loader
Picha

Athari za wanafunzi kupenda anasa

MBUNGE wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba anawaasa wanafunzi kuzingatia masomo na kuweka kando anasa kwani kuziendekeza ni sumu kwa maisha yao.

Mwigulu anasema siyo tu kwamba anasa hazina faida kwa maisha yao ya sasa ya shule, lakini zitawaweka kwenye wakati mgumu siku za mbele. Dk Mwigulu, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, aliyasema hayo kwenye mahafali ya Shule ya Sekondari ya Tusiime iliyoko Tabata jijini Dar es Salaam.

Mahafali hayo yalifanyika hivi karibuni kwenye viwanja vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Julius Nyerere. Katika nasaha zake, Dk Mwigulu anasema pamoja na ukweli kwamba walimu na uongozi wa shule hiyo ya Tusiime wanawekeza nguvu nyingi kuwafundisha kama, wanafunzi wenyewe wasipotilia maanani masomo nguvu wanazotumia walimu na uongozi wa shule zinaweza zisizae matunda yaliyotarajiwa kwenye mitihani yao.

Dk Mwigulu anasema alianza kuijua Tusiime baada ya kuitwa bungeni wanafunzi 10 bora akiwemo mmoja wa shule hiyo na kisha alitoa nafasi kwa shule hiyo kuchagua wanafunzi wa kutembelea Bunge wakiwa wageni wake.

Mwanasiasa huyo msomi anawaasa wanafunzi kuhakikisha wanafaulu kwa daraja la kwanza na la pili na kwamba yeye binafsi anaamini kwa namna walivyoandaliwa na walimu wao mahiri hana shaka kuwa wana uwezo wa kufaulu kwa madaraja hayo pekee. Kwa wanafunzi wa kike, Dk Mwigulu anawataka wajiweke mbali na vishawishi vya wanaume ambao wanaweza kuwarubini kwa kuwapa vijizawadi vidogo vidogo kama chipsi, wakidhani kuwa wanawapenda sana.

“Anayekupenda ni mzazi wako aliyekusomesha kuanzia chekechea hadi hapo ulipofikia. Sasa akija mtu na chipsi kuku akakudanganya kwamba yeye ndiye anakupenda sana mwongo. Wewe zingatia masomo yako na kwa bahati nzuri mna walimu waliobobea na ambao wana uwezo wa hali ya juu katika kufundisha. Someni kwa bidii,” anasema Mbunge huyo wa Chama Cha Mapinduzi.

“Mzazi amejinyima vitu vingi apate fedha za kukusomesha shule nzuri kama hii na mimi naona hakuna upendo kama huo, hivyo wapeni zawadi wazazi na walezi wenu na zawadi nzuri ya kuwapa ni kufaulu kwa kiwango cha juu cha daraja la kwanza au la pili tu,” anasema. Dk Mwigulu anasema elimu bora kwa mwanafunzi ni silaha ya kumuwezesha kupambana na yanayomkabili mbele ya safari yake ya maisha kwa kujiamini.

Anawaambia kwamba tofauti na miaka ya nyuma, sasa hivi kuna ushindani mkubwa katika soko la ajira iwe kitaifa na hata kimataifa na kwamba aliyeelimika vyema ndiye ataibuka mshindi kwenye soko hilo. Dk Mwigulu pia ameipongeza bodi ya shule hiyo ya Tusiime na uongozi kwa ujumla kwa kuendelea kuwekeza katika elimu kwa kuwa shule hizo kuanzia hatua ya awali, msingi hadi sekondari zimekuwa zikitoa elimu bora inayostahili kwa vijana wa Kitanzania.

Anaamini kuwa uwekezaji unaofanywa na shule hiyo ya Tusiime ni moja ya njia ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi mahiri wa Rais John Magufuli wa kuhakikisha vijana wanapata elimu bora kwa manufaa ya taifa.

Anasema taifa linahitaji vijana wazalendo na wasomi ambao watakuwa wahandisi mahiri, marubani, wanasheria wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya watanzania wote kwa sababu bila elimu nchi haiwezi kupiga hatua katika nyanja zozote zile.

Anasema hata mkakati wa nchi kuelekea kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda ambayo ni moja ya ajenda za serikali ya awamu ya tano haitaweza kufanikiwa bila kuwepo wataalamu wa fani mbalimbali kama uchumi, uhandisi na nyinginezo nyingi.

Anasema taifa halina budi kuwa na wataalamu wa kutosha ili waweze kuwa chachu katika mkakati wa nchi kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 huku msukumo mkubwa ukiwa ni katika uwekezaji wa viwanda na kilimo. Tangu mwaka 2012, wanafunzi wa shule ya Tusiime katika ngazi ya shule ya msingi , sekondari na kidato cha sita wamekuwa wakifanya vizuri kwa takribami asilimia 100.

Mwaka 2013, zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi waliohitimu kidato cha sita katika shule hiyo walipata nafasi katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Tanzania. Tangu mwaka huo wanafunzi wanaokwenda vyuo vikuu kutoka Tusiime idadi yao imeendelea kuwa juu.

Katika matokeo ya shule ya msingi ya mwaka jana, Tusiime iliyokuwa imesajili wanafunzi 200 na wote kufanya mtihani ilikuwa ya kwanza katika wilaya ya Ilala kati ya shule 90, ikawa ya tatu katika mkoa wa Dar es Salaam kati ya shule 433 na ikawa ya 20 kitaifa kati ya shule 9736.

Kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana (CSEE), Tusiime ilikuwa na wanafunzi 59 waliopata daraja la kwanza, 161 wakapata daraja la pili, wanafunzi 62 daraja la tatu, 21 daraja la nne na hakuna aliyepata daraja 0. Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita (ACSEE) mwaka huu 2018, Tusiime ilifanikiwa kutoa wanafunzi watatu katika wavulana kumi bora kitaifa kwa masomo ya Biashara. Wanafunzi hao ni Charles Kanuda, Kelvin Melamari na Josadack Chobaliko.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi