loader
Picha

Amani na utulivu ni ngao yetu

WAISLAMU wa Tanzania jana waliungana na Waislamu wengine duniani kusherehekea sikukuu ya Idd el Hajj kwa amani, furaha na mshikamano uliojaa upendo na umoja wa aina yake.

Sisi tunapenda kuungana na viongozi wa serikali na dini waliotoa mawaidha na hotuba zilizosheheni umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika taifa letu kwa kuepuka dalili yoyote ile inayolenga kutokomeza amani na utulivu uliopo.

Hakuna ubishi kwamba bila amani na utulivu ni vigumu kwa nchi yoyote ile kukabiliana vilivyo na vita dhidi ya umasikini, maradhi na ujinga ili kujiletea maendeleo endelevu.

Kuonesha msisitizo juu ya jambo hili adhimu kulidumisha kwa ustawi wa Tanzania, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika Baraza la Idd Kitaifa lililofanyika Uwanja wa Msikate Tamaa, Vingunguti Dar es Salaam akawataka Watanzania kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani na kudumisha amani na upendo ili kuweza kuyafikia maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Ni ujumbe uliotawala ibada za Sikukuu ya Idd el Hajj katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuongeza nia ya dhati kwa Watanzania kuilinda tunu hiyo ya amani kwa nchi yetu na watu wake.

Kutokana na ukweli huo, sisi tunapenda kutoa mwito kwa wananchi wote wakiwemo viongozi wa dini, serikali, siasa na wale wa jamii kushikamana na kushirikiana kuwabaini na kutoa taarifa mapema katika vyombo vinavyohusika hususani polisi, yeyote anayethubutu kutuharibia amani yetu kwa kisingizio chochote kile.

Tunasema hivyo, kwa sababu sote tutakuwa na uhakika wa kuwa salama iwapo wakorofi wanaokusudia kutuharibia amani na utulivu wetu wakishughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli inapambana kuwakomboa watu wake kutoka katika lindi la umasikini kwa kutumia vizuri rasilimali zake yakiwemo madini, maliasili, kukuza kilimo na sera ya ujenzi wa viwanda itakwama iwapo amani na utulivu utavurugwa.

Tunaamini kwamba kutokana na tunu hii ya amani miradi mikubwa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa uzalishaji umeme wa Stiegler's Gorge, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi mkoani Tanga nchini Tanzania na mingineyo, itakamilika kwa wakati.

Hatua hiyo bila shaka ni nguzo muhimu kwa kutoa ajira kwa vijana wetu na kuimarisha uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla wake. Tuilinde amani yetu kwa nguvu zote.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi