loader
Picha

Taasisi zizingatie sheria za manunuzi

WAZIRI wa Fedha, Dk Philip Mpango ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza kuwepo kwa viashiria vikubwa vya rushwa kwenye taasisi 13, na miradi 93 iliyotekelezwa kwa fedha za umma.

Ametoa maagizo hayo juzi Dar es Salaam wakati akipokea tathmini ya utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Tumeguswa na maagizo ya Waziri Mpango na matokeo ya tathmini iliyofanywa na PPRA na tunaungana nao kuitaka Takukuru ichunguze na kuwachukulia hatua watakaobainika kukosea.

Kubainika kwa viashiria hivyo katika hatua za awali na utekelezaji wa mikataba wa taasisi hizo 13 siyo tu unaitia doa serikali ya awamu ya tano inayopiga vita rushwa, ubadhirifu na wizi, bali inaonesha kuna watu hawajui wajibu wao.

Katika hali ya kawaida tulitarajia kuwa taasisi 13 zilizotajwa na PPRA zina wataalamu wa fani ya manunuzi wanaojua sheria na taratibu zake na wajibu wao katika kuwahudumia wananchi.

Ndio maana tunashangazwa na kusikitishwa na habari kuwa taasisi hizo zinaongoza kwa viashiria vya rushwa katika zabuni zao na kuashiria matatizo kwa menejimenti na watumishi wa taasisi hizo.

Tukiwa chombo cha umma kinachohamasisha utendaji uliotukuka unaotakiwa na Rais John Magufuli na viongozi wenzake wa juu nchini tunasema, hatukubaliani na viashiria na hata vitendo halisi vya rushwa, wizi au ubadhirifu.

Hatubaliani navyo kwa sababu kufanyika kwake ni chanzo cha kuzorota au kutofanyika kabisa kwa miradi ya serikali kutokana na kukosa watu wazuri wa kuitekeleza kutokana na waliopewa kwa rushwa kukosa sifa ya kazi au kufanya chini ya kiwango kufuatia kuishiwa fedha za kuifanya.

Ni matarajio yetu kuwa taasisi hizi 13 ambazo zimebainika zitachunguzwa kwa kina ili zile zenye matatizo makubwa ziwajibishwe kwa mujibu wa sheria za PPRA na zile za nchi. Kwa taasisi ambazo hazijaguswa na tathmini hiyo, ni vyema zikaichukulia kama fundisho la kuendelea kusimamia vyema maadili na sheria za manunuzi na utekelezaji wa miradi yao yote.

Kinyume cha hayo, ni kuzikaribisha PPRA na Takukuru kuwachunguza na watakapobainika, kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Hatutarajii kuna watendaji wanaoomba hayo yawakute. Badala yake, tunaomba kila mtaalamu wa fani ya ugavi kusimamia sheria na taratibu za utoaji zabuni kuanzia hatua ya awali hadi utekelezaji bila kuacha shaka ya kuhisiwa kutotenda haki.

Tunaamini wataalamu wengi wa ugavi nchini wamesomeshwa vizuri na wanamudu kazi zao, hivyo itakuwa rahisi kuachana na vishawishi vya rushwa ili watende haki kwao na wateja pia.

Wakifanya hivyo, wataitendea haki taaluma yao na kuipa heshima lakini pia kuziepusha taasisi zao na kashfa kama iliyozipata hizi taasisi 13.

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka maarufu mabasi ya mwendokasi, umekuwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi