loader
Picha

Agizo la JPM utengenezaji kivuko kingine muafaka

AGIZO la Rais John Magufuli la kumtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kutangaza zabuni ya kivuko kipya kitachokuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200, kwa ajili ya kutoa huduma katika visiwa vya Ukara na Bugorora wilayani Ukerewe, Mwanza, limekuja katika wakati muafaka.

Tunasema limekuja wakati muafaka kwa kuwa tayari wananchi hao baada ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere, sasa hawana usafiri wa uhakika, kwani vivuko vinavyotumika sasa zitatumika kwa muda tu ili kusaidia kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka visiwa hivyo.

Maagizo ya Rais ambayo yametaka zabuni hiyo kuelekeza wazi kivuko kibebe watu 200 na mizigo tani 50 yanaonesha wazi jinsi serikali inavyojali watu wake.

Tunaamini kwa kutengenezwa kwa kivuko hicho na kusukwa upya kwa kivuko cha Mv Nyerere baada ya kuibuliwa, kitasaidia kupunguza tatizo la usafiri katika visiwa hivyo, jambp ambalo limekuwa likizungumzwa kila mara.

Kwa kuwa kivuko hicho kilichoagizwa kitakuwa na uwezo mara mbili ya kile cha mwanzo na kikija kuunganishwa na hicho kinachoibuliwa hali ya usafiri katika visiwa hivyo tunaamini itatengamaa.

Tunaamini kazi inayofanywa na serikali yetu chini ya usimamizi madhubuti wa Rais Magufuli kuangalia kilichosibu kivuko hicho na kisha kukipa uhai mpya wa kuendelea na kazi itafanyika kwa kasi kubwa ili kupunguza maumivu kwa wananchi.

Pamoja na maumivu ya sasa ya kupoteza ndugu, kwa kuwa maisha lazima yaendelee na kutegemeana kwa visiwa katika huduma, juhudi zinazofanywa za kurejesha hima usafiri katika maeneo hayo ni furaha ya kila mmoja.

Pasi shaka, kauli ya Rais Magufuli ya kuitishwa kwa zabuni ya haraka kutengeneza kivuko kikubwa kitakachokuwa mbadala wa kivuko cha Mv Nyerere kwa kubeba abiria zaidi ya 200 ikiambatana na kuongeza muda wa safari hadi usiku kwa lengo la kupunguza msongamano wa abiria, kutafanya ajali katika Ziwa Victoria kuwa historia.

Tunasema itakuwa historia kwa kuwa kutakuwa na nafasi pana ya watu kutekeleza majukumu yao kwa uhakika bila ya kubeba shaka za maisha katika safari.

Kwa kuwa serikali ya awamu ya tano ni ya vitendo tunaamini kabisa baada ya miezi mitano au sita, kivuko kipya kitakuwa kimekamilika na visiwa vingi vitakuwa na ahueni, hasa kwa kutambua kwamba tayari tathmini imeshafanyika katika mialo ambayo inaweza kutumika kushusha abiria.

Pamoja na utengenezaji wa kivuko kipyao ambao tunaamini utakwenda sanjari na ukarabati mkubwa wa kivuko kilichozama baada ya kuibuliwa, watumishi wa mitambo hiyo ya usafiri wanatakiwa kujifunza namna bora zaidi ya kuweka usalama kabla ndani ya vyombo husika.

Wakati tunasubiri ripoti ya nini hasa kilisibu kivuko cha Mv Nyerere, ni dhahiri mwenendo wa kupakia abiria ulikuwa na shaka katika safari zote hivyo ni vyema kuanza kujitathmini katika utoaji wa huduma nzuri kwa usalama zaidi.

Kwa kuwa tayari tuna kampuni hapa nyumbani yenye uwezo wa kujenga meli nzuri na madhubuti, tunaamini wataomba zabuni hizo kuonesha umahiri na pia kuzidi kuimarisha ujuzi katika nyanja ya utengenezaji wa meli nchini.

Tunapowatakia heri wanajeshi wetu kukamilisha kazi ya kuibua kivuko hicho mapema zaidi, tunaomba wananchi wenye utaalamu katika mambo ya usafiri wa maji kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuwa salama katika maji yanayotuzunguka. Mungu Ibariki Tanzania.

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka maarufu mabasi ya mwendokasi, umekuwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi