambako kumekuwepo na migogoro baina ya wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hizo, hivyo kuathiri shughuli za hifadhi na usimamizi wa wanyamapori pamoja na kilimo na ufugaji, hasa malisho. Migogoro hiyo baina ya wananchi na hifadhi imekuwa moja ya masuala yaliyotawala kikao cha Bunge kilichomalizika mjini Dodoma hivi karibuni. Moja ya migogoro hiyo ipo Mpanda Vijijini mkoani Katavi.

Mbunge Rhoda Kunchela anahoji, ni lini serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya hifadhi na wananchi katika Kata ya Kapalamsenga, Isengule na Ikola ulikochukua muda mrefu bila suluhu, hivyo kusababisha usumbufu na hasara kwa wananchi? Je, serikali haioni kuwa mgogoro huo umesababisha umasikini mkubwa kwa wananchi kushindwa kuendeleza shughuli za kiuchumi kwenye maeneo yao hivyo, ifanye haraka kutafuta ufumbuzi? Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga anasema Kata ya Kapalamsenga, Isengule na Ikola zipo wilaya ya Tanganyika (Mpanda Vijijini) na zinajumuisha maeneo ya ushoroba wa wanyamapori ijulikanayo kama Katavi-Mahale.

Ushoroba huo ni njia kuu ya wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa Katavi kwenda Hifadhi ya Taifa Mahale. Kutokana na wanyamapori hususan tembo kupita katika maeneo hayo, wenyeji wanautambua ushoroba husika kama ‘Tembo na Mwana’. Pamoja na ushoroba huo kufahamika kwa baadhi ya wananchi, kulikuwa na mkanganyiko kuhusu eneo sahihi (mipaka ya mapito ya wanyamapori). Hii ilitokana na baadhi ya wananchi na hasa wahamiaji na wafugaji kutoka mikoa ya jirani, kuvamia na kuharibu maeneo ya mapito ya wanyamapori bila kufuata taratibu na kujichukulkia ardhi kiholela.

Katika kutafuta ufumbuzi wa migongano iliyopo juu ya matumizi ya ardhi, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, imechukua hatua mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja na kwanza, kuhakikisha mipaka ya ushoroba inajulikana kwa wananchi kwa kutenga na kuainisha maeneo kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori kama vile sokwe. Hao ni sokwe wanapatikana katika Kata za Kapalamsenga, Ikola, Isengule, Mwese na Kasekese hasa katika safu za milima ya Wansisi na Mgendebe. Pili, kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji na kutunga sheria ndogo za usimamizi wake kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 na 2016/2017.

Kwa sasa vijiji vyote vilivyopo Kata za Kapalamsenga, Ikola na Isengule vimeshafanyiwa mpango shirikishi wa matumizi bora ya ardhi. Pia, eneo la ushoroba wa wanyamapori limebainishwa na kutengwa, hivyo kuondoa mkanganyiko uliokuwepo awali. Aidha, kwa kuwa kanuni za usimamiaji wa shoroba na maeneo mtawanyiko zimeshaandaliwa, serikali ina mpango wa kutafuta suluhu ya kudumu kwa wananchi katika vijiji vyote vilivyopitiwa na shoroba za wanyamapori, vinavyopakana na maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji ili kuondoa migogoro inayohusu umiliki na matumizi ya ardhi. Ni kwa msingi huo anasema, serikali inawaomba wananchi wote waheshimu mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kanuni mpya za ushoroba.

Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha anasema kumekuwepo tabia ya baadhi ya askari wa Hifadhi ya Taifa Serengeti (Senapa) kuwakamata wananchi ndani ya hifadhi na wakati mwingine wasipowaua, huwapeleka mbali na mahakama za wilaya ya Serengeti. Anahoji, je, ni lini kitendo cha mauaji ya watu wanaozunguka Hifadhi ya Serengeti kitakoma na lini askari hao wa Senapa, wataacha kupeleka watuhumiwa waliokamatwa ndani ya hifadhi nje ya mahakama za wilaya.

Hasunga anasema askari wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na miongozo mbalimbali iliyopo. “Ni kweli kwamba baadhi ya wananchi wamekuwa wakikamatwa kwa kufanya shughuli au kuingia kwenye hifadhi bila kufuata taraibu zilizopo,” anasema Hasunga. Anasema wengi wamekuwa wakijihusisha na ujangili ndani ya hifadhi. Kwa msingi huo, askari wa hifadhi huwakamata watuhumiwa wote na kuwafikisha katika Jeshi la Polisi na hatimaye mahakamani kwa hatua zaidi. Kwa mujibu wa Hasunga, jumla ya kesi 437 zimefunguliwa na zipo katika hatua mbalimbali za usikilizaji.

Anasema: “Hifadhi ya Taifa Serengeti imepakana na wilaya nane tofauti. Mtuhumiwa anapokamatwa ndani ya hifadhi anapelekwa katika kituo cha polisi kilicho jirani kwa hatua zaidi. Baadhi ya watuhumiwa wamekuwa na tabia ya kufanya uhalifu kwa kufuata mienendo ya wanyamapori wahamao.” Anatoa mfano akisema, kati ya mwezi Mei na Juni ya kila mwaka, wanyamapori wengi wanahamia maeneo ya Kusini na Magharibi mwa hifadhi, ambayo kiutawala yako wilaya za Bariadi na Bunda.

Hivyo, baadhi ya watuhumiwa kutoka Wilaya ya Serengeti huenda katika wilaya nyingine kufanya ujangili wa wanyapori ambao kwa kipindi hicho hawapatikani kirahisi katika eneo la wilaya yao. Kutokana na hali hiyo, watuhumiwa wamekuwa wakikamatwa na kushitakiwa katika mahakama za eneo au wilaya walizokamatwa wakifanya uhalifu. Anasema, ni vema wananchi wazingatie taratibu zote za hifadhi na kuachana na ujangili ili kuepuka adhabu hizo na washirikiane na serikali kulinda hifadhi za taifa.

Mgogoro mwingine ni kati ya wananchi na Hifadhi ya Wanyamapori Selous. Mbunge Hamida Mohamed Abdallah anasema mgogoro wa ardhi katika Hifadhi ya Selous wilayani Kilwa umechukua nafasi kubwa kati ya serikali na wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hiyo. Anasema: “Mpaka halali haujulikani, kwani mwaka 1994 ulikuwa Mto Matandu na mwaka 2010 mpaka huo ulisogezwa mpaka Bwawa la Kihurumila Kijiji cha Kikulyungu, je, serikali ipo tayari kuhakiki eneo hilo ili kutatua mgogoro uliopo kati yake na wananchi wa Kijiji cha Kihurumila?” Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maliasili, Hasunga anasema Kijiji cha Kikulyungu ni moja ya vijiji tisa vinavyopakana na Pori la Akiba la Selous kwa wilaya ya Liwale.

Ndani ya pori hilo, kuna bwawa lijulikanalo kama Kihurumila ambalo ni sehemu muhimu ya mazalia ya samaki na wanyamapori kama vile mamba. Katika miaka ya 1970 wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu walikuwa wakivua samaki katika bwawa hilo baada ya kupewa vibali maalumu. Hata hivyo, mwaka 1982 serikali ilizuia shughuli za uvuvi kutokana na baadhi ya wananchi kukiuka taratibu za kuvua samaki, ikiwemo matumizi ya sumu. Mpaka wa Pori la Akiba Selous umewekwa kwa kuzingatia Tangazo la Serikali Namba 275 la 1974. Tangu wakati huo hadi sasa mpaka huo haujafanyiwa marekebisho yoyote.

Hata hivyo, wananchi wa Kikuluyungu hawakukubaliana na tafsiri na uhakiki wa mpaka uliofanyika licha ya vijiji vine kukubaliana na uhakiki huo. Aidha, wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu wanadai kwamba Bwawa la Kihurumila ni sehemu ya eneo la kijiji hicho. Wizara hiyo ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilituma maofisa kuhakiki mipaka ya vijiji vitano, kati ya vijiji tisa, vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Liwale vinavyopakana na Pori la Akiba Selous.

Vijiji hivyo ni Kimambi, Kikulyungu, Barikiwa, Chimbuko na Ndapata. Uhakiki huo ulishirikisha pia maofisa kutoka Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi Tanzania (NLUPC), maofisa ardhi wilaya ya Liwale, taasisi isiyo ya kiserikali ya World Wide Fund, wananchi na viongozi wa kata na vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Liwale. Kazi hiyo ililenga kutatua mgogoro wa mpaka na kutangaza WMA ya Liwale. Hata hivyo, wananchi wa Kikulyungu waliwafanyia vurugu wataalam wa Wizara ya Ardhi walipotembelea eneo la mgogoro kwa ajili ya kutafsiri Tangazo la Serikali na kusababisha wataalamu kukimbia kuokoa maisha yao. Kufuatia hali hiyo, wizara imepanga kukutana na viongozi wa Mkoa wa Lindi, akiwemo mbunge huyo, ili kutatua mgogoro huo kwa manufaa ya uhifadhi na ustawi wa wananchi.

Rais John Magufuli amewapa wiki moja ...

foto
Mwandishi: Nelson Goima

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi