loader
Picha

Watanzania 8 waokolewa ukahaba nje ya nchi

WANAWAKE wanane wa Kitanzania na wengine 16 kutoka nje ya nchi, wameokolewa kufanya biashara ya ukahaba, baada ya kudanganywa kuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa lengo la kupatiwa kazi nzuri.

Aidha, kati ya wanawake hao wanane wa Kitanzania, wawili wanawasili leo saa saba mchana wakitokea Thailand, ambako walikuwa wakifanyishwa kazi hiyo ya ukahaba. Kamishna Msaidizi Magereza aliyeko katika Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji wa Haramu wa Binadamu, Ahmed Mwendadi alisema hayo jana kwenye mafunzo ya majaji kuhusu masuala ya kupambana na usafirishaji huo haramu wa binadamu jijini Dar es Salaam.

Mwendadi alisema wanawake hao wanane wa Kitanzania kati ya hao wanne walitolewa nchini India na wanne nchini Thailand, ambapo kati ya hao wanne, wawili wanafika leo mchana saa saba. “Wanaotoka nje kuja Tanzania tumewahi kuokoa wanawake 12 kutoka nchini Burundi waliokuwa wanapita kwenda Uarabuni pamoja na Wanyarwanda wanne ambao walikutwa mkoani Singida wakifanyishwa kazi za nyumbani,” alisema Mwen-dadi.

Alisisitiza kuwa Sekretarieti hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, imebaini kuwa wanawake wengi wamekuwa wakisafirishwa nje ya nchi ya Tanzania kwa ajili ya kufanyishwa kazi ya ukahaba katika nchi za India, Thailand, Malasia pamoja na Indonesia. Aliitaja mikoa inayoongoza kwa usafirishaji wa biashara hiyo ya binadamu kuwapeleka nje ya nchi kuwa ni Dar es Salaam, Tanga, Kigoma, Mwanza, Shinyanga, Singida na Dodoma hususan katika wilaya ya Kondoa.

“Hatua tunazochukua ni kufanya utafiti ili kubaini hayo, ikiwa ni pamoja na kutoa uelewa kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria pamoja na mbinu za kuwagundua wahanga. Pili kutoa elimu kwa umma,” alisema. Alisema wanatarajia kuanza kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kutoa elimu, ikiwamo jitihada kubwa ya serikali kuzuia pasipoti za makundi, lengo likiwa ni kuzuia watu wasiingie katika biashara haramu.

Alisema serikali pia imechukua hatua ya kunyang’anya leseni kampuni zote zilizosajiliwa kutafutia kazi Watanzania nje ya nchi. Alisema nchini mpaka sasa kesi 23 za biashara hiyo haramu, zinaendelea mahakamani na kesi saba zimeshatolewa hukumu. Awali, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kupambana na Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, Adatus Magere alisema takwimu halisi za matukio hayo mpaka sasa hawana japo tatizo hilo lipo.

“Hili ni tatizo kubwa hapa nchini kwa sababu uhalisia unapoajiri binti kutoka kule Iringa kuja Dar es Salaam kwa tafsini ni usafirishaji wa binadamu kwani ujira unaomlipa wa kazi na pesa unayolipa hailingani na kazi anazozifanya,” alisema Magere. Alisema biashara hiyo ipo katika maeneo mawili nchini; watoto wadogo wanatolewa mikoani kuletwa katika miji mikubwa kwa ajili ya kutumikishwa katika kazi, wengi wao hawaelezwi ukweli wanakwenda kufanya nini matokeo yake wanaishia kwenye ukahaba.

“Wale ambao wanasafirishwa ni waathirika wanapochukuliwa wanapewa hadhi ambayo si kweli. Wakishachukuliwa na kwenda Uarabuni, Pakistan, India, China matokeo yake wanaishia kutumika katika Danguro,” alisema. Alisema wadau wakubwa wa jambo hilo ni polisi, magereza, ustawi wa jamii, uhamiaji na majaji kwani wana mpango kazi unaoshirikisha wadau wengi katika kupambana na biashara hiyo.

Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Temeke, Karim Mushi alisema mafunzo wanayoyapata yana mchango mkubwa yatawasaidia, kwani biashara haramu inahitaji uelewa mkubwa kwa wahusika wote.

Akimwakilisha Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Jaji wa Kanda ya Mashariki Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, Beatrice Mutungi alipongeza jitihada zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Kitengo cha Usafirishaji Haramu wa Biashara ya Binadamu kwa kutoa elimu kwa wasimamizi wa sheria ili kuwaongezea elimu na maarifa zaidi wa kufanya kazi kwa ufanisi.

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais (Menejimenti ya Utumishi ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi