loader
Picha

Barabara za pembezoni kupunguza athari za mafuriko, foleni

UJENZI unaoendelea wa barabara za pembezoni au kama ilivyozoeleka kuitwa barabara za mitaani katika Jiji la Dar es Salaam, utasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la mafuriko na msongamano wa magari nyakati za mvua au masika. Kutokana na uharibifu wa barabara hizo, baadhi yake ziligeuka kuwa mifereji ya kupitishia maji wakati wa mvua, hivyo kuongeza msongamano wa magari kwenye barabara kuu za Jiji.

Katika wilaya zote za Dar es Salaam, tunashuhudia wakandarasi wakiendelea na ujenzi wa barabara hizo tena kwa ubora wa hali juu. Nasema ubora wa hali ya juu kwa sababu mbali na ujenzi wa barabara zenyewe, lakini pia tunashuhudia aina ya mitaro ya kupitishia maji inavyojengwa. Aina hii ya ujenzi ni muhimu kwa Jiji hili kwa kuwa baadhi ya wakazi wake, waligeuza mitaro ya barabara kuwa sehemu za kutupa takataka, hali iliyosababisha mitaro mingi kuziba na kusababisha mafuriko kwenye makazi ya watu.

Wakati wa akizungumza kwenye Kongamano la kujadili hali ya uchumi na siasa nchini Tanzania katika kutathimini miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni, Rais John Magufuli alisema kuwa Serikali yake imetenga Sh bilioni 660 kwa ajili ya ujenzi wa barabara jijini Dar es Salaam.

Dk Magufuli alisema kuwa kutokana na fedha hizo, wananchi wanashuhudia ujenzi wa barabara za pembezoni kila mahali katika Jiji hili. Alisema Serikali yake imejipanga kuboresha na kuimarisha miundombinu ya barabara jijini hapa. Mpango huu wa Serikali umekuja wakati mwafaka kwa kuzingatia ukweli kwamba barabara nyingi za pembezoni katika Jiji hili zilikuwa kikwazo kwa wasafiri wanaotumia daladala na magari binafsi, lakini pia zilikuwa hatarishi kwa sababu wakati wa mvua ilikuwa vigumu kutofautisha barabara na mto, maana maji yalikuwa yakifunika barabara na kukimbia mithili ya mto.

Kutokana na uwekezaji huu ambao Serikali unaufanya kwenye barabara za Dar es Salaam, natamani kuona wananchi wakizitumia vizuri kwa kutovunja mifuniko ya mifereji hasa kwa madereva kupaki magari juu yake, wananchi kutotupa takataka juu ya mifereji hiyo au kukata barabara kwa ajili ya kupitisha mabomba ya maji. Miongoni mwa barabara ambazo zilikuwa kero kubwa wa wananchi ni barabara zinazoingia na kutoka kituo cha mabasi ya daladala cha Makumbusho pamoja na barabara ya Tandale Uzuri.

Barabara hizo zilikuwa kero kubwa kutokana na mashimo makubwa yaliyokuwepo, lakini pia magari kukwama nyakati za mvua, na waenda kwa miguu kumwagiwa maji machafu na wenye magari, hali ambayo leo huwezi kuikuta tena Makumbusho kutokana na ubora wa barabara zilizojengwa. Kwa kuwa Serikali imeamua kutenga Sh bilioni 660 kwa Jiji la Dar es Salaam, ombi langu kwa Serikali ni kwamba, ujenzi huu pia uende sambamba na kujengwa upya kwa baadhi ya madaraja kwenye maeneo korofi kama vile daraja lililopo Tandale kwa Mtogole.

HIVI karibuni Wizara ya Nchi Ofi ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi