loader
Picha

Neema yawashukia pacha waliotenganishwa Muhimbili

WATOTO pacha wa jamii ya Kimasai waliotenganishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, wameruhusiwa kutoka hospitali na zaidi wakileta neema kwa wazazi wao baada ya nyumba ya familia hiyo kukarabatiwa kwa lengo la kuiweka katika mazingira mazuri ya watoto hao kuishi. Aidha, zaidi ya Sh milioni 34 zimetumika kufanikisha upasuaji huo na gharama mbalimbali zilizohusisha matibabu na huduma nyingine tangu walipofika kwa mara ya kwanza hospitalini hapo Julai 13, mwaka huu.

Pacha hao waliozaliwa Julai 12, mwaka huu katika Kijiji cha Kigogo wilayani Kisarawe mkoani Pwani wakiwa wameungana kuanzia tumboni, walifanyiwa upasuaji wa huo wa mafanikio Septemba 26, mwaka huu, baada ya kupokewa kutoka Hospitali ya Kibaha pamoja na mama yao, Esther Simon (22) aliyezalishwa na mkunga wa jadi.

Mbali na ukarabati wa nyumba hiyo unaotarajiwa kufanywa na United Bank For Africa (BOA) utakaogharimu kiasi cha Sh milioni 18, watoto hao Precious na Grecious, pia wamekatiwa bima ya miaka 10 pamoja na kufunguliwa akaunti maalumu iliyowekwa kianzio cha Sh milioni mbili zilizochangwa na wafanyakazi wa benki hiyo.

Pia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenyewe imeahidi kuendelea kuwahudumia bure watoto hao hadi watakapotimiza umri wa kujitegemea, mbali na huduma nyingine ambazo watoto hao na familia hiyo kwa ujumla imenufaika nazo kwa kipindi chote walichokuwa wakipata matibabu hospitalini hapo.

Kutenganishwa kwa watoto hao kunaifanya hospitali hiyo kujenga historia ya pili kwa kufanya upasuaji baada ya operesheni kama hiyo iliyofanyika mwaka 1994 ambayo hata hivyo kwa mujibu wa hospitali hiyo, mmoja wa watoto waliokuwa wametenganishwa, alifariki baadaye baada ya kuruhusiwa kutoka hapo.

Akizungumza wakati wa kuwaaga sambamba na kuwakabidhi misaada hiyo jana, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema kuruhusiwa kwa watoto hao kunatokana na uchunguzi wa kina ulioonesha kuwa kwa sasa wapo salama.

Profesa Museru alisema kwa kipindi chote ambacho watoto hao walikuwa wamefanyiwa upasuaji huo, timu ya madaktari ilikuwa ikiendelea kufuatilia afya za watoto hao hadi kule ambapo familia hiyo inatoka kwa lengo la kuondoa uwezekano wa watoto hao kupata madhara yoyote yanayoweza kujitokeza.

“Timu yetu ilipokwenda kufuatilia ilijiridhisha kuwa mazingira ya familia wanakotokea watoto hao siyo mazuri na kwamba yasingeweza kufaa watoto hawa kwenda kuishi na ndipo tukapata wazo la kuwatafuta wadau mbalimbali ili watusaidie katika hili, nawashukuru UBA, kwa kuitikia mwito huo,” alisema Museru.

Aidha, Profesa Museru alisema baada ya familia hiyo kupata msaada huo wa kukarabatiwa nyumba yao, anaamini watoto pacha hao kwa sasa watakuwa katika hali ya usalama wakati ambao pia hospitali hiyo pia itaendelea kuwa karibu nao na kuwapa huduma mbalimbali pale itakapohitajika.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji Watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Petronila Ngiloi alisema uchunguzi uliokuwa umefanywa ulibaini kuwa watoto hao walikuwa wameungana sehemu kubwa ya ini na ikaonekana upasuaji huo unaweza hospitalini hapo.

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais (Menejimenti ya Utumishi ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi