loader
Picha

Daraja Tazara litunzwe lichangie uchumi

DARAJA la juu la magari katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara, linaelekea kukamilika likiweka historia ya kuwa la kwanza nchini.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Patrick Mfugale, kazi ya ujenzi wa daraja hilo zimekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na liko mbioni kukamilika.

Tunaipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kujenga daraja hilo muhimu kupunguza foleni za magari hasa yanayotoka bandarini Kurasini na pia yanayotoka na kwenda Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Kukamilika kwake siyo tu kutaifanya Tanzania iingie katika orodha ya nchi zenye madaraja kama hilo duniani, bali kutasaidia kuchagiza maendeleo ya uchumi kwa kuongeza kasi na idadi ya magari yanayopita barabara hizo mbili.

Tafsiri ya kuongezeka kwa kasi hiyo ni kuwa watu wanaopita katika njia hizo watakuwa na muda na fursa zaidi ya kushiriki shughuli za uchumi kwa haraka na kwa muda mrefu zaidi.

Na hiyo maana yake ni kuwa, wataweza kutoa mchango mkubwa zaidi katika uzalishaji mali na hivyo kukuza pato la Taifa na uchumi wetu.

Ndio maana tunaipongeza serikali na wahisani, Japan waliofadhili ujenzi huo na kuomba wananchi wote kuunga mkono hatua hiyo kwa kulitumia vyema daraja hilo kukuza uchumi.

Wananchi wanapaswa kuunga mkono hatua hiyo ya serikali na wafadhili kujenga daraja hilo kwa kuongeza jitihada katika uzalishaji maji na hivyo kukuza uchumi wa nchi ili ijitegemee.

Mbali ya kuongeza uzalishaji, ni matarajio yetu kuwa, watu wote watakuwa walinzi wa daraja hili ili liweze kudumu na kuwa lenye manufaa.

Wafanye hivyo wakijua kuwa daraja hilo na pia miundombinu mingine inayojengwa na serikali kwa fedha zake au hata za wafadhili na wahisani inagharimu mamilioni ya shilingi hivyo ilindwe.

Wahenga walisema kitunze kidumu. Ni vizuri kila mwananchi akawa mlinzi wa daraja hilo leo na siku zijazo lengo la kujengwa kwake litimie na kuifanya Serikali iendelee kujenga mengine.

Ni matarajio yetu kufunguliwa kwa daraja hilo itakuwa mwanzo wa mengine mengi kujengwa nchini katika maeneo mbalimbali hivyo watu wote walipokee kwa kulitunza, lidumu liwafae.

Kwa maeneo mengine yanayoendelea kujengwa madaraja kama hilo kama Ubungo makutano ya barabara ya Mandela na Morogoro, tunasema waendelee kutoa ushirikiano mkubwa Tanroads na kwa kampuni inayojenga daraja hilo kubwa.

Wananchi wafanye hivyo wakijua wazi ujenzi huo unalenga kuwanufaisha wao na vizazi vyao kwa shughuli za kiuchumi wanazofanya hivyo mchango wao ni muhimu kufanikisha ujenzi.

Kwa mara nyingine, tunawashukuru wananchi walioathiriwa na ujenzi wa daraja la Tazara kwa uvumilivu mkubwa uliowezesha lijengwe.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi