loader
Picha

Bodaboda zingatieni agizo la Lugola

KUMEKUWA na ukiukwaji wa sheria na kanuni zake kwa madereva wa pikipiki zinazofanya biashara ya kubeba abiria na hasa katika ubebaji wake uliopitiliza maarufu ‘mshikaki’ na pia kukatiza kwenye mataa bila kujali sheria za barabarani.

Ni kutokana na tabia hii iliyokithiri, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga marufuku waendeshaji hawa wa bodaboda wanaobeba abiria zaidi ya mmoja kuacha tabia hiyo mara moja ili kuepusha ajali.

Waziri Lugola pia akawataka polisi kutorudi nyuma, wahakikishe wanawakamata na kuwafikisha mahakamani waendeshaji bodaboda wasiofuata sheria za usalama barabarani.

Waziri Lugola aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ragati, Kata ya Kasuguti, Jimbo la Mwibara, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara juzi.

Nasi tunasisitiza kwamba agizo la Waziri Lugola sio tu lizingatiwe na wahusika bali halina budi kutekelezwa kwa nguvu zote kwa mustakabali wa maisha ya Watanzania.

Ni ukweli ulio wazi kwamba wengi wanatumia bodaboda kurahisisha usafiri wa kuwafikisha haraka kwa kukwepa foleni hasa kwa walio mijini, lakini wanaweza kumudu gharama kutokana na uduni wa maisha ikilinganishwa na teksi au bajaji.

Ni kutokana na uduni wa maisha, abiria wengi wanaona ni heri wachangie pikipiki moja au familia moja inaona ni heri itumie fedha kidogo kwa kupakia zaidi ya mtu mmoja kwenye pikipiki moja.

Pamoja na kutumia gharama kidogo, lakini madhara yake yana gharama kubwa ikiwemo ya kupoteza maisha au kupata vilema vya maisha na pengine kutumia fedha nyingi hospitalini baada ya kupata ajali.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba pikipiki ina uwezo wake. Kisheria, mwendeshaji pikipiki anawajibika kubeba lawama kwa kuwa amefunzwa lakini abiria wengine hawana mafunzo yoyote.

Kifungu cha 41A cha Sheria ya Usalama Barabarani kinamtia hatiani mtu yeyote anayesababisha majeruhi au kifo kutokana na kuendesha pikipiki, guta, bajaji au baiskeli.

Pia ni lazima abiria avae helmeti au kofia ngumu ili kuzuia kuumiza kichwa inapotokea ajali.

Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 39 (11) na (12) cha sheria ya Usalama barabarani kinachomlazimisha abiria wa pikipiki kuvaa helmeti.

Tunalikumbusha Jeshi la Polisi na hasa wa usalama barabarani kutumia nguvu ya sheria na kanuni zake kuwakamata waendesha bodaboda wanaohatarisha maisha ya Watanzania kama alivyoagiza Waziri Lugola.

Wapo wachache wanaotii sheria bila shuruti, lakini madereva wa bodaboda walio wengi wanahitaji nguvu ya ziada katika kuhakikisha wanafuata sheria.

Tunasema hivyo kwa kuwa, mishikaki, kutovaa kofia ngumu na kukatiza kwenye mataa limekuwa ni suala la kawaida kwa madereva hawa na polisi wa usalama barabarani wameshindwa kabisa kuwadhibiti kwani wanapita mbele yao bila kuchukuliwa hatua.

Ifike mahali, kama madereva hawa hawataki kufuata sheria, walazimishwe kwa kuwa wamesababisha vifo vingi kwa watu wasiokuwa na hatia, majeruhi wengi na kuacha majonzi kwa familia nyingi hapa nchini.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi