loader
Picha

Wafanyabiashara tumieni vizuri muda wa TRA

UAMUZI wa serikali wa kuwasamehe wafanyabiashara na walipakodi riba na adhabu kutokana na malimbikizo ya kodi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Kodi ni chanzo kikuu cha mapato ya serikali yoyote ile duniani katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Wananchi wasipolipa kodi, inakuwa vigumu kwa serikali kuwapatia wananchi hao huduma za jamii kama vile afya, elimu, maji pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, reli, nishati pamoja na kuboresha usafiri wa anga.

Kwa kuzingatia umuhimu na mchango wa walipakodi na wafanyabiashara nchini, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) imeamua kuwasamehe riba na adhabu ambazo wadau hao wa kodi walikuwa wakikabiliana nazo kisheria.

TRA inapaswa kupongezwa kwa uamuzi huo ambao nayo inatekeleza agizo lililotolewa na Rais John Magufuli alipokutana na wafanyabiashara nchini hapa hivi karibuni ambao walimweleza kikwazo kikubwa ni riba ambayo kwao ni kubwa kiasi cha kuwafanya washindwe kulipa kabisa madeni yanayowakabili.

Rais Magufuli akaiagiza TRA iangalie kama inaweza kuwasamehe riba hiyo ili waweze kulipa kodi wanayodaiwa.

Hata hivyo, pamoja na kutimiza agizo hilo, TRA imetoa muda wa miezi sita ili madeni hayo yawe yamelipwa vinginevyo, watalazimika kulipia riba zao kama mwanzo.

Uamuzi huo unazifanya pande zote mbili, yaani walipakodi na wafanyabiashara kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine kuanza upya kutoka pale palipokuwa na mkwamo kutokana na sababu mbalimbali.

Juzi, TRA iliamua kutoa semina kwa wafanyabiashara na walipakodi nchini kwenye Ukumbi wa Mwl Nyerere jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, lakini kubwa zaidi kuwaeleza kusudio la Serikali la kuwasamehe riba na adhabu kutokana na malimbikizo ya kodi zao.

Mwitikio mkubwa wa walipakodi na wafanyabiashara kwenye semina ile, ni ishara tosha kwamba uamuzi wa Serikali ulikuwa sahihi wa kutaka kuwasaidia wadau hao kodi.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Kamishna wa Idara ya walipa kodi wakubwa wa Mamlaka ya Mapato nchini, Alfred Mregi, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, amewataka wafanyabiashara na walipakodi kuanza kupeleka maombi yao kwa ajili ya kupata msamaha huo ndani ya muda uliowekwa.

Nitoe wito kwa Wafanyabiashara na Walipakodi kuzingatia muda waliopewa kwa kuwa siku zote muda ni mali na majuto ni mjukuu.

Majuto daima huwa ni mjukuu kwa sababu katika jambo hili, Serikali imeweka bayana kwamba lengo lake ni kuwasaidia walipakodi na wafanyabiashara kuweza kuinua kiwango chao cha ulipaji kodi kwa hiari.

TRA wameweka wazi kuwa kusamehewa kwa riba na adhabu, kunatoa unafuu kwa wafanyabiashara na walipakodi kulipa kodi wanazotakiwa kisheria pasipo riba na adhabu hizo.

Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikiwasisitiza wananchi kulipa kodi kwa hiari tena kwa wakati ili iweze kutimiza wajibu wake kwa wananchi wote. Kukwepa kodi au kutokulipa kodi kwa wakati ni sawa na kujicheleweshea maendeleo yetu wenyewe.

Utekelezaji wa msamaha huu, utaiwezesha Mamlaka ya Mapato nchini kukusanya Sh bilioni 500 kutoka kwa wafanyabiashara na walipakodi.

KISWAHILI ni kati ya lugha kongwe na yenye historia kubwa ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi