loader
Picha

Viwanda vyapunguza changamoto za ajira

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema changamoto ya upatikanaji wa ajira hususani kwa vijana imeanza kupungua nchini baada ya viwanda vingi kuanza kufanya kazi.

Aliyasema hayo juzi jioni alipotembelea kiwanda cha kukoboa kahawa cha BUKOP na cha kusindika kahawa cha Tanica, mjini Bukoba.

Alisema kwa sasa tabia ya vijana wengi kukaa vijiweni imepungua kwenye maeneo mengi nchini baada ya wengi kuajiriwa katika viwanda mbalimbali vilivyoanzishwa na kufufuliwa.

Waziri Mkuu alisema viwanda vimekuwa vikitoa ajira nyingi kwa wananchi, ambapo alitolea mfano kiwanda kimoja cha Tanica kilichoajiri watumishi 800.

"Nyie mlioajiriwa kiwandani hapa hakikisheni mnafanya kazi kwa bidii, weledi, uaminifu na uadilifu wa hali ya juu ili kukiwezesha kiwanda kuendelea na uzalishaji," alisisitiza.

Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku nne, inayolenga kufuatilia maendeleo ya viwanda na zao la kahawa, ambalo ni kati ya mazao makuu sita ya biashara.

Awali, Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Linus Leopord alisema kwa mwaka wanazalisha tani 600 za kahawa iliyokaangwa na kusagwa, ambayo inatosheleza mahitaji ya soko.

Pia kiwanda cha kahawa cha Tanica kina uwezo wa kuzalisha kahawa ya unga tani 500 kwa mwaka ila kutokana na uchakavu wa miundombinu kinazalisha tani 300 kwa mwaka.

Kuhusu masoko, Leopord alisema kwa sasa mauzo yameongezeka, wanauza tani 50 ya kahawa iliyokaangwa na kusagwa kwa mwezi, ambapo awali walikuwa wanauza tani 32.

Kadhalika, meneja huyo alisema wameimarisha na kuongeza soko la nje ambapo kwa sasa wanauza tani 35 za kahawa ya unga kwa mwezi, awali walikuwa wanauza tani 20.

Alisema kiwanda cha Tanica kinamilikiwa na Chama cha ushirika cha KCU kwa silimia 53.37, KDCU asilimia 31.8 , Hazina asilimia (7.67, TFC asilimia 6.22 na wafanyakazi wa Tanica asilimia 0.92.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Bernard Limbe kuhakikisha anatafuta eneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo.

Aliyasema hayo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi waliokuwa wakifanya biashara katika eneo bandari kuondolewa bila ya kupewa eneo lingine.

Waziri Mkuu alisema ni marufuku kuwaondoa wananchi katika maeneo yao ya kufanyia biashara bila ya kuwaonesha eneo jingine ambalo watalitumia kwa biashara zao.

WAKUU wa Mikoa ya Tabora na Geita, wamesema Jukwaa la ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Bukoba

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi