loader
Picha

5% wakutwa homa ya ini, wabunge 100 wapima

TAASISI ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) jijini Dar es Salaam imepima watu 1,200 maambukizi ya homa ya ini B na C (Hepatitis B,C) na kati yao 62 ambao ni sawa na asilimia 5.2 wamekutwa na maambukizi ya kirusi hicho.

Aidha, wakati upimaji huo ukiendelea katika taasisi hiyo, kambi nyigine ya upimaji ugonjwa huo iko bungeni Dodoma na tayari wabunge 100 wamejitokeza kupima. Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani katika taasisi hiyo, Dk Chrispine Kahesa alisema jana kuwa mwitikio wa watu unazidi kuwa mkubwa watu wengi wanajitokeza kupima na kupata chanjo na tangu juzi wameanza kuwapima wabunge.

“Idadi ya watu waliokuwa wakijitokeza wakati tunaanza huduma hii Septemba mwaka huu watu waliokuwa wakijitokeza kwa siku ilikuwa hawazidi kumi, lakini sasa wanafika hadi 40, na sasa tumeamua kwenda hadi Dodoma kwa wabunge nao wanajitokeza sana,” alisema Dk Kahesa.

Septemba mwaka huu, taasisi hiyo ilitangaza kutoa huduma ya upimaji virusi vya homa ya ini aina A na B pamoja na kutoa chanjo kwa gharama ya Sh 20,000, ikiwa ni sehemu ya kuzuia saratani ya ini. Virusi hivyo husababisha mtu kupata saratani ya ini. Dk Kahesa alisema kwa Dodoma kambi hiyo ya utoaji wa huduma ya upimaji, chanjo pamoja na kutoa elimu juu ya ugonjwa huo itafanyika kwa wiki mbili kuanzia juzi.

Alisema watu wanaojitokeza asilimia 63 ni wanawake na watu wengi ni rika la vijana, watu wazima hawana muamko mkubwa. Aidha, alisema kuwa watu ambao wanakwenda kwa ajili ya huduma hiyo na kukutwa na maambukizi, ni wale ambao wamezoea kupima magonjwa mbalimbali, hawana hofu na hivyo walikwenda kwa ajili ya chanjo wakiamini kuwa hawajapata maambukizi.

“Wengi wanaokuja hapa ni wazoefu, yaani wanajiamini kuwa ni wazima wanasema wamekuja kupata chanjo, lakini tukipima tunakuta kuwa wameshapata maambukizi, inakuwa ni vigumu sana kwao kupokea majibu lakini tunawapa ushauri wanapokea vizuri tu,” alisema. Hata hivyo, alisema ikipangwa kwa aina ya kazi, watumishi walioko katika sekta ya afya asilimia 10 yao wamekutwa na maambukizi hayo.

“Watu walioko katika sekta ya afya ni watu ambao tunasema wako hatarini zaidi kupata maambukizi haya kwaajili ya mazingira ya kazi zao, ndio wanaowahudumia wagonjwa hawa kwahiyo ni vizuri wakajitokeza kupima na kupata chanjo,” alisema Dk Kahesa. Maulid Tarimo ni mmoja ya vijana ambao wamejitokeza kupima na kupata chanjo ya ugonjwa wa homa ya aini, alisema kilichomsukuma kwenda hospitali kwa ajili ya huduma hiyo ni baada ya watu wawili aliokuwa akifanya nao kazi kupoteza maisha kwa nyakati tofauti kutokana na ugonjwa huo.

“Mwaka 2015 wenzetu wawili walikufa kutokana na ugonjwa huu, waliugua sana mpaka wakapelekwa India ndio tukajua tatizo lao, basi baada ya hapo nimekuwa nikisoma huku na huko kutafuta ambapo nitapata chanjo hii,” alisema Tarimo.

Ugonjwa wa homa ya ini ni hatari na maambukizi yake ni kama ilivyo kwa ugonjwa wa Ukimwi, hata hivyo serikali kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inatoa dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo kwa wagonjwa ambao wamepima na kubainika kuwa navyo ili virusi hivyo visiweze kushambulia ini. Hata hivyo, inaelezwa kuwa, kuna uwezekano mtu kuwa na virusi hao lakini mwili wake ukawa na uwezo wa kuvishambulia na kuvimaliza bila kutumia tiba yoyote.

SERIKALI inafi kiria kulibadilisha Baraza la Taifa la Hifadhi na ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi