loader
Picha

Binti Mtanzania aua mama yake kwa kunyimwa ufunguo wa gari

MSICHANA Mtanzania Caroline Kyara (19) anashikiliwa na Polisi mjini Mazini, nchini Eswati zamani ikijulikana kama Swaziland, kwa tuhuma za kumuua kwa kumchoma kisu mama yake mzazi, Amina Kyara (55), baada ya kunyimwa funguo za gari.

Tukio hilo lilitokea kati ya Oktoba 2 na Oktoba 5, mwaka huu, katika maghorofa ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (SNPF), ambako ndiko nyumbani kwa Amina na familia yake ya watoto watatu ambapo binti huyo ni mtoto wa mwisho.

Taarifa zinasema kuwa mume wa Amina alikuwa Mtanzania Profesa wa Chuo Kikuu nchini Eswati aliyefariki dunia miaka 16 iliyopita na kuzikwa Tanzania na wakati huo alimuacha mwanawe ambaye sasa ni mtuhumiwa akiwa na miaka mitatu.

Naibu Msemaji wa Polisi mjini Mazini (DPICO), Nosipho Mnguni alithibitisha tukio hilo na kusema wanamshikilia binti huyo huku taarifa zaidi zikisema Amina atasafirishwa kuja Tanzania kwa ajili ya maziko yatakayofanywa eneo alikozikwa mumewe.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Grace Mujuma alisema amesikia taarifa hizo ila wanafuatilia tukio hilo ili kupata taarifa rasmi.

Vyombo vya habari nchini Eswati vimeripoti tukio hilo huku vikiwanukuu baadhi ya majirani na ndugu wa Amina kuwa mtuhumiwa alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Eastern Mediterranean nchini Uturuki, akisoma Shahada ya Uchumi Mwaka wa Pili.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema, siku ya tukio ilikuwa pia ndiyo siku ya binti huyo kurudi chuoni, hivyo alijiandaa na kumtaka mama yake ambaye alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi St Joseph ampeleke uwanja wa ndege tayari kwa safari yake ya kurejea chuoni, ila mama yake alimwambia ameshamuita dereva teksi ampeleke.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa binti huyo aliendelea kung’ang’ania mama yake ampeleke au ampe funguo za gari aende lakini mama yake alikataa na kumwambia asubiri kwani dereva teksi ameshaitwa na yuko karibu. Ilidaiwa kuwa baada ya mama yake kusema hivyo, mtuhumiwa aliondoka kwa hasira na kwenda jikoni kisha akarejea na kisu na kumchoma mama yake na kusababisha kifo chake.

Baada ya tukio, mashuhuda akiwepo dereva teksi ambaye alikuwa ameshafika, alisema mtuhumiwa alijifungia ndani na kuvua nguo zote, tukio ambalo hakuna aliyefahamu kwa nini alifanya hivyo, ndipo walipopiga simu Polisi kutoa taarifa na kisha polisi kufika na kuchukua mwili wa marehemu na mtuhumiwa huyo.

“Tulitaka kumuokoa mama dhidi ya ukatili wa binti yake, lakini ilikuwa bahati mbaya kwani nilichelewa kidogo na wakati huo mama alianguka chini huku damu zikivuja kutoka kwenye sehemu ya jeraha la kisu,” alisema dereva huyo ambaye jina lake halikupatikana mara moja.

Vyanzo vya habari nchini humo vinasema kuwa baada ya kifo cha mumewe miaka 16 iliyopita, mama huyo ambaye alikuwa mwalimu kitaaluma, aliamua kuendelea kuishi nchini humo kwa ajili ya kuweza kuwasomesha watoto wake ambao kwa wakati huo wawili walikuwa wakubwa kiasi na mtuhumiwa alikuwa na miaka mitatu. Taarifa zinasema kuwa familia inaendelea na vikao kupanga siku ya kumuaga marehemu nchini humo kabla ya kusafirishwa kuja Tanzania kwa ajili ya maziko.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick na Mashirika

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi