loader
Picha

Mpasuko Kamati ya Bunge ya Bajeti

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia na Makamu wake, Jitu Soni wamejiuzulu nyadhifa zao jana, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amethibitisha. Aidha, wajumbe wa kamati hiyo walikutana saa 11 jioni kwa ajili ya kuchagua viongozi wengine wa kushika nyadhifa hizo. Mwenyekiti mpya aliyechaguliwa ni George Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe mkoani Dodoma na Makamu wake ni Mashimba Ndaki, ambaye ni Mbunge wa Maswa Magharibi mkoani Simiyu.

Taarifa za kujiuzulu kwa viongozi hao zilianza kuenea jana mchana kwenye viwanja vya Bunge, ingawa wahusika hawakuwa tayari kulizungumzia hilo. Habari kutoka ndani ya Kamati ya Bajeti, zilibainisha kuwa Hawa ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM) na Soni (Babati Vijijini), walitangaza uamuzi wao huo kwenye kikao cha kamati hiyo jana. Hata hivyo, sababu za viongozi hao wa juu wa Kamati ya Bunge ya Bajeti kujiuzulu, hazikuweza kupatikana hadi tunakwenda mitamboni. Pamoja na juhudi za wahusika kuzungumzia suala hilo zilikuwa ngumu baada ya Hawa kutopatikana kwa njia ya simu na alipoonekana kwenye viwanja vya Bunge, alisema hayuko tayari kuzungumzia suala hilo.

Kwa upande wa Soni, yeye alipopokea simu alisema kuwa yuko kwenye kikao, atafutwe baadaye na alipotafutwa alisema kuwa ameitwa kwenye vikao vya chama. Alipotafutwa Katibu wa Bunge, Kagaigai, alikiri kupewa taarifa za kujiuzulu kwa viongozi hao wawili, huku akisema hajui sababu kwa sababu hajapewa barua rasmi. “Ni kweli nimeambia mwenyekiti na makamu wamejiuzulu, lakini sababu za wao kujiuzulu sizijui maana mpaka sasa hakuna barua ambao nimeipokea,” alisema. Wajumbe wengine waliopo kwenye kamati hiyo ni David Silinde, Mbaraka Dau, Mendard Kigola, Maria Kangoye, Abdallah Bulembo, Ali Hassan Omar, Freeman Mbowe, Martha Umbulla, Makame Kassim Makame, Dk Dalaly Kafumu, Albert Ntabaliba.

Wengine ni Ibrahim Hassanali Raza, Oran Njeza, Riziki Lulida, Hasna Mwilima, Stephen Masele, Mashimba Ndaki, Prof.Anna Tibaijuka, Balozi Adadi Rajabu, Dk Immaculate Semesi, Shally Raymond, Andrew Chenge na Hussein Bashe. Akihojiwa baada ya kuchaguliwa, Simbachawene alisema anawashukuru wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bajeti kwa kumchagua kuwa mwenyekiti. Alisema kamati hiyo ni ngumu na mhimili mkubwa wa Bunge na Serikali, hivyo atajitahidi kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na kanuni kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa. Majukumu makuu ya Kamati ya Bunge ya Bajeti ni kupitia na kujadili mapendekezo ya bajeti za taasisi na wizara zote nchini, ikiwemo Bajeti Kuu na kutoa mapendekezo ya namna ya kutekeleza na kuboresha matumizi ya bajeti hizo.

TANZANIA na Uganda zimeanzisha rasmi Jukwaa la Biashara baina ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi