loader
Picha

Tanzania yaongoza unafuu bei ya mafuta EAC

TANZANIA ina bei nafuu zaidi ya mafuta, inayowawezesha watumiaji wake kupata mafuta ya petroli na dizeli kwa bei rahisi, ukilinganisha na nchi zingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ripoti inasema. Aidha, wataalamu wanasema kuwa sera za Tanzania kwenye uagizaji na usambazaji mafuta, zinawajali na kuwabeba wananchi kwa kuwa na tozo za kodi nafuu, gharama za usafirishaji nafuu na uagizaji ulio nafuu, tofauti na ilivyo kwa Kenya, ambayo hivi karibuni asilimia 16 iliongezwa kama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Kwa mujibu taarifa ya Septemba 3 mwaka huu, iliyotolewa na tovuti ya kimataifa ya Global Petrol Prices, Bei ya lita moja ya petroli Tanzania inauzwa kwa wastani wa dola 1.04 (sawa na Sh 2,377) wakati lita moja ya dizeli inauzwa dola moja (sawa na Sh 2,286). Profesa wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema kuwa kwa hali ya kawaida, bei za mafuta ziko juu kwenye nchi ambazo hazina bahari, ukilinganisha na zile ambazo zinapitiwa na bahari.

“Kwa hali ya kawaida Tanzania itakuwa na bei za chini za mafuta…lakini bei ya mafuta huchangiwa na mambo mbalimbali zikiwemo kodi na gharama za usafirishaji,” alisema. Nchi ya Uganda ni ya pili Afrika Mashariki kwa kuwa na bei ya chini ya petroli, ambapo lita moja inauzwa dola 1.09 (sawa na Sh 2,491.7) huku dizeli lita moja ikiuzwa dola moja (sawa na Sh 2,286). Mpaka juzi Jumanne, Uganda ilikuwa na bei ya dizeli inayolingana na ile ya Tanzania licha ya kuwa ni nchi ambayo haina bahari wakati Kenya ambayo ina sehemu kubwa kwenye Bahari ya Hindi, imekuwa moja ya nchi zenye bei kubwa za mafuta kwa siku za hivi karibuni.

Juzi Jumatano, tovuti hiyo ya kimataifa ilieleza bei ya petroli kwa lita nchini Kenya kuwa ilikuwa ni dola 1.15 (sawa na Sh 2,628.9) wakati dizeli ilikuwa ikiuzwa dola 1.04 (sawa na Sh 2,377). Rwanda pia ni nchi ya pili katika EAC yenye bei kubwa ya mafuta. Petroli lita moja nchini humo inauzwa dola 1.26 (sawa na Sh 2,880) wakati dizeli inauzwa kwa dola 1.24 (sawa na Sh 2,287). Burundi ndiyo nchi kwenye jumuiya hiyo yenye bei kubwa ya mafuta. Nchini Burundi bei wastani wa lita moja ya petroli ni 1.27 (Sawa na Sh 2,903) huku dizeli ikiuzwa kwa bei hiyo hiyo ya Sh 2,903. Profesa wa Uchumi kutoka Chuo cha Dar es Salaam (UDSM), Razack Lokina alisema kuwa bei ya mafuta kuwa Tanzania ukilinganisha na nchi zingine za Afrika Mashariki, inachangiwa na sera zinazosimamia kodi, uagizaji na usafirishaji.

Alisema, “Bei ya mafuta ya Tanzania na Kenya zinatofautiana kutokana na sera za nchi hizo, Kenya hivi karibuni wameongeza kodi ya mafuta mpaka asilimia 16, na kwa Tanzania haijaongeza hivyo wananchi wa Tanzania hawajakutana na kadhia hiyo. “ Unaweza kuwa kwenye ukanda wa bahari, lakini nchi ikawa ina bei kubwa ya mafuta kuliko zile nchi ambazo hazina bahari…Hii inatokana na sera za nchi, ndiyo maana leo hii bei ya mafuta nchini Uganda inaonekana kidogo kuliko Kenya licha ya kuwa Kenya ina bandari kwenye Bahari ya Hindi. “Mfano Tanzania ina mfumo mmoja mzuri sana ambao unaitwa ‘Bulk Procurement’ huu ni ununuzi mzuri wa mafuta ambao muagizaji anakuwa mmoja na anatozwa fedha ndogo kwenye manunuzi ya kiwango kikubwa cha mafuta”. Profesa Lokina alisema kuwa bei za mafuta zinategemeana na jinsi nchi zinavyosimamia sera na kutoweka kodi kubwa kwa mafuta.

KUPANDISHWA KODI YA MAFUTA KENYA

Wakati, sera zikitajwa kuchangia kupanda au kushuka kwa bei ya mafuta, Serikali ya Kenya imeongeza kodi ya mafuta mpaka kufikia asilimia 16, huku ongezeko hilo lilielezwa kuwa huenda likahatarisha uchumi wa Afrika Mashariki. Mchumi Dk Hildebrand Shayo alisema kuwa kupanda kwa bei ya mafuta nchini Kenya, huenda ikaleta madhara ya muda mfupi kwenye uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Dk Shayo ambaye anafanya shughuli zake jijini Dar es Salaam, alisema, “Tutegemee mabadiliko ya baadhi ya bidhaa kwa siku zijazo kwa sababu Kenya ndiyo yenye uchumi mkubwa kwenye EAC kwa muda mrefu.”

Alisema uwepo wa bei nafuu ya mafuta Tanzania, ukilinganisha na nchi zingine za EAC, haitakuwa na madhara ya muda mfupi, isipokuwa madhara yake kwenye bei ya bidhaa ni ya muda mrefu. “Bei kubwa za mafuta, huongeza gharama za uzalishaji na biashara kwa ujumla, kama Kenya wataangalia suala la kodi na kuliona linawaumiza, wanaweza kuhamishia uzalishaji wa bidhaa zao nchini Tanzania ili kuzipunguzia kampuni zao gharama,” alisema. Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo alisema kuwa unafuu wa bei ya mafuta uliopo Tanzania, unaotofautiana na nchi zingine wanachama wa EAC, unaonesha wazi kuwa inatokana na mfumo ulio nafuu wa ununuzi wa kiwango kikubwa cha mafuta kwa wakati mmoja.

“Kuna mfumo unaotumika kwenye uagizaji wa mafuta mengi kwa wakati mmoja, yaani ‘Transparent Bulk Procurement System (BPS)’. Mfumo huo unasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kadhalika,” alisema na kuongeza kuwa mfumo huo umesaidia kupunguza usumbufu.

BEI ZA MAFUTA ZA MATAIFA YOTE DUNIANI ZINAPATIKANAJE?

Kwa mujibu wa tovuti hiyo ya kimataifa, bei za mafuta kote duniani inachangiwa na kodi za nchi husika na sera za utozaji na kwamba nchi zote zina uwezo wa kujua na kuweka bei ya mafuta kwenye soko la dunia na kuzipangia bei kulingana na matakwa yao.

BEI ZA MAFUTA ZA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI NCHI BEI PETROLI BEI DIZELI

Tanzania Sh 2,377 Sh 2,286

Uganda Sh 2,491.7 Sh 2,286

Kenya Sh 2,628.9 Sh 2,377

Rwanda Sh 2,880 Sh 2,287

Burundi Sh 2,903 Sh 2,903.2

NCHI ZA AFRIKA ZENYE BEI NAFUU ZAIDI ZA MAFUTA NCHI BEI PETROLI BEI DIZELI

Sudan Sh 777.2 Sh 525.7

Algeria Sh 800.1 Sh 434.3

Nigeria Sh 937.2 Sh 1,303

Misri Sh 982.9 Sh 708.6

Angola Sh 1,303 Sh 1,097.2

BEI RAHISI ZAIDI ZA MAFUTA NCHI ZA DUNIANI NCHI BEI PETROLI BEI DIZELI

Venezuela Sh 22.8 Sh 11.4

Iran Sh 662.9 Sh 160

Sudan Sh 777.2 Sh 525.7

Kuwait Sh 800.1 Sh 868.6

Algeria Sh 800.1 Sh 434.3

WASTANI WA BEI YA PETROLI DUNIANI

Dola 1.16 (sawa na Sh 2,651.7) kwa lita

WASTANI WA BEI YA DIZELI DUNIANI

Dola 1.06 (sawa na Sh 2,423.1) kwa lita BEI ya dola moja ya Marekani kwa shilingi ya Tanzania ni Sh 2,286 (CHANZO: BoT- 05/09/2018).

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi