loader
Picha

Waziri Mpina na juhudi kuepusha samaki wasitoweke

RAIS John Magufuli amekamilisha ziara ya kikazi takribani siku kumi tangu Septemba 3, 2018 katika Ukanda wa Ziwa Victoria iliyohusisha mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na Simiyu. Kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, Rais Magufuli anawataka wanasiasa wa vyama vyote waunge mkono juhudi za serikali kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria ili nchi ifaidi rasilimali za uvuvi na kujenga uchumi kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Kimsingi, Tanzania inaongoza kwa kumiliki asilimia 51 ya ziwa lote katika nchi za Afrika Mashariki wakati Uganda inamiliki asilimia 43. Kenya inamiliki asilimia 6 pekee, lakini katika kipindi fulani mapato ya yatokanayo samaki na mazao yake kwa Kenya, yamekuwa sawa na Tanzania kutokana na usimamizi dhaifu uliokuwapo katika sekta hii nchini.

Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na wizara yake kwa jitihada kubwa kupambana na uvuvi haramu kupitia operesheni maalumu aliyoianzisha kudhibiti uvuvi haramu katika ziwa hilo ijulikanayo kama ‘Operesheni Sangara 2018 .’ Katika pongezi zake, Rais anataka operesheni hiyo iendelee ili kukomesha uvuvi haramu unaotishia kumaliza samaki. Kimsingi, baadhi ya aina za samaki kama gogogo, furu na kamongo zimepotea.

Katika hotuba zake, Rais anasema: “… “Luhaga Mpina; chapa kazi waache wanaolaumu hilo walaumu leo, lakini kesho ndio watafurahi.” Anawataka wanaomlaumu Waziri Mpina kuacha kufanya hivyo na badala yake, wamlaumu yeye (Rais kama kuna mantiki) kwa kuwa ndiye aliyemteua kufanya kazi hiyo anayosema anaifanya vizuri na kwa kuzingatia Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya Mwaka 2003. Rais anasema analolifanya Waziri Mpina kupitia Operesheni Sangara 2018, limeibua mafanikio makubwa kwani samaki wameanza kuongezeka na samaki wakubwa wameanza kuonekana.

Kutokana na matunda hayo na mengine, Rais anasema serikali itajenga kiwanda kikubwa cha kuchakata samaki katika mji wa Nansio wilayani Ukerewe ili wavuvi wapate soko la uhakika la kuuza samaki kutoka katika Z iwa V ictoria. Anasema katika vita ya kupambana na uvuvi haramu, Serikali itafanya kazi hiyo bila kubagua mtu, cheo au chama cha siasa ili kunusuru hazina ya nchi. Ndiyo maana Rais anasema: “Hata akivua Waziri Mpina yeye mwenyewe tutamshika, tunataka Tanzania yenye mwelekeo mzuri wa kufuata Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya 2003.

Ukitaka kutibu jipu lazima zitoke damu. Nchi hii ni yetu lazima tuijenge sisi wenyewe kwa manufaa yetu.” Kwa mujibu wa Mkuu wa Nchi, nchi nyingi duniani zinaendesha uchumi wake kwa kutegemea sekta ya uvuvi. Anatoa mfano wa Namibia anayosema asilimia 35 ya uchumi wake unatokana na mapato katika sekta ya uvuvi. Rais anaweka bayana kuwa, Serikali imejipanga kukomesha hujuma katika kazi hiyo kama ilivyokuwa awali Tanzania ilifanikiwa kukamata meli iliyokuwa ikivua samaki aina ya Jodari bila kufuata sheria katika Ukanda wa Bahari Kuu.

Anasema meli hiyo ilizamishwa makusudi ili kukosesha ushahidi mahakamani. “Juhudi za kupambana na uvuvi haramu,” Rais Magufuli anasema zinapaswa kuungwa mkono na kila mwananchi vinginevyo, utafika wakati Z iwa V ictoria likakosa samaki. Anasema vizazi vilivyotangulia wangefanya kosa hilo, kizazi cha sasa kisingefaidi samaki hawa. Kwa msingi huo, anasema serikali haitakubali kuendelea kumaliza rasilimali za samaki kama ambavyo imeandelea kumaliza viwanda vya kuchakata samaki. Waziri Mpina anamshukuru Rais na kuahidi kuendelea kusimamia sheria na maelekezo yote yanayotolewa.

Anasisitiza kuwa, Operesheni Sangara 2018 itakuwa endelevu na itasambaa katika maziwa yote, bahari, mito mikubwa na mabwawa ili kuhakikisha sekta ya uvuvi inachangia kikamilifu katika uchumi wa nchi yetu. Tanzania ina ukubwa wa eneo la km za mraba 945,040. Kati ya hizo, kilometa za mraba, km 346,337 (sawa na asilimia 36.7) ni maji. Waziri anasema uwekezaji katika viwanda vya kuchakata samaki nchini, ulianza mwaka 1992 na vikaanzishwa viwanda 13, lakini kutokana na sababu mbalimbali viwanda vimekuwa vikipungua na kubaki vinane vinavyofanya kazi huku uzalishaji ukiwa umeshuka hadi tani 171 kwa siku; sawa na asilimia 16 ya uwezo wa viwanda.

Kimsingi inaelezwa kuwa, kupungua kwa viwanda vya samaki kumejitokeza pia katika nchi za Kenya na Uganda. Nchini Kenya kuna viwanda 2 vinavyofanya kazi kati ya viwanda 9 vilivyokuwepo, huku Uganda ikiwa na viwanda 7 vinafanya kazi, kati ya 18. Nchini Tanzania, viwanda 13 vilivyokuwepo vilikuwa vimesimika mitambo yenye uwezo wa kuzalisha tani 1,065 kwa siku na kutoa ajira 4,08 8 . Aidha, V iwanda 8 vinavyofanya kazi vimeajiri jumla ya wafanyakazi 2,179. Kuhusu biashara ya mabondo, Waziri Mpina anasema, biashara ya mabondo ilianza sambamba na uzalishaji wa samaki katika miaka ya 1990 ambapo viwanda vilisafirisha mabondo yaliyogandishwa kwenda nchi za Bara la Asia.

Baada ya mahitaji ya mabondo kuongezeka miaka ya 2000, wafanyabiashara kutoka Asia walianza kuja nchini na kujishughulisha na ukusanyaji wa mabondo, kuyakausha na kuyapeleka katika masoko ya China na Hong Kong. Katika Z iwa V ictoria vilibainika kuwepo viwanda 22 vya kuchakata mabondo. V iwanda 6 pekee ndivyo vilivyopewa vibali. Hadi sasa viwanda 9 vya kuchakata mabondo vina vibali (mwaka 2017/ 18 ) na viwanda 13 vimefungiwa.

Anasema takwimu za mavuno ya sangara katika Z iwa V ictoria zinaonesha kuwa miongoni mwa sangara waliokidhi kuvuliwa (wenye urefu wa sm 50 hadi 85) yalishuka kutoka asilimia 19.9 mwaka 2005 hadi asilimia 6.1 mwaka 2015. Wavuvi wa sangara kwa sasa wanalenga samaki walio chini ya sm 50 na juu ya sm 85 kinyume cha wanaoruhusiwa kuvuliwa kisheria (sm 50 hadi 85). Urefu huo wa sangara unaoruhusiwa kisheria unaendana na ukubwa wa mabondo ya urefu wa sm 17-30 kulingana na utafiti uliofanyika mwaka 2015.

Waziri anasema utafiti wa mwaka 2017 unaonesha kwamba, asilimia 96.6 ya sangara wote ziwani Tanzania, hawazidi sentimita 50 na walio kati ya sentimita 50 hadi 85 ni asilimia 3.0, sawa na tani 20,163. Sangara wanaozidi sentimita 85 ni tani 2,372 sawa na asilimia 0.4 na wanaongezeka kwa asilimia 14 kwa mwaka. Kisheria, samaki aina ya sangara wanaopaswa kuvuliwa ni walio kati ya sentimita 50 mpaka 85. Hii inamaanisha kuwa, sangara chini ya sentimeta 50 ni wachanga.

Aidha, samaki zaidi ya sentimeta 8 5 ni wazazi hivyo hawapaswi kuvunwa ili waendeleze rasilimali hiyo. Hata hivyo, kuwepo kwa asilimia kubwa ya sangara wachanga kunaweza kuongeza uzalishaji wa samaki endapo wataachwa wakue kwa kudhibiti uvuvi haramu. Mpina anataja matokeo ya Operesheni Sangara kuwa ni pamoja na kupungua kwa uvuvi haramu katika Z iwa V ictoria kwa takribani asilimia 60 ukilinganisha na hali ilivyokuwa kabla ya Operesheni Sangara 2018.

Matokeo mengine ni kuongezeka kwa ukubwa na wingi wa samaki wanaochakatwa viwandani badala ya samaki wachanga na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa utoroshaji rasilimali za uvuvi kwenda nje ya nchi. Mengine ni kuongezeka kwa uelewa kuhusu athari za uvuvi na biashara haramu miongoni wa wadau, kuongezeka kwa mapato yatokanayo na biashara ya samaki katika masoko. Kwa mfano, katika Soko la Kirumba Mwaloni, mapato kwa mwezi yameongezeka kutoka Sh milioni 30 mpaka milioni 190 kwa mwezi.

Biashara ya samaki wachanga kwenye masoko imepungua, kuondoa wageni waliokuwa wanavua kwenye maji yetu; na Tanzania kuendesha operesheni ya kudhibiti uvuvi haramu pasipo kutumia nguvu kubwa ukilinganisha na nchi nyingine za Afika Mashariki. Katibu Mkuu wa Uvuvi, D k Rashid Tamatama anasema Tanzania, Kenya, na Uganda zimeamua kwa pamoja kufanya Operesheni Okoa Sangara (Operation Save the Nile Perch - OSNP) tangu mwaka 2009 katika Z iwa V ictoria.

Gharama ya Operesheni hiyo iliamuliwa kutoka katika michango ya nchi wanachama. Kila nchi ilitakiwa kuchangia D ola za Marekani 600,000. Fedha hizi mwanzo zilipangiwa kufanya Sensa ya Uvuvi na usajili wa vyombo vya uvuvi. D k Tamatama anasema Waziri Mpina kama Mwenyekiti aliyemaliza muda wake katika kikao cha kwanza cha Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi kilichofanyika E ntebe, Uganda Machi 2, 2018 anapendekeza fedha hiyo itumike kufanya OSNP katika Z iwa V ictoria.

Mawaziri wote wanaosimamia sekta ya uvuvi wa Tanzania, Kenya na Uganda walisaini makubaliano hayo. Katika utekelezaji wa makubaliano hayo, kikao cha kikanda cha wataalamu kimefanyika mwanzoni Agosti 2018 na kupanga kazi na bajeti ya kutekeleza OSNP katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda. Bajeti hiyo imewasilishwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata idhini ya matumizi ya fedha. John Mapepele ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Anapatikana kwa 0784441180

ROSEMARY Dickson ni miongoni mwa wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi ...

foto
Mwandishi: John Mapepele

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi