loader
Picha

Misemo ya Kiswahili- 1

LEO katika mfululizo wa safu ya Kiswahili kwa wageni tunatupia macho katika matumizi ya Misemo ya Kiswahii, lengo likiwa ni kuwawezesha wageni kuwa na uwezo wa kutumia misemo hiyo kikamilifu.

Misemo ni kauli fupifupi ambazo hutumiwa na jamii kusisitiza ukweli wa jambo fulani. Kauli hizi huunganisha mawazo au dhana tofauti kuwa mwili mmoja na kupitisha ujumbe uliokusudiwa na mnenaji au mwandishi.

Pia, misemo ni fungu la maneno ambalo hutumiwa na jamii tofauti kwa lengo la kusisitiza maadili fulani. Kwa mfano tukisema, ‘mtu amegonga mwamba’ hatumaanishi kwamba amepiga jiwe kubwa kwa kifaa chochote au kwa mkono, bali tunamaanisha kwamba ameshindwa kuendelea katika jambo fulani.

Ifuatayo ni misemo ya Kiswahili na maana yake.

Kupata jiko

Huu msemo haumaanishi kununua au kuazima jiko la kupikia. Una maana ya kupata mke au kuoa. Kwa hivyo, mtu anaposema nimepata jiko anamaanisha kuwa ameoa.

Kuangusha uso

Maana ya huu msemo ni kuona aibu au soni mbele ya watu kwa jambo baya ulilolitenda. Mfano wa matumizi ni kama: ukitenda mema hapatatokea haja ya kujishusha hadhi kwa kuangusha uso kila wakati.

Enda msobesobe

Maana kamili ya msemo huu ni kuenda pasipo na utaratibu wowote. Pia huweza kumaanisha kuenda pasipo na hiyari. Mfano katika sentensi: Alipougua malaria alikuwa akienda msobesobe.

Enda mvange

Kabla ya kutoa maana ya msemo huu, ni vizuri uelewe kuwa maana ya neno ‘mvange’ ni ‘kombo’. Kwa hivyo msemo huu unaweza kuwa ‘enda kombo,’ na maana yake mambo kufanyika kwa namna isiyotarajiwa. Kwa mfano, namshukuru Mola kwa sababu biashara yangu haikwenda mvange.

Chokoza nyuki mzingani

Mzinga ni nyumba ya nyuki. Msemo huu unamaanisha kwenda palipo na hatari na kujaribu kuichokoza au kuikabili kijinga hatari hiyo. Mfano katika sentensi: kung’oa Simba usinga wake wa shingoni ni mfano wa kumchokoza nyuki mzingani.

Bwaga wimbo

Maana yake ni kuanzisha au kuongoza wimbo. Msemo huu huwezeka kutumika katika sentensi kama ifuatayo; mahadhi ya aliyeubwaga wimbo yalikuwa mazuri.

Anua jamvi

Maana ya msemo huu ni kutamatisha jambo au shughuli fulani uliyoanzisha. Pia kukunja jamvi ina maana sawa na kuanua jamvi. Kwa mfano, baada ya wanariadha kuanua majamvi yao, walirejea nchini.

Choma mkuki

Maana ya msemo huu ni ‘kufuma’ au ‘shambulia’ kwa kutumia mkuki. Kwa mfano, siku hizi vituko ni vingi, aghalabu watoto wanawachoma mikuki wenzao kwa utesi wa mashamba.

Fanya ndaro

Neno ndaro linamaanisha sifa au sifu. Msemo huu unamaanisha kujisifu kwa jinsi mtu anavyozumgumza. Kwa mfano, ni vizuri uyaeleze yote uliyoyapitia bila ya kujifanyia ndaro na kumbe hamna lolote.

Fanya speksheni

Speksheni ni neno ambalo lina maana sawa na ukaguzi. Hivyo basi, msemo huu unamaanisha fanya ukaguzi au kagua. Kwa mfano, mkubwa wa kituo cha polisi hufanya speksheni ya nyumba zote za polisi kila Jumapili.

Fanya udhia

Msemo huu unamaanisha kufanya usumbufu. Kwa mfano, hakudhamiria kufanya udhia kwa matamshi yake kwani aliyoyasema ni ya kweli.

Harusi ya mzofafa

Neno ‘mzofafa’ lina maana sawa na maringo au madaha. Harusi ya mzofafa ina maana sawa na harusi iliyonoga kwa mbwembwe na hoihoi. Kwa mfano, Bwana alituandalia harusi ya mzofafa hatutaisahau.

Kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa

Msemo huu una maana kuwa unapewa sifa usizostahili. Msemo mwingine ulio na maana sawa ni kuvalishwa kilemba cha ukoka.

Chezea unyango wa kima

Msemo huu huweza kutumika kuonya mtu dhidi ya jambo fulani. Kwa mfano, “wewe, utakiona leo, nitakuchezesha unyago wa kima”. Inaaminika kuwa kima hucheza ngoma (unyago) ili kuwatoa vigori (wari). Tendo hili hufanyika kwa siri na endapo watagundua umewaona, lazma nawe uchezeshwe. Kwa hivyo, kuwa makini na mambo ya watu, usije ukachezeshwa unyago wa kima!

Bura yangu sibadili na rehani

Huu ni msemo ambao una maana lukuki, baadhi ya watu hutafsiri neno ‘bura’ kama kitu cha tunu kichakavu. Kwa hivyo msemaji wa msemo huu humaanisha kuwa hawezi badili kitu chake cha tunu kwa kipya.

Usiache mbachao kwa msala upitao

Katika msemo huu, wahenga wametumia neno ‘mbachao’ linatamkwa “mbachao,” yaani ni kifaa duni kinachotumiwa kufanyia Ibada, kwa mfano, mkeka au jamvi kuukuu (Kidukwa)..sasa wamesisitiza usije ukauacha kwa “msala” upitao..Msala nao ni mkeka maalumu wa kusalia lakini si duni kama ilivyo m-bachao. Pia, msemo huu una maana sawa na usiyadharau madafu, embe ni tunda la msimu.

Mwanya ni kilema pendwa

Wengi hawafahamu kuwa hata kama mwanya ni kilema, lakini ni kilema kinachopendwa na wengi. Vilema vya aina hii hutambulika kama ‘vilema pendwa’, vipo vingi kwa uchache ni baadhi ya matege ya miguu, makalio makubwa, vifua na misuli mikubwa.

Mungu hakupi kilema akakunyima mwendo

Msemu huu una maana kuwa mtu anapaswa kuridhika na alicho nacho. Funzo kuu ni kuwa haina haja kutamani vitu ambavyo vimezidi uwezo wetu.

Mlevi haukubali ulevi

Msemo huu una maana kuwa hata anywe vipi hakubali kuitwa mlevi. Msemo huu umewalenga mahasidi na mafisadi ambao hukataa chungu ya ukweli.

Chongo kwa Mnyamwezi kwa Mswahili amri ya Mungu

Wengine hutumia neno ‘chogo’ badala ya ‘chongo’, yote heri alimradi haipotoshi maana ya usemi huu.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Oscar Mbuza

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi