loader
Picha

Walipwa mamilioni Dar kupisha mradi mwingine mabasi ya mwendo kasi

BAADA ya mafanikio makubwa katika awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam ambao ni wa kwanza na wa kihistoria katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), awamu ya pili iko mbioni kuanza.

Uhakika wa kuanza kwa awamu ya pili umekuja baada ya serikali kuanza kulipa fidia katika awamu ya pili ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) utakaohusisha barabara za Kilwa, Kawawa, Sokoine, Gerezani,Bandarini na Chang’ombe yenye urefu wa kilometa 20.3.

Imeelezwa kuwa, walipwa fidia 104 wanaostahili wameanza kulipwa kupitia benki na wakishamaliza, ujenzi utaanza kwani tayari mkandarasi amepatikana.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo akiwasilisha bungeni mapitio, makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2018/19, alisema ujenzi wa miundombinu ya DART ya Mbagala na Gongo la Mboto, umepangwa kuanza Desemba mwaka huu.

Alisema mradi huo utatekelezwa kupitia mkopo wa dola za Marekani milioni 141.71 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Aidha, kwa awamu ya tatu ya ujenzi (kwenda Gongo la Mboto), utahusisha barabara za Nyerere, Uhuru, Bibi Titi, Azikiwe, Shaurimoyo, Lindi na Maktaba zenye urefu wa kilometa 23.6 kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 148.2 kutoka Benki ya Dunia.

Akizungumza na gazeti hili, Meneja Uhusiano wa Wakala wa DART, William Gatambi alisema walioainishwa kulipwa fidia ni 104 na baada ya kukamilisha malipo ujenzi utaanza.

Awali, DART kupitia Mtendaji Mkuu wake, Ronald Lwakatare katika tangazo lake kwa umma lililotolewa jana liliwataka wananchi walioguswa na mradi huo katika barabara ya Kilwa, Dar es Salaam kuwasilisha nyaraka muhimu kwa ajili ya ulipaji fidia.

“DART tunaendelea na ulipaji fidia kwa wananchi hao ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya awamu ya pili ya mradi kuanzia katikati ya jiji la Dar es Salaam hadi Mbagala Rangi Tatu na Barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni, barabara ya Chang’ombe, Mgulani hadi makutano ya barabara za Kilwa eneo la Mgulani JKT,” alisema.

Aliwakumbusha wananchi waliothaminiwa nyumba zao kwa ajili ya kulipwa fidia, lakini hawajajitokeza mpaka sasa, kuchukua barua zao za utambulisho wa mlipwa fidia kutoka kwa wenyeviti wa serikali za mitaa yao ili waweze kulipwa fidia husika.

Alisema barua za utambulisho wa mlipwa fidia pamoja na maelekezo ya nyaraka nyingine zinahitajika kwa ajili ya ulipaji wa fidia yatatolewa na wenyeviti wao wa mtaa. Lwakatare alisema wananchi wanaohusika katika malipo hayo ni waliothaminiwa nyumba zao chini ya mradi wa DART katika mitaa ya Mianzini, Misheni na Keko katika barabara ya Chang’ombe/Mgulani.

Waziri Jafo akizungumzia usanifu wa awamu ya nne ya ujenzi wa miundombinu hiyo ya DART, alisema utafanyika kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 97.9 kutoka Benki ya Dunia.

Usanifu utahusisha barabara za Sam Nujoma, Bagamoyo, Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi zenye urefu wa kilometa 25.9. Malengo mengine ya DART ni ujenzi wa maegesho katika maeneo ya mfumo wa wakala; kukamilisha taratibu za upatikanaji wa mtoa huduma wa pili (SP2), mkusanyaji nauli, msimamizi wa fedha pamoja na mshauri mwelekezaji kwa ajili ya awamu ya tatu.

Aidha, usanifu wa ujenzi wa miundombinu ya DART, utakaohusisha barabara za Sam Nujoma, Bagamoyo, Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi zenye urefu wa kilometa 25.9, pia unaanza mwaka huu wa fedha.

Kwa awamu ya kwanza, serikali imeshirikiana na Benki ya Dunia kujenga miundombinu mbalimbali inayotumiwa na mabasi hayo kwa ujenzi wake kuhusisha barabara zenye jumla ya kilometa 20.9 ambazo ni Kimara – Kivukoni, Magomeni – Morocco na Faya – Karikaoo.

Mradi huo wa awamu ya kwanza umetoa huduma kwa majaribio kutumia kampuni ya UDART kwa zaidi ya miaka miwili sasa wanajielekeza katika kutoa huduma kimataifa kwa kutangaza zabuni ili kumpata mtoa huduma wa kimataifa katika ushindani atakayepatikana Machi mwakani.

Mtoa huduma huyo atakayeendesha usafiri huo kwa kushirikiana na kampuni ya mabasi hayo iliyoendesha mradi katika wakati wa mpito UDART itawezesha mabasi hayo ya kasi kuongezeka kutoka 140 yaliyopo sasa na kufikia 305 hivyo kuongeza tija ya usafiri huo jijini Dar es Salaam.

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga ameonesha kukerwa na ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi