loader
Picha

Mikoa 5 hatarini kupata ebola

MIKOA mitano Tanzania iko katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa ebola. Ugonjwa huo upo katika nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) hasa kwenye jimbo la Kivu Kaskazini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema jijini Dar es Salaam kuwa, mpaka sasa bado Tanzania haina mgonjwa wa ebola.

Ameitaja mikoa iliyo hatarini kuwa ni Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi na Songwe kwa kuwa inapakana na DRC. Katika siku 10 tangu kutangazwa kuibuka upya kwa ugonjwa huo kuna wagonjwa 91 nchini humo.

Waziri Ummy amewataka wakuu wa mikoa katika maeneo hayo, kuitisha kikao cha dharura na cha msingi chenye kueleza namna wanavyoweza kukabiliana na suala hilo pindi akitokea mgonjwa watakayemhisi katika eneo husika.

Amesema Tanzania ina maeneo matatu yanayoweza kupima na kuthibitisha sampuli za ugonjwa huo ambapo ni katika maabara ya Taifa, maabara iliyopo katika Hospitali ya KCMC na Hospitali ya Mbeya.

Amezitaja dalili za ebola kuwa ni pamoja na homa, kichefuchefu na kutapika, kuharisha, vidonda vya koo, kuumwa kichwa, maumivu ya misuli, kusumbuliwa na tumbo, kuchoka na hata kukosa hamu ya kula.

Amesema kuibuka upya kwa ugonjwa huo katika nchi hiyo kumetokea katika Jimbo la Kivu Kaskazini na Ituri, maeneo yaliyoelezwa kupakana kwa karibu na nchi za Rwanda na Uganda na kuiweka Tanzania katika hatari kubwa.

“Hili jambo ni kubwa, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeiweka Tanzania katika hatari ya maambukizo maradufu hasa ikizingatiwa machafuko ya migogoro ya watu katika eneo hilo na hatari ya kukimbilia mipakani,” amesema Waziri Ummy huku ikisisitiza kuwa ugonjwa huo hauna dawa.

Alisema Tanzania iko katika hatari kubwa na wasiwasi unaongezeka zaidi kutokana na kuwepo kwa njia za panya zilizo wazi, ingawaje hadi sasa Tanzania haina mgonjwa wa ebola.

Kuhusu mikoa hiyo alisema ni muhimu kwa viongozi wa afya kuelewa dalili za ugonjwa huo ili kuongeza tahadhari hata katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KIA) na uwanja wa Songwe.

Alisema katika mikoa hiyo, wakuu wa mikoa ni muhimu kuwa na kikao hicho cha msingi ili kujiridhisha iwapo watapata mgonjwa watakayekuwa na wasiwasi naye kujua hatua muhimu zinazotakiwa kichukuliwa kwa haraka.

Alisema ni muhimu kujua namna ya kuchukua sampuli kwa haraka na zinapelekwa katika maabara zipi na kwa usafiri gani na maeneo ya kuweka mgonjwa pindi atakapohisiwa.

Kuhusu maandalizi kwa Tanzania, alisema tayari wataalamu wapya 33 wameajiriwa kwa vituo vya afya vya mkoani, kufuatilia wasafiri katika maeneo mbalimbali na wiki ijayo yatatolewa mafunzo kwa wataalamu wengine 80 katika maeneo ya mipakani ili kuwajengea uwezo katika mikoa ya Mwanza, Kigoma na Kagera.

Kadhalika, alisema mganga mkuu wa serikali pamoja na timu kutoka Wizara ya Afya watakwenda katika mikoa hiyo kufuatilia kwa ukaribu.

Mlipuko wa ebola kwa DRC ni wa mara ya 10 na tangu kutangazwa kwa awamu hii kuanzia Agosti 10, mwaka huu kulikuwa na wagonjwa 26 na vifo 10 na kwa kipindi cha siku 10 wagonjwa hao wamefikia 91 na vifo 50.

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kutowachagua wagombea uongozi katika Uchaguzi ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi