loader
Picha

Miaka 150 uinjilishaji Tanzania, historia fupi ya TEC

“MIAKA 150 ya Uinjilishaji inazidi kutupa hamasa kwa kazi nyingi zinazofanywa na zinazoendelea kufanywa na viongozi wa dini. Tuzidi kudumisha umoja, amani na mshikamano… Mungu Wetu ni Mungu wa Amani, hivyo tuzidi kushirikiana katika ujenzi wa amani hiyo ambayo ni tunu kutoka kwake.”

Ndivyo anavyoandika Katibu Mtendaji wa Tume ya Uhusiano na Dini Mbalimbali wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Benedict Shemfumbwa kuhusu ‘Historia Fupi Juu ya Dini Mbalimbali na Mahusiano Yao Nchini Tanzania’ kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara.

Maadhimisho haya yanaanza leo Novemba 2 hadi Novemba 4, 2018, huko Bagamoyo katika Jimbo Katoliki la Morogoro (Kiserikali Bagamoyo ipo mkoani Pwani). Hii ni sehemu inayoaminika kuwa Mlango wa Imani Afrika Mashariki. Ilikuwa kituo cha kukusanyia watumwa kabla ya kupelekwa Zanzibar kwa meli.

Katika mazungumzo na wanahabari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo anasema: “Kanisa Katoliki limekuwapo nchini kwa miaka 150, lakini siyo kwamba wamisionari wa kwanza walifika kwa miaka hiyo tu, kabla walishuka visiwani Zanzibar katika utawala wa awali wa Waarabu walipotawala nchi kama wageni na makao yao yakiwa Zanzibar.

Anasema hao pia walikuwa na shughuli nyingine walizofanya Bara hasa Dar es Salaam (Dari Salama) yaani nyumba salama.

“Ndiyo maana sultani alipotaka kupumzika kutoka Zanzibar, alifika Dar es Salaam wanapoishi wamisionari wa White Fathers (Wamisionari wa Afrika); hiyo nyumba haijafanyiwa mabadiliko,” anasema Kardinali Pengo.

Anasema Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu waliona licha ya ubaya wa biashara ya utumwa, pia inaweza kuwa mlango wa kuinjilisha.

Anaongeza: “Mwanzoni walionekana kama waliotaka kufaidi biashara ya watumwa, lakini lengo lao lilikuwa kuwapata waliokuwa watumwa ili kuwafanya watu huru kuendesha maisha yao, hivyo hawakununua watumwa ili wawatumikishe katika mashamba, bali wahusiane na kujenga imani.”

Ndipo wakaanzisha kijiji kandokando ya eneo lile walilofikia na kusimika msalaba katika Kijiji cha Maria na licha ya kupandikiza msalaba, pia walikuwa na imani kuhusu nguvu wanayoweza kupata kupitia Maria; Mama wa Yesu.

Anasema: “Katika kijiji hicho wakaamua kulea na kuelimisha watumwa hao kuhusu kusoma, kuandika, ujenzi, mapishi na mambo mengine mengi muhimu.”

Waliokamatwa kutoka sehemu mbalimbali zikiwamo za Tabora na maeneo mengine ya mwambao, wakawa wanaongozana na wamisionari ili kutafsiri kwa ajili ya watu wengine lugha za makabila mbalimbali ili kuwaunganisha na watu wa asili kutokana na hao kuwa wameandaliwa hapo Bagamoyo.”

Anasema Kanisa limeendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii zikiwamo za elimu na afya hata katika maeneo yaliyokuwa hayajafikiwa na huduma hizo.

Inaelezwa kuwa, wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu walisimika msalaba katika fukwe za Bagamoyo Machi 3, 1868.

“Mwaka huo huo pia, ndipo lilipozaliwa Shirika la Wamisionari wa Afrika ambalo limekuwa kundi la pili la wamisionari kuunga mkono kazi ya Uinjilishaji Tanzania Bara. Hawa, walifika Bagamoyo wakiwa na miaka 10 ya uhai kama shirika.

Kimsingi,makundi matatu ya wamisionari yalichukua njia tofauti kuingia Tanzania Bara.

Kazi ya uinjilishaji ilianza na mbegu ya imani ikapandwa katika maeneo mbalimbali. Kanisa likaanza kuonekana katika sura yake kuanzia mbatizwa wa kwanza hadi pale eneo fulani lilipokidhi kuwa na hadhi ya vikarieti au jimbo.

Wengi wa maaskofu na wasimamizi wa kitume walioteuliwa na Baba Mtakatifu wakati huo, walitoka miongoni mwa wanashirika lililokuwa linafanya umisionari katika eneo husika.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini katika andiko lake la Mwanzo wa Uinjilishaji Tanzania anasema: “Zanzibar ndio ulikuwa mlango wa kuingia Afrika Mashariki hasa Tanzania Bara kwa sababu tangu mwaka 1856 Tanzania Bara hasa sehemu ya Pwani na vituo vya njia za biashara hadi Kongo na Maziwa makuu ilikuwa chini ya utawala wa Sultani wa Zanzibar.”

Anasema, Sultani alifanikiwa kudhibiti njia kuu za biashara ingawa hakukuwa na pesa wala nguvu za kiutawala Tanzania Bara kikamilifu. Hata hivyo kabla ya ukoloni wa Wazungu, isingewezekana kuinyemelea na kuingia ndani zaidi bila idhini yake.”

Padri Benedict Shemfumbwa katika mada kuhusu ‘Historia Fupi Juu ya Dini Mbalimbali na Mahusiano yao Nchini Tanzania’ anaandika: “Jambo moja kubwa na la kujivunia ni pale wamisonari wa Shirika la Roho Mtakatifu walipomtembelea Sultani Sayyed Majid katika jumba lake lililojulikana kama Beit el Ajab naye aliwauliza: “Mnataka kufanya nini hapa?”

Wamisionari wakamjibu: “Tumekuja kuwahudumia wagonjwa, kusaidia maskini, kufundisha watoto na kufundisha ujuzi wa namna mbalimbali.”

Sultani akasema: “Karibuni sana; nyumba yangu ni nyumba yenu, watu wangu ni watu wenu, na mimi ni ndugu yenu.” Mwanzo huu ulikuwa mzuri na wa kuigwa katika uhusiano baina ya Wakristo na Waislamu na moyo huu unapaswa kuendelezwa.

Kiutendaji kila askofu alikuwa na mamlaka kamili katika eneo lake akiwajibika moja kwa moja kwa Baba Mtakatifu na kufuata miongozo ya utume wa kanisa na ile ya shirika lake.

Kanisa la Tanzania linazidi kukua Maendeleo ya jamii nayo yakaonekana wazi na hivyo kuyafanya mawasiliano kuwa nafuu. Taratibu, msukumo kutoka kwenye mipaka ya mashirika na kuunda utendaji wa pamoja ukaanza kujitokeza.

Chanzo kinasema: “Ndoto hii ilikuwa hai pale ambapo maaskofu wapatao sita kutoka mashirika mbalimbali walipojitokeza kuhudhuria mkutano wa kwanza wa aina yake uliofanyika Dar es Salaam Julai 1912.”

Ingawa kumbukumbu hazimtaji wazi askofu aliyetoa wazo la kuwa na mkutano huo, mazingira yanaonesha kuwa huenda ni Askofu Spreiter wa Dar es Salaam aliyewaalika.

TEC inawataja waasisi hao wa Baraza la Maaskofu kuwa ni pamoja na Askofu Thomas Sporeiter, OSB wa Dar es Salaam, Askofu Aloyce Munsch, C.SSp wa Kilimanjaro, Msimamizi wa Kitume, August van Waesberghe, M. Afr, Vikarieti ya Tanganyika, Msimamizi wa Kitume, L. Bernhard, CSSp, Vikarieti ya Zanzibar na Msimamizi wa Kitume, Pfeffermann, Vikarieti ya Unyanyembe.

Katika mkutano huo, waliweka misingi ya mikutano mingine na kwamba angalau mikutano ya namna hiyo ifanyike kila baada ya miaka mitano na wakaazimia mkutano wa pili ufanyike Tabora mwaka 1915, lakini kukaibuka Vita ya Kwanza ya Dunia kabla ya kutekeleza mkutano huo.

Utekelezaji ulitimia mwaka 1925 baada ya kupatikana utulivu wa kisiasa. Vita na matokeo yake vilizaa changamoto nyingi za kichungaji, kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Ikumbukwe kuwa, mwisho wa Vita ya Kwanza ya Dunia ilikuwa mwisho wa utawala wa kikoloni wa Mjerumani na kuingia utawala wa Mwingereza.

“Utawala mpya ulikuja na sura mpya za mahusiano na taasisi za kimisionari hususan katika suala la utoaji elimu.” “Haikuwa rahisi wamisionari kupokea mfumo mpya wa kisekulari katika kuendesha taasisi zao za elimu. Kukaibuka hitaji la kipekee la maaskofu kukutana kujadili changamoto hii,” linasema TEC.

Inaelezwa kuwa mkutano wa tatu uliitishwa na Mjumbe wa Baba Mtakatifu aliyetumwa kutembelea nchi za Kiafrika zilizokuwa chini ya Utawala wa Mwingereza na ukafanyika Dar es Salaam mwaka 1928.

Uliweka mwongozo thabiti wa umuhimu wa kujikita katika utume wa elimu na kuweka miongozo iliyowezesha utendaji wa maaskofu kwa miongo miwili na nusu iliyofuata. Wakakubaliana kuwa na mikutano mikuu kila baada ya miaka mitatu, badala ya mitano.

Kumbukumbu za Mkutano wa Wakuu wa Misioni Tanganyika wa Mwaka 1928 zinaonesha kuwa, ni katika mkutano hu ndipo Askofu Hinsley alipotamka kwamba: “Kama kunatokea mjadala wa kufanya uamuzi wa nini kifanyike kati ya kujenga kanisa au shule, basi shule ipewe kipaumbele.”

Kwa kauli hii, utume wa elimu uliwekwa kama moyo wa mashirika ya kimisionari katika maeneo yao. Kadhalika, mfumo wa vikao vya maaskofu ulianza kujengeka. Kuzaliwa kwa TEC Vita ya Pili ya Dunia nayo iliacha changamoto nyingi zilizohitaji nguvu ya pamoja ya maaskofu.

Mkutano wa mwaka 1956 uliona ni vema maaskofu kuunda chombo rasmi cha kitaifa cha Maaskofu Katoliki na kuwa na ofisi ya kudumu katika makao makuu ya nchi. Kikaundwa chombo kilichoitwa Tanganyika Catholic Welfare Conference (TCWC) makao yake yakiwa Dar es Salaam.

Jina la Baraza hilo limepita katika mabadiliko kadhaa kutoka TCWC mwaka 1956, mwaka 1961 likabadilika na kuwa Tanganyika Episcopal Conference (TEC) na sasa Tanzania Episcopal Conference (TEC) toka mwaka 1965.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka maofi sa habari, uhusiano na ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi