loader
Picha

Wasichana nchi 25 wanyimwa uhuru kutumia simu za mkononi

NCHI 25 duniani, ikiwemo Tanzania zimebainika kuwa na tatizo la wasichana kukosa uhuru wa kutumia simu za mkononi ikilinganishwa na wavulana.

Utafiti uliofanywa na asasi isiyo ya kibiashara ya Girl Effect na Vodafone Foundation unaonesha wavulana wana uwezekano wa kumiliki simu mara 1.5 zaidi, simu janja mara 1.3 zaidi kuliko wasichana.

Utafiti huo unabainisha kuwa chanzo cha tatizo hilo ni upendeleo wa kijamii na vikwazo vingine vyenye kuzuia matumizi ya simu kwa wasichana. Mkurugenzi wa Ufundi na Utafiti wa Kidijiti wa Girl Effect, Kecia Bertermann alisema uhuru wa kutumia simu za mkononi kwa wasichana nchi zinazoendelea ni mdogo kuliko inavyotarajiwa.

“Wakati asilimia 44 tu ya wasichana waliohojiwa katika utafiti walisema wanamiliki simu, zaidi ya nusu asilimia 52 walisema wanapata simu kwa kuazima... “... Hata hivyo, utafiti unaonesha simu zinafanya wasichana kujisikia kutotengwa (50%), kuwa na uhuru wa kupata elimu (47%), kujiburudisha (62%), kuwafunulia habari zilizofichika (26%), na kuwafanya wajiamini (20%),” alisema Bertermann.

Utafiti huo ulitaja nchi 25, baadhi yake ni India, Afrika Kusini, Tanzania, Bangladesh, Nigeria, Malawi na Rwanda ambazo matumizi ya simu kwa wasichana yapo chini. Alisema utafiti huo wa ubora na uwiano, uliofanyika nchi 25, umebaini uhuru wa matumizi ya simu kwa wasichana unadhibitiwa kiasi kikubwa na mazoea ya kijamii yanayozuia kuwa na uhuru sawa na wavulana.

Alisema zaidi ya theluthi mbili sawa na asilimia 67 ya wavulana waliohusishwa utafiti, waliripoti kumiliki simu ikilinganishwa na asilimia 44 ya wasichana na asilimia 28 walisema waliazima ikilinganishwa na zaidi ya nusu asilimia 52 kwa wasichana.

Nigeria, Malawi na Tanzania, wavulana wana uwezekano mkubwa wa kutumia simu kwa shughuli nyingi zaidi kama WhatsApp na Facebook, kutafuta habari kwa mtandao, au kutafuta kazi kuliko wasichana.

Alifafanua kwa upande wa wasichana hutumia simu kwa kazi za kawaida zenye kuhitaji ujuzi na ufahamu mdogo sana, mathalani kuwapigia wazazi wao au kutumia kikokoteo.

Kwa India na Bangladesh, wasichana wanaoonekana kutumia simu, mara nyingi hutazamwa vibaya na wanajamii, kwa maana wazazi wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupiga marufuku matumizi ya simu. “Wasichana ambao huvunja sheria zihusianazo na simu pia wana uwezekano mkubwa wa kuadhibiwa kwa kukemewa, kupigwa, kufukuzwa shule au hata kufungishwa ndoa mapema,” alieleza.

Alisema Malawi na Rwanda ambako upatikanaji wa simu na ujuzi wa wasichana wa teknolojia ni mdogo zaidi, hata wasichana wanaogopa simu zinaweza kufanya ‘wapotee’ kutokana na kuwasiliana na wavulana.

Mkurugenzi wa Vodafone Foundation, Andrew Dunnett alisema: “Wasichana wanaachwa nyuma. Katika nchi nyingi upatikanaji wa simu ni muhimu kwa elimu, maendeleo na afya ya wasichana.

“Tunahitaji kukabiliana na ukweli kwamba wasichana na wavulana hawana uhuru sawa wa kupata simu na huduma za kiubunifu mahususi kwa ajili ya wasichana ili kukidhi mahitaji yao katika muktadha huu.”

Alisema wanahitaji utafiti huo ujulishe na kuunga mkono sekta za teknolojia na maendeleo kukidhi mahitaji ya wasichana kuleta maendeleo ya ukweli katika kufikia Malengo Endelevu ya Maendeleo.

Alisema Vodafone Foundation wakishirikiana na Girl Effect wamedhamiria kuwawezesha wasichana milioni saba katika nchi nane walioathirika na upatikanaji wa huduma wanazohitaji kupitia simu.

Alisema wakishirikiana na washirika na wafadhili wengine, lengo lilikuwa kukusanya fedha zinazofikia hadi jumla ya dola za Marekani milioni 25 katika kipindi cha miaka mitano, ukiwamo mchango wa dola za Marekani milioni tano kutoka kwa Vodafone Foundation ili kufikia malengo haya makubwa.

Utafiti huu ni wa kwanza wa aina yake unaowahimiza viongozi katika tasnia za maendeleo na teknolojia kutambua vikwazo vya kijamii vinavyokwaza wasichana kuwa na uhuru wa kutumia simu za mkononi.

SERIKALI inafi kiria kulibadilisha Baraza la Taifa la Hifadhi na ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi