loader
Picha

Tupime afya kupunguza tiba isiyo ya lazima

WATANZANIA juzi waliungana na wenzao nchi nyingine kuadhimisha Siku ya Moyo duniani.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Ijumaa, Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam ilipima wanahabari kubaini wenye matatizo na kuwapa tiba na ushauri.

Juzi, JKCI iliendesha kliniki ya wazi Kigamboni kwa wananchi bure huku madaktari wenzao wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma pia wakiadhimisha siku hiyo kwa kuhudumia watu.

Tunazipongeza JKCI na Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kujitolea kuadhimisha Siku ya Moyo kusaidia wananchi kujua hali za afya zao.

Kwa kufanya hivyo, hospitali hizo zimeonesha kweli ni za umma zinazojali maisha ya waajiri wao, wananchi na hivyo kustahili kupongezwa.

Ni kweli hospitali zimeanzishwa kwa lengo la kutoa huduma ya afya kwa wananchi wagonjwa lakini utaratibu wa kutoa huduma za ziada ni ubunifu unaostahili kupongezwa kwani ni fursa.

Ni fursa kwa sababu unawezesha wananchi na hasa wagonjwa wasio na uwezo wa kifedha na bima, muda wa kwenda hospitali kukagua afya zao au wako mbali, kunufaika na huduma hizo.

Ndio maana tunawiwa kuwapongeza watendaji wa hospitali hizo na nyingine zenye utaratibu kama wao kuwakumbuka wananchi wanyonge.

Kwa kuwafuata wananchi waliko, taasisi hizo zimeweza kuwahamasisha watu wengi zaidi kupima na kujua afya zao na hivyo kuwaokoa.

Haitoshi tu hopistali yenye majengo na vifaa na wataalam wazuri kama hizo mbili kujifungia ndani na kusubiri tu wagonjwa ndio wawafuate.

Kwa kutoka na kwenda maeneo ya nje waliko watu, watendaji wa hospitali hizo wamejifunza mambo mengi ikiwemo ukweli kuwa, tatizo la moyo ni kubwa kuliko inavyoweza kufikiriwa.

Kwa mfano, takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO) zinaonesha watu milioni 17.5 wanakufa kila mwaka kutokana na matatizo ya moyo. Inaelezwa takwimu zinaonesha watoto 136,000 huzaliwa wakiwa na magonjwa ya moyo kila mwaka na kati yao, 3,400 wanahitaji upasuaji.

Ni kufuatia ukweli huo tunaungana na taasisi hizo kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa za kupima afya yao kujua maradhi mbalimbali yanayowakabili na kuyaepuka au kutumia dawa.

WHO inasema watu wapatao milioni 38 duniani wanakufa kila mwaka kwa magonjwa ya kuambukiza yakiwemo ya moyo na mengine.

Cha kushangaza ni kuwa, kati ya wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo ni watu wenye uwezo mkubwa wakimiliki magari wanayokatia bima na kuyakagua kama mazima lakini hawajali kukatia bima maisha yao wala kupima afya zao.

Ni matumaini yetu baada ya maadhimisho ya Siku ya Moyo, wananchi wengi zaidi watakuwa wamehamasika kupima afya zao hospitalini.

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka maarufu mabasi ya mwendokasi, umekuwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi